Social Icons

Saturday, 20 August 2016

Naibu Katibu Mkuu CWT Alaani Kitendo cha Walimu Kudanganya Idadi ya Wanafunzi







Stephano Simbeye,

VWAWA:
 
Naibu Katibu Mkuu wa chama cha Walimu Tanzania (CWT) Ezekiel Oluoch amelaani kitendo kinachofanywa na baadhi ya walimu cha kuongeza wanafunzi hewa na kuwa amechukizwa na tabia hiyo ambayo amesema imekifedhehesha chama hicho na kwamba serikali ichukue hatua kali Zaidi ya kuwavua madaraka.

Kauli hiyo aliitoa jana katika ukumbi wa kanisa la Moravian Nsala mjini Vwawa wilayani Mbozi mkoani Songwe kuwa tabia baadhi ya walimu wakuu kuzidisha idadi ya wanafunzi ili wajipatie kipato cha ziada imekikata mapembe kutokana na kuwa kimekuwa kikipambana kutaka walimu wakuu wa shule za msingi na wakuu wa shule za sekondari kupatiwa posho na stahiki nyingine nyingi.

“ jambo hili linanifanya nikose usingizi kutokana na jitihada tunazofanya kuwapigania walimu harafu tunasikia wanafanya mambo ya kipuuzi ambayo yamekikata mapembe chama hicho, ambapo hivi sasa walimu wakuu wameanza kupatiwa posho hizo” alisema Oluoch

Alisema serikali iwachukulie hatua kali, Zaidi ya kuwavua madaraka walimu hao pia amewakumbusha walimu hao umuhimu wa kutimiza wajibu wao kuwa upo kwa mujibu wa sheria za mahusiano kazini

Mmoja wa walimu Grace Chanya akizungumzia suala la baadhi ya walimu wakuu kuongeza idadi ya wanafunzi hewa kuwa inatokana na mfumo mbaya wa utunzaji takwimu ambapo mwalimu wa darasa anakuwa na takwimu zake kupitia daftari la mahudhurio, huku mwalimu Mkuu wa shule ana takwimu kupitia daftari la usajili wa wanafunzi.

Alisema chanzo cha takwimu hizo kupishana ni kutokana na wanafunzi wanaohamia kutoingizwa kwenye kumbukumbu zote na hivyo kuleta tofauti inayojitokeza.

Habari Zaidi zinaeleza kuwa mchezo wa kuzidisha wanafunzi umekuwa ukifanyika muda mrefu tangu kipindi ambacho serikali ilikuwa ikitoa fedha za ruzuku (capitation glant), na kuwa hali hii inachangiwa na mamlaka kutokuwa makini katika takwimu.

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya mbozi Edina Mwaigomole akizungumza kwa njia ya simu kuhusu tatizi la baadhi ya walimu wakuu kuzidisha idadi ya wanafinzi kwa lengo la kudanganya ili wapatiwe fedha za ziada zinazotolewa na serikali katika utekelezaji wa elimu bure, alisema tayari ameunda kamati ndogo ya uhakiki anbayo anatarajia umpatie ripoti wiki ijayo ambayo atalinganisha na takwimu zilizopo.

Tayari katika mikoa ya Arusha, simiyu na wilaya ya Kinondini jijini Dar es salaam  kuwapo kwa idadi kubwa ya wanafunzi hewa.
Mwisho.

No comments:

Post a Comment