Stephano Simbeye, Mbozi
Halmashauri ya wilaya ya Mbozi mkoani Songwe
imefanya mapitio ya bajeti ya 2017/2018
ili kuziba pengo lililotokana na vyanzo vilivyoondolewa na serikali kuu na
vingine kupunguzwa viwango.
Uamuzi huo ulifikiwa jana katika kikao maalumu cha baraza la
madiwani hao kilichofanyika katika ukumbi wake mjini Vwawa ambapo waliongeza
vyanzo kadhaa vipya, kuimarisha vyanzo ambavyo vilikuwepo lakini vilikuwa
havikusanywi kwa sababu mbalimbali.
Awali akieleza sababu za mabadiliko hayo Kaimu Mtunza Hazina
wa halmashauri ya Mbozi Deodatus Mtaremwa alisema yanatokana na mabadiliko ya
sheria ya fedha ya mwaka 2017 ambayo imefuta baadhi ya vyanzo vya mapato
vilivyokuwa vinakusanywa na halmashauri na vingine kupunguzwa viwango.
Alisema ushuru wa mazao ya chakula umepunguzwa kutoka
asilimia 5 hadi asilimia 2, ushuru wa kahawa umepunguzwa kutoka asilimia 5 hadi
3, pia kuondolewa kwa baadhi ya vyanzo kama ushuru wa mabango, kodi ya majengo
vimeathiri bajeti ya halmashauri kwa asilimia 32.
Diwani wa kata ya Halungu Maarifa Mwashitete alisema
halmashauri hiyo imekuwa ikitegemea chanzo kimoja cha ushuru wa zao la kahawa na
mazao ya chakula huku ikiviacha vyanzo vingine, lakini kutokana na kuteteleka
kwa zao hilo wamelazimika kuangalia vyanzo vingine ili halmashauri iweze
kujiendesha.
“ Vyanzo vingi vilikuwepo lakini kutokana na uzembe tu
vilikuwa havifuatiliwi na vikakusanya ili viingize mapato katika halmashauri
jambo ambalo limefanya halmashauri kukosa mapato” alisema Mwashitete
Ili kufanikisha ukusanyaji wa mapato katika chanzo cha mazao
watendaji watapaswa kuwatambua wakulima wao ili kuwadhibiti wafanyabiashara
wanaotumia mwanya wa kusafirisha mazao yasiyozidi tani moja bila kulipa ushuru
kama ilivyoagizwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Pombe
Magufuli hivi karibuni.
Bartoni Sinienga ni Diwani toka kata ya Ipunga alipendekeza
halmashauri kujenga kiwanda kidogo cha kusindika baadhi ya mazao ili kuongeza
thamani na kujipatia mapato, pia alipendekeza vyanzo vingine vinne vipya
ambavyo vitasaidia kuongeza mapato ya halmashauri.
Alivitaja vyanzo hivyo kuwa ni pamoja na kuanza kutoza ushuru
wauzaji wa mabaki ya vyakula (Pumba) kiasi cha asilimia 2 ya bei, kutoza vibari
vya usafirishaji mifugo, mashine za kupukuchua mahindi, kuwatoza mafundi
wajenzi wa nyumba, na bidhaa za ngozi kutozwa asilimia 3.
Kwa upande wake Mwanasheria wa halmashauri Deogratus Nchimbi
aliwatahadharisha madiwani kuepuka kuingiza vyanzo ambavyo vitakuwa kero kwa
wananchi ambapo vinaweza kuongeza tatizo badala ya kutatua tatizo.
Mwenyekiti wa halmashauri ya Mbozi Erick Ambakisye alisema
changamoto ya kukosa mapato ndiyo iliyowafanya waitishe kikao cha dharura ili
kujadili na kupitisha mkakati wa bajeti ya mwaka 2017/2016 katika kuongeza
mapato ya ndani ya halmashauri na kukusanya kwa asilimia 100.
Alisema wameamua kuweka mkazo wa makusanyo katika vyanzo
kadhaa vya ushuru wa madini ambapo Makampuni hayo yalikuwa yanalipa Sh.
1.2milioni kwa mwaka kwa tozo la asilimia 0.02 na kwamba hivi sasa chanzo hicho
kitatozwa ada ya Sh. 3000 kwa tani moja itakayosafirishwa madini ya makaa yam
awe, marumaru na udongo wa kutengenezea saruji.
Ambakisye alisema ili kufanikisha ukusanyaji wa ushuru wa
madini halmashauri yake inatarajia kujenga mzani mpakani mwa wilaya hiyo katika
kijiji cha Nanyala ili kupima magari yaliyobeba madini hayo kwa lengo la kupata
takwimu sahihi ambapo awali walitegemea takwimu kutoka TMAA.
Mwenyekiti huyo alieleza vyanzo vingine kuwa ni kutoza ada
ya uhai wa vikundi ambapo vipo vikundi 700 ambavyo vitalipa Sh. 20000 kila
kimoja na kiiingizia mapato halmashauri ya zaidi ya Sh. 140milioni, vikundi
zaidi ya 700 vya kuweka na kukopa vitatozwa ada ya mikopo ambayo pia itaipatia
halmashauri hiyo zaidi ya Sh. 140milioni,
Aliongeza vyanzo vingine kuwa ni kuyatoza makampuni
yanayonunua kahawa wilayani hapa, vikundi vinavyonunua mazao, wafanyabiashara
binafsi wanaonunua mazao mchanganyiko na kwamba makusanyo hayo yataipatia
halmashauri Sh. 1.55 kwa mwaka kiasi ambacho ni ongezeko la zaidi ya Sh. 800milioni
ukilinganisha na makisio ya awali.
Mmoja wa watendaji Rose Vicent aliiomba halmashauri hiyo
kuwaongezea nguvu kazi na ulinzi kutokana na ugumu wa kukusanya mapato ambapo
mara nyingi kazi hiyo inawafanya wachukiwe na wananchi.
“Ukiwa mtendaji hutakiwi kupendwa na watu lazima uvae sura
kavu, tunaomba tupatiwe ushirikiano wa kiusalama kila kata wawepo askari kata
ambao watalipwa kutokana na kazi wanayofanya kutokana na asilimia za
mgawanyo”alisema
Afisa Tarafa ya Vwawa Haji Hamis Ibrahim alisema upo ugumu
katika utekelezaji wa maazimio ambayo madiwani wameyafikia kutokana na wao
wenyewe kuingilia utendaji na hasa kuwatetea baadhi ya wananchi wakati
wanatozwa ushuru jambo ambalo linakwamisha kazi.
“ mgtakumbuka katika bajeti iliyopita mlikiri kuwa mmeikosea
lakini jambo la ajabu ilipofika utekelezaji mkawataka watendaji wajieleze, huku
mkisahau kuwa ninyi wenyewe mlikosea tangu mwanzo, hata hivyo watendaji
wawezeshwe vitendea kazi ili kufikia malengo” alisema Ibrahim.
Mwisho
No comments:
Post a Comment