Na Stephano Simbeye
VWAWA: Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya
Mbozi,mkoani Songwe wamekiri wazi kwamba hawajui kutafsiri taarifa za fedha
kutokana na kutokuwa na uelewa wa hesabu na kuwa kitendo cha kuwataka wapitishe
taarifa hizo ni sawa na kuwataka wabariki jambo ambalo hawana uwezo nalo.
Hayo yalijili jana katika kikao cha dharura
cha cha baraza kamili la madiwani cha kufunga hesabu za halmashauri hiyo katika
kipindi cha mwaka wa fedha wa 2015 unaoishia Juni 30,2016 na kuziwasilisha kwa
mkaguzi na mdhibiti wa hesabu za serikali (CAG) kwa ajili ya ukaguzi septemba
30 kabla ofisi haijafungwa.
Diwani wa kata ya Igamba Exzaud Kibona
alisema ni vigumu kupitisha mambo magumu bila kuwapa muda wa kuyapitia na kuwa
na uelewa ambao utaleta ufanisi.
"Mumetuletea taarifa ya fedha ili
tuipitishe, sijui mlikusudia nini kulifanya jambo hili kuwa la dharura kiasi
hiki, kututaka madiwani tupitishe mambo makubwa ya halmashauri yetu kwa muda
mfupi" alisema Kibona.
Sebastian kilindu ni diwani kata ya Mlowo
alisema wapo hewani kwani hawaelewi cha kufanya na kuhoji kuna ulazima gani wa
kuleta kwa dharura jambo hilo, wangepewa muda wa kutosha ili waweze kuhoji kwa
manufaa ya halmashauri yao lakini kwa sasa hawana cha kuhoji.
" tunabuluzwa hapa na utaratibu uliowekwa
kupata taarifa nyeti dakika ya mwisho utaratibu huo ubadilike kuiepusha halmashauri yetu na
aibu ya kupata hati za mashaka muda mrefu” alisema Kilindu
Naye diwani kata ya Halungu Maarifa
Mwashitete(Chadema) alisema kazi ya kufunga hesabu za halmashauri imefikishwa
kwao si kwa lengo la kufanyiwa kazi bali ili iidhinishwe na kupewa baraka za
baraza la madiwani maana hakuna hata diwani mmoja anayeweza kuijadili.
Mkuu wa wilaya ya Mbozi John Palingo
aliungana na madiwani hao kwa kusema kwamba taarifa hiyo imeandaliwa kitaalamu,
hivyo kwa mtu asiyekuwa mhasibu hawezi kuielewa hata angepewa muda wa kuisoma,
lakini aliwashauri madiwani kuhakikisha watendaji wa halmashauri wanafuata
taratibu wakati wote wa utendaji wao na kuwa na nyaraka zote zinazohusiana
matumizi ya fedha za umma.
Hata hivyo aliwasihi madiwani kuamini
kilichopo kwani yeye kama mhasibu amepitia na ameona hesabu ziko vizuri.
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Mbozi
Edina Mwaigomole alisema wamelazimika kuitisha kikao cha dharura kwa vile
walikuwa wanafanya kazi ya kuandaa kwa kupita maeneo mbalimbali ya wilaya na
kwamba ilikuwa ni lazima iwasilishwe Septemba 30 mwaka huu.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa halmashauri
Elick Ambakisye akitoa azimio la kikao hicho alisema kwa vile wajumbe wa baraza
lake hawana uelewa wa hesabu, pia hawajapata fursa ya kuipitia wameamua
kuipitisha hesabu hizo kwa sharti la kuingia mkataba na watendaji wa
halmashauri kusudi iwapo ukaguzi wa (CAG) utatoa hati chafu watawajibika kwa
matokeo hayo.
Halmashauri ya wilaya ya Mbozi imekuwa
ikipata hati za mashaka katika kipindi cha miaka minne mfululuzo jambo ambalo
limezua hofu.
Mwisho
No comments:
Post a Comment