Stephano
Simbeye, wananchi
ssimbeye@mwananchi.co.tz
MLOWO: Jeshi
la polisi mkoani Songwe limeingia dosari baada ya askari wa kituo cha polisi
Mlowo kudaiwa kumpiga na kumuua mkazi wa
eneo hilo Stanslaus Kalinga (42) kitendo ambacho kimesababisha kuzuka kwa
vurugu kati yake na wananchi waliogoma kuuzika mwili wa kijana huyo
Vurugu hizo
zimetokea jana Agosti 28 mwaka huu ambapo inadaiwa kuwa kifo cha kijana huyo
kinatokana na kipigo cha askari wa jeshi hilo waliokuwa doria usiku wa kuamkia
Agusti 26 mwaka huu saa nne usiku katika eneo hilo wakati mwananchi huyo
akirejea nyumbani kwake kasha kukamatwa
kwa kosa la uzembe na uzurulaji.
Mmoja wa wananchi hao Ibrahim Chimela alisema kuwa
kilichowafanya wakatae kuuzika mwili huo ni kupinga utaratibu unaotumika
kuwakamata wananchi wakati wa doria kuwa si mzuri kwa kuwa doria huanza mapema
kitendo kinachoonekana kama usumbufu kwao, hivyo hawako tayari kuzika hadi pale
wahusika wa kitendo hicho watakapo chukuliwa hatua.
Alisema kitendo cha askari polisi
kituo cha Mlowo kuanza doria mapema kinawaletea usumbufu kutokana na kuwa muda
huo wanakuwa bado wanaendelea na shughuli zao za kibiashara Lakini wamekuwa
wakikatishwa.
Naye Martha Khalid alisema jeshi la
polisi liweke muda muafaka wa kuanza doria ili kuepusha msuguano unaoweza
kujitokeza kati ya jamii na jeshi hilo kwa kuwa wapo ambao wamekuwa wakikamatwa
wakati wakitoka katika shughuli zao za kibinadamu za kila siku na kulitaka
jeshi la polisi kuwashirikisha viongozi wa ulinzi shirikishi ambao wanawafamu
vyema wananchi hao.
Kwa upande wake diwani wa kata ya Mlowo
Sebastian Kilindu akizungumzia tukio hilo alisema kuwa kinachotakiwa ni
kufuata utawala bora kwa raia na polisi kutojichukulia sheria mkononi ili
kuepusha mgongano huo huku akilitaka jeshi hilo kurudi kwa wananchi ambao ndiyo
wenye uwezo wa kuwatambua wahalifu na kulisaidia jeshi la polisi.
Mwakilishi wa ukoo wa marehemu huyo George
Tweve akizungumzia tukio hilo alisema kuwa wao kama familia wamelipokea kwa
masikitiko suala hilo kwa kuwa ni tukio la ghafula na kijana huyo alikamatiwa
upenuni kwake na hakuwa na rekodi za uhalifu hivyo jeshi la polisi liwe na
ushirikiano na viongozi wa kijiji ili kuepusha matukio kama hayo.
Akithibitisha tukio hilo kamanda wa
polisi mkoani Songwe Mathiasi Nyange alikiri tukio hilo kutokea lakini alisema
kwamba kijana huyo alifia hosipitalini na si katika kituo cha polisi na
kuongeza kuwa wanaendelea na uchunguzi kubaini kilichosababisha kifo chake na
uchunguzi ukikamilika atatoa taarifa kamili.
Kaimu Mganga mkuu wilayani Mbozi
ambaye pia ni Katib u wa Afya Theotim mwamwongi alipotakiwa kuzungumzia suala
hilo alisema suala hilo linashughulikiwa kimkoa hivyo hana mamlaka ya
kulisemea.
Hata hivyo jitihada za mwandishi wa
habari hizi hazikuzaa matunda wakati akitaka kuwaona viongozi wa mkoa akiwemo
mkuu wa mkoa, hawakuweza kupatikana kutokana na kuwa walikuwa katika kikao cha
kamati ya ulinzi na usalama.
Aidha siku ya leo bado wakazi wa
Mlowo wameshikiria msomamo wao ule ule na kuwa Mbunge wa jimbo la Mbozi na
Diwani wa kata ya Mlowo walikuwa ndani ya kikao cha kamati ya ulinzi na usalama
kujaribu kupata suluhu ya jambo hilo.
Hili ni tukio la kwanza la kifo
chenye utata kikihusisha Jeshi la Polisi mkoani hapa na kusababisha vurugu
ambazo zilisababisha Polsi kulazimika kutumia mabomu ya machozi ili kuwatawanya
wananchi hao ambao walipeleka makande katika kituo cha polisi ili msiba
uendelee hapo.
Mwisho
Stephano Simbeye - VWAWA:
Serikali mkoani Songwe imepiga marufuku wananchi kuuza ardhi katika kipindi hiki ambacho inafanya mchakato wa kupima kila kipande cha ardhi, ili kuwamilikisha wananchi ili iweze kuwasaidia kupata mitaji itakayowasaidia kujiinua kiuchumi.
Agizo hilo limetolewa jana na mkuu wa mkoa wa Songwe Luteni Mstaafu Chiku Galawa alipokuwa akifunga mafunzo ya siku tano ya wakusanyaji takwimu na kuandaa rasimu ya mkoa yaliyofanyika katika ukumbi wa Vwawa sekondari wilayani Mbozi, kuwa upo uwezekano wa madalali kuweka kivutio cha bei nzuri ya ardhi kwa sasa lakini isiwafae katika siku za baadaye.
"Tumeamua tuanze na kipaumbele cha kurasimisha ardhi yetu kwa kuipima ili tujue kila kipande kinamilikiwa na nani na kwa matumizi yepi ambapo wananchi wanaomiliki ardhi hiyu watapewa hati miliki ambazo zitakuwa zimeiongeza thamani nakuwa mtaji muhimu wa kuwaondoa kutoka kipato walichonacho na kuwa kipato cha kati ifikapo 2025"alisema Galawa.
Alisema mkoa umeamua kuanza na takwimu kama kipaumbele chake cha kwanza ili kuandaa takwimu sahihi zitakazosaidia kuandaa rasimu ya wasifu wa mkoa na kujua pato la mwananchi wa hali ya chini la sasa na kufahamu namna ya kulipandisha, na kwa kuwa asilimia 80 ya wananchi ni wakulima ambao wanatumia ardhi kama mtaji hivyo ni wajibu wa serikali kuipima.
Galawa alisema kuwa mkoa hautaruhusu mwekezaji ambaye atataka kumiliki ardhi wakati wa kuwekeza bali awekeze kwa ubia na wazawa ambao ndiyo wenye ardhi ubia ambao utasaidia kutoa ajira na kuongeza kipato kwa wananchi.
Kwa upande wake Meneja urasimishaji ardhi kutoka (MKURABITA) Wizara ya Ardhi Joseph Werema alisema upo uwezekano mkubwa wa kufanilisha progam hiyo kwani wananchi wengi rasilimali yao ni ardhi, hivyo wakipimiwa itaongezeka thamani na hivyo kuwasaidia kiuchumi.
Alisema faida ya kurasimisha ardhi na kupatiwa hatu ni nyingi ikiwa ni pamoja na kuweka kama dhamana kwenye vyombo vya fedha ili kujipatia mikopo itakayowaendeleza kiuchumi, pia itasaidia kuwafahamu wananchi wake na shughuli wanazofanya ili wanapopanga kuwainua kiuchumi watakuwa wanafahamu kwa sasa uchumi wao uko wapi.
Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo Freza Asenga alisema mafunzo hayo yatawasaidia namna ya kufahamu kuandaa takwimu ambazo zitawasaidia kuandaa rasimu ya mkoa wa Songwe, na kujua pato la mwananchi wa Songwe kwa ujumla na kujipanga namna ya kusaidia kuinua pato hilo kufikia malengo yanayotarajiwa.
Alisema mafunzo hayo pia yatasaidia mkoa kujua jinsi ya kupanga mipango yake kiuchumi, kijamii kwa kutambua rasilimali zilizopo na kuzipangia utaratibu na kuweza kufahamu pato la mwananchi kwa ujumla.
Mkazi wa kijiji cha Isandula Wilson Salamba alisema agizo la kukataza kuuza ardhi ni zuri lakini serikali inapaswa ifahamu kwanini watu wanauza ardhi ambapo sabbu hiyo ndiyo ikifanyiwa kazi wananchi hawatauza ardhi kwani wanatambua kuwa ardhi ni rasilimali mama ya uchumi.
Alitaja baadhi ya sababu zinazosababisha kuuza ardhi kuwa ni pamoja na mahitaji ya fedha za kupeleka watoto shule, matibabu na wakati Fulani njaa inapojitokeza katika kaya wanalazimika kuuza ardhi ili kujikimu na hayo.
Mwisho
Stephano Simbeye, - Bara
Imeelezwa kuwa tatizo la udumavu ambalo linawakabili wakazi wa mkoa wa Songwe, litamalizwa iwapo jamii itaondokana na tabia ya kupenda kula vyakula vya aina moja kwa mazoea, licha ya eneo hili kuzalisha aina mbalimbali za vyakula ikiwemo aina ya mizizi kama viazi lishe.
Wito huo umetolewa na katibu tawala wa wilaya ya Mbozi Tusubileghe Benjamini wakati akizungumza na wakazi wa kijiji cha Bara kata ya wilayani Mbozi mkoani hapa kuwa kilimo cha viazi lishe ambavyo huvumilia ukame kitawafanya wananchi kupata vitamin A ambayo husaidia kupunguza udumavu kwa watoto walio chini ya miaka 2 na kusaidia kuongeza uwezo wa kuona.
“ suala la udumavu wa watoto linapaswa kuchukuliwa hatua tangu siku mimba inapotungwa hadi mtoto anapotimiza umri wa miaka miwili na kuendelea” alisema Katibu Tawala huyo.
Aidha Tusubileghe aliwataka wananchi kuunda vikundi mbalimbali vya kilimo cha viazi hivyo na kuvisajili ili kuweka uwezekano na urahisi wa kupata mikopo kutoka taasisi mbalimbali na kuwataka viongozi katika vikundi hivyo kuepuka kuvitumia kwa manufaa yao na kunufaika zaidi na kuahidi kuwawajibisha watakaofanya vitendo hivyo.
Mkoa wa Songwe una kiwango kikubwa chaq udumavu unaokadiriwa kuwa asilimia 36 hali ambayo inafanya hatua za maksudi zianze kuchukuliwa ili kuweza kuokoa watoto kuwa na udumavu na kupoteza nguvu kazi ya taifa siku za usoni.
Mtafiti wa mazao ya mizizi kutoka kituo cha kilimo Uyole John Kigwinya alisema kuwa lengo la watafiti kuzalisha viazi hivyo ni kusaidia kupunguza tatizo la vitamin A kwa asilimia 51 katika jamii kwa kuwa kilimo cha viazi hivyo ni rahisi kutokana na kuwa huvumilia ukame kitendo ambacho husaidia pia kupunguza uhaba wa chakula katika jamii.
Alisema viazi hivyo vina virutubisho muhimu kwa afya ya binadamu hivyo iwapo vikiliwa kila wakati vitasaidia katika makuzi ya watoto na hata watu wazima.
 |
No comments:
Post a Comment