Stephano Simbeye, Mwananchi
Mbunge wa Tunduma Frank Mwakajoka amekamatwa na Jeshi la
Polisi leo alipokuwa katika mahakama ya wilaya ya Mbozi mkoani Songwe,
kufuatilia kesi ya Mbunge mwingine wa Chadema Pascal Haonga.
Katibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo wilayani Mbozi
James Mbasha amethibitisha kukamatwa kwa mbunge huyo lakini amesema hajui kosa
linalomkabili isipokuwa tangu asubuhi alisikia kuwa mbunge huyo anatafutwa.
Mbunge wa jimbo la Mbozi mkoani Songwe Pascal Haonga
(Chadema) na wenzake wawili wamefikishwa katika mahakama ya wilaya ya Mbozi
kujibu mashitaka mawili ya kufanya vurugu na kuwazuia askari Polisi kufanya
kazi yao kinyume na sheria.
Imedaiwa mahakamani hapo na mwendesha mashitaka Mkaguzi wa
Polisi Samwel Saro kuwa washitakiwa wawili Pascal Haonga (36) na Wilfred
Mwalusanya (32) saa 7 mchana Agosti 28
mwaka huu wote kwa pamoja walimzuia askari polisi kutimiza majukumu yake ya
kumkamata Mashaka Mwampashi ambaye hakuwa mjumbe katika uchaguzi wa kupata
Mwenyekiti wa Mamlaka ya mji mdogo wa Mlowo kinyume na kifungu 114 A (a) cha
kanuni ya adhabu sura ya 16.
Aliwasomea shitaka la pili washitakiwa Pascal Haonga,
Wilfred Mwalusanya na Mashaka Mwampashi(32) kuwa wote kwa pamoja wanashitakiwa
kwa kosa la kumfanyia vurugu msimamizi wa uchaguzi ambaye ni Kaimu Mkurugenzi
Mtendaji wa halmashauri ya Mbozi Lauteri Kanoni bila uhalali huku wakijuwa
kufanya hivyo ni kosa kinyume na kifungu 89(1) b cha kanuni ya adhabu sura ya
16.
Washitakiwa wote wamekana mashitaka yanayowakabili mbele ya
Hakimu Mkazi Mfawidhi wilaya ya Mbozi Asha Waziri ambaye alisema dhamana iko
wazi kwa kila mshitakiwa kuwa na wadhamini wawili wenye barua utambulisho
kutoka kwa watendaji wa maeneo yao na bondi ya Sh. 2 milioni kila mmoja.
Washitakiwa wote wametimiza masharti ya dhamani hivyo
kuachiwa huru hadi Septemba 25 mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa tena mahakamani
kwa kuwasomea maelezo ya awali.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment