Social Icons

Tuesday, 23 August 2016

Lowasa atoa Somo kwa Wanachadema mkoa wa Songwe







 
Stephano Simbeye,Mbozi.
 
Wanachama wa chama cha demokrasia na maendeleo CHADEMA wametakiwa kuachana na siasa za harakati ,migomo na maandamano kwani hali hiyo inachangia kubomoa dola bali wavunje makundi na kuweka umoja kuhakikisha wanashika dola 2020.
 
Rai hiyo ilitolewa jana na aliyekuwa mgombea wa urais kupitia chama hicho Edward Lowasa kwa niaba ya umoja wa katiba ya wananchi UKAWA wakati akizungumza na wanachama wa chama hicho wilayani Mbozi mkoani Songwe katika ukumbi wa Moravian Vwawa mjini.
 
Lowasa alisema kuwa maandamano na migomo ya kiharakati inaweza kusababisha watanzania wakapigana wenyewe kwa wenyewe na kuwataka wanachama wa chama hicho wavunje makundi yaliyojitokeza wakati wa uchaguzi na kukijenga chama ili kiweze kushika dola katika uchaguzi mkuu wa mwaka  2020
 
Aliitaka serikali kuruhusu mikutano ya vyama vya siasa ili kila chama kitimize haki yake ya kikatiba ya kufanya mikutano kuimarisha vyama vyao na si mikutano kuwa ya upande mmoja wa chama tawala.
 
Mwenyekiti  wa baraza la wazee wa chama hicho Hasheem Juma Issa akizungumzia kuhusu operasheni UKUTA alisema kuwa wameamua kufikisha ujumbe kwa wananchi kwa kufanya maandamano ya amani Septemba Mosi mwaka huu na kuongeza kuwa hilo si la mkoa wa Songwe pekee bali ni nchi nzima huku maandamano hayo yakiambatana na mikutano ya hadhara.
 
Aidha aliongeza kuwa kulingana na katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaruhusu vyama vya Siasa kufanya mikutano, hivyo na wao waruhusiwe kufanya mikutano hiyo kwa kuwa Tanzania ni ya watanzania wote na hivyo misingi ya kikatiba iheshimiwe.
 
Naye kada wa chama hicho ambaye pia ni Diwani wa kata ya Ichenjezya Bahati Mbughi alisema chama kipeleke ruzuku katika ngazi za chini ili kusukuma nguvu katika kukijenga huku akiwataka wanachama wenzake wa CHADEMA kuachana na chuki zinazozalishwa wakati wa kura za maoni kipindi cha uchaguzi na kuacha kuitana mamluki.
 
Naye Richard Kibona aliwataka viongozi wa ngazi za juu kuacha kupokea malalamiko kutoka kwa kila mtu na kuyafanyia kazi bali watazame nani kayapeleka na jinsi ya kuyatatua si kuchukua maamuzi bila kutazama msingi wa malalamiko hayo na kuutaka uongozi wa chama hicho kuunda tume maalum ya kuchunguza makosa hayo.
 
Aidha mara baada ya mkutano huo kumalizika msafara wa Lowasa ulilekea Tunduma na hatimaye safari ya kuelekea Sumbawanga mkoani Rukwa kuendeleza mikakati ya chama hicho.
Mwisho.

No comments:

Post a Comment