Wednesday, 28 September 2016
Baraza la Mamlaka ya Mji wa Vwawa Lashinikiza Halmashuri Kulipa Deni la Sh. Mil. 145 ndani ya wiki Mbili
Na: Stephano Simbeye,
VWAWA:Baraza la Mamlaka ya Mji mdogo wa Vwawa wilayani Mbozi mkoani Songwe limetoa siku 14 kwa halmashauri ya wilaya kuwa iwe imelipa deni la Sh. 145 milioni inazodaiwa na mamlaka hiyo ambazo ilizitumia pasipo ridhaa yake kwa kutumia mwanya wa kuwa wamiliki na watia saini wa baada ya kufungwa akaunti za Mamlaka kwa maelekezo ya serikali.
Uamuzi huo umetolewa jana kwa kauli moja baada ya wajumbe wa vyama vya CCM na Chadema kuondoa tofauti zao za kiitikadi kwa kujali maslahi ya wananchi ktika kikao cha dharura kilichofanyika katika ukumbi wake huku mkuu wa wilaya hiyo John Palingo akiwa mgeni rasmi kuwa wamechoshwa na kitendo cha halmashauri ya Mbozi kuhodhi fedha zinazokusanywa na mamlaka hiyo kutoka vyanzo mbalimbali vya mapato, huku ikishindwa kuzitoa ili zifanye kazi ya kuwaletea maendeleo wananchi.
Mwenyekiti wa Mamlaka ya mji mdogo wa Vwawa Efraim Mwakateba alimwambia mkuu wa wilaya kuwa pamoja na jitihada zake za kutatua tatizo hilo lakini watenaji wa halmashauri wamedharau maagizo na makubalino ambayo yamekuwa yakifikiwa mbele yake hivyo wanatarajia kutoa maazimio mazito yenye nia ya kutetea fedha za walipa kodi kutowafikia walengwa.
“ baada ya mazungumzo ya mezani kutoleta mafanikio tumuamua na tumedhamilia kuingia katika mgogoro na halmashauri ili kuishinikiza irejeshe fedha za wananchi ili tutekeleze ahadi tulizowaahidi na tumeamua kufuata njia sahihi za kulitatua jambo hili tusijeonekana tumevunja sheria”alisema Mwakateba.
Alisema iwapo halmashauri haitatekeleza hilo ifikapo Oktoba 12 mwaka huu wataitisha mkutano wa hadhara wa wananchi wote ili kuwashawishi waache kulipa ushuru ikiwemo kodi za majengo, ushuru wa masoko, maegesho ya magari na wafanya biashara zao bure.
Mjumbe wa baraza hilo Yared Mtafya alisema suala hilo lilianza mwaka juzi mara baada ya kutakiwa kufunga akaunti za mamlaka kwa maelekezo ya serikali ambapo fedha zote zinazokusanywa huingizwa kwenye akaunti za halmashauri ya wilaya, hivyo iwapo mamlaka inahitaji kutumia inalazimika kuandika dokezo ili kupata fedha hizo jambo ambalo limekuwa ni kinyume ambapo tangu mwaka jana walikusanya zaidi ya Sh 126 milioni na mwaka huu tangu kuanza kwa mwaka wa fedha wamekusanya zaidi Sh. 39 milioni lakini hadi sasa hakuna dokezo ambalo limepitishwa.
“ Mheshimiwa mkuu wa wilaya pia tumekuwa kila tukifuatilia tunaambiwa kuna tatizo la mfumo lakini tulipokwenda kujifunza kwenye mamlaka nyingine za miji midogo tulikuta wenzetu wana mfumo mzuri na wana kifungu kidogo (sub vote) ambacho halmashauri haikitumii lakini hapa kwetu hakuna kitu kama hicho” alisema Mtafya.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya Mbozi Hosana Nshuro akijibu hoja hizo alikiri kuwapo na mapungufu mengi lakini aliwaomba radhi wajumbe wa baraza hilo kutokana na mapungufu ya kiutendaji ambayo yamekuwa yakitokea wakati wote.
Alisema hivi sasa mapungufu yamerekebishwa na kuwa yote yaliyozungumzwa atayachukua na kwenda kuyafanyia kazi na kwamba hali hiyo haitojitokeza tena.
Naye Mkuu wa wilaya ya Mbozi John Palingo alitoa siku tatu kwa halmashauri hiyo iwe imeanza kulipa deni la mamlaka ya mji mdogo wa Vwawa na kwamba wasipofanya hivyo atachukua hatua ikiwa ni pamoja na kuwaweka mahabusu saa 24 na kwamba pia apatiwe mpango wa kulipa deni hilo hadi litakapokwisha ili iwe rahisi kufuatilia.
Alikemea kitendo cha kila wakati kusikia mfumo wa uhasibu ni mbvu ili hali wanaye mtaalamu wa Tehama na kwamba kama hana uwezo wamuondoe na kuajili mtu mwenye uwezo wa kazi hiyo.
Mwisho.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment