Na: Stephano Simbeye MBOZI:
Halmashauri ya wilaya ya Mbozi mkoani Songwe imetenga
zaidi ya Sh. 800 milioni kwa ajili ya kujenga soko la kisasa la mazao mchanganyiko
katika mwaka ujao wa fedha ili kuanzisha kituo cha manunuzi cha kuaminika na
kutatua kero ya muda mrefu ya wakulima kunyonywa na wachuuzi.
Hayo yameelezwa jana katika kikao cha baraza la Madiwani
kilichokutana mjini Vwawa ili kupitisha makisio ya bajeti ya mwaka 2018/2019
kuwa wilaya ya Mbozi ni mzalishaji mkubwa wa mazao ya chakula lakini hakuna
soko la uhakika la kuuzia mazao ambalo litasaidia wakulima kuuzia mazao yao
huku serikali ikisimamia vipimo halali.
Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Erick Ambakisye alisema moja
ya vipaumbele katika bajeti ijayo ni ujenzi wa soko la kisasa la mazao ambapo zimetengwa
zaidi ya Sh. 800milioni ili kujenga soko hilo ambalo aliwataka wataalamu
kutafuta eneo zuri litakalofikika kirahisi na watu wote, pia kipaumbele kingine
ni kufungua barabara zote zilizoharibika kutokana na mvua zinazoendelea
kunyesha ambapo zimetengwa Sh. 200milioni ambazo zitakabidhiwa kwa wakala wa
barabara za mjini na vijijini (TARURA)kwa ajili ya kazi hiyo.
Alisema hatua hiyo imekuja kufuatia soko la awali la mazao
lilokuwepo huko nyuma lilijengwa Tunduma lakini baada ya mgawanyo wa wilaya ya
Mbozi na Momba na Tunduma kuwa halmashauri ya mji imelazimu Mbozi kufanya
mchakato mwingine wa ujenzi wa soko la mazao.
Aidha Ambakisye alibainisha kuwa katika mwaka ujao wa fedha
halmashauri yake inatarajia kukusanya zaidi ya Sh. 5.8 bilioni ikiwa ni mapato
ya ndani ikiwa ni ongezeko la zaidi ya Sh. 1 bilioni ukilinganisha na bajeti ya
mwaka unaoendelea wa 2017/2018 na kuwa katika makusanyo ya mwaka wa fedha wa
2017/18 hadi sasa wamefikia asilimia 54.
Diwani kata ya Nyimbili Tinson Nzunda aliishauri idara ya
fedha ya halmashauri kutafuta takwimu halisi za mapato yatokanayo na zao la
kahawa na kuacha kutegemea takwimu za watu wengine ambao wamekuwa wakiidanganya
na hivyo kusababisha kupata mapato kidogo ukilinganisha na uhalisia wa
uzalishaji wa zao hilo.
Diwani wa Halungu Maarifa Mwashitete alisema iwapo watendaji
wa halmashauri wakiacha kufanya kazi kwa mazoea watawezesha kufikia mafanikio
ya makusanyo ya makisio waliyoyafanya na iwapo ikiwa kinyume chake hapatakuwa
na muujiza wa kufikia malengo.
Naye Katibu tawala mkoa wa Songwe anayeshughulikia uwekezaji
Halima Mpita aliitaka halmashauri ya Mbozi kuanza kujiendesha kibiashara kwa
kuboresha rasilimali zake ili ziweze kuongeza pato ambalo litasaidia kuiongezea
mapato na hatimaye kuelekeza kwenye miradi ya maendeleo.
Alitoa mfano baadhi ya vivutio vya utalii ambavyo viko chini
ya halmashauri vikiboreshwa vitasaidia kuiingiza mapato, kutumia shamba la
serikali la Magamba kuzalisha mbegu na shughuli nyingine nyingi zinzoweza
kuongeza mapato yake.
Iwapo uamuzi huu utafanikiwa utakuwa umeunga mkono jitihada
za asasi isiyokuwa ya kiserikali ya MIICO ambayo imeanzisha kampeni ya kutaka
kuwepo na bei elekezi katika mazao ya chakula itakayozingatia gharama za
uzalishaji ili kumkomboa mkulima na kufanya kilimo kiwe na mvuto.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment