Social Icons

Thursday, 31 August 2017

Mbunge wa Tunduma Ashikiriwa



Stephano Simbeye, Mwananchi
Mbunge wa Tunduma Frank Mwakajoka amekamatwa na Jeshi la Polisi leo alipokuwa katika mahakama ya wilaya ya Mbozi mkoani Songwe, kufuatilia kesi ya Mbunge mwingine wa Chadema Pascal Haonga.

Katibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo wilayani Mbozi James Mbasha amethibitisha kukamatwa kwa mbunge huyo lakini amesema hajui kosa linalomkabili isipokuwa tangu asubuhi alisikia kuwa mbunge huyo anatafutwa.

Mbunge wa jimbo la Mbozi mkoani Songwe Pascal Haonga (Chadema) na wenzake wawili wamefikishwa katika mahakama ya wilaya ya Mbozi kujibu mashitaka mawili ya kufanya vurugu na kuwazuia askari Polisi kufanya kazi yao kinyume na sheria.

Imedaiwa mahakamani hapo na mwendesha mashitaka Mkaguzi wa Polisi Samwel Saro kuwa washitakiwa wawili Pascal Haonga (36) na Wilfred Mwalusanya (32)  saa 7 mchana Agosti 28 mwaka huu wote kwa pamoja walimzuia askari polisi kutimiza majukumu yake ya kumkamata Mashaka Mwampashi ambaye hakuwa mjumbe katika uchaguzi wa kupata Mwenyekiti wa Mamlaka ya mji mdogo wa Mlowo kinyume na kifungu 114 A (a) cha kanuni ya adhabu sura ya 16.

Aliwasomea shitaka la pili washitakiwa Pascal Haonga, Wilfred Mwalusanya na Mashaka Mwampashi(32) kuwa wote kwa pamoja wanashitakiwa kwa kosa la kumfanyia vurugu msimamizi wa uchaguzi ambaye ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya Mbozi Lauteri Kanoni bila uhalali huku wakijuwa kufanya hivyo ni kosa kinyume na kifungu 89(1) b cha kanuni ya adhabu sura ya 16.

Washitakiwa wote wamekana mashitaka yanayowakabili mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wilaya ya Mbozi Asha Waziri ambaye alisema dhamana iko wazi kwa kila mshitakiwa kuwa na wadhamini wawili wenye barua utambulisho kutoka kwa watendaji wa maeneo yao na bondi ya Sh. 2 milioni kila mmoja.

Washitakiwa wote wametimiza masharti ya dhamani hivyo kuachiwa huru hadi Septemba 25 mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa tena mahakamani kwa kuwasomea maelezo ya awali.
Mwisho.

No comments:

Post a Comment