Social Icons

Monday, 3 October 2016

Wapinga Wazo la Kuipandisha Hadhi Hospitali ya wilaya



Stephano Simbeye, 

VWAWA:Wazo la kutaka kuipandisha hadhi hospitali ya wilaya ya Mbozi (Vwawa) kuwa  hospitali ya rufaa ya mkoa wa Songwe limekataliwa na Baraza la Madiwani wa Halmashauri  wilayani hapa na kutaka wazo hilo lielekezwe katika hospitali ya Misheni Mbozi.

Uamuzi huo ulitolewa mwishoni mwa wiki wakati wa kikao cha dharura cha madiwani hao ambao walidai kuwa wazo hilo ni zuri Lakini lielekezwe kwenye hospitali ya Misheni ya Mbozi inayomilikiwa na Kanisa la Moravian jimbo la Kusini Magharibi kutokana na kuwa katika hospitali ya wilaya kuna majengo   machache pia hakuna eneo litakaloruhusu upanuzi.

Diwani wa kata ya Mpito Richard Mahawa (CCM) alisema katika hospitali ya wilaya palipofikiriwa kuwa hospitali ya mkoa hapafai kwa vile eneo lake ni dogo ambalo haliwezi kukidhi mahitaji yanayotakiwa kuwa hospitali ya mkoa.

Diwani wa kata ya Igamba Exaud Kibona alisema kutokana na mazingira yalivyo katika hospitali ya Misheni Mbozi yanakidhi kutumika kuwa hospitali ya rufaa ya mkoa ukianzia katika miundombinu ya barabara, majengo na pia kuna nafasi ya kutosha kwa ajili ya upanuzi.

Awali Kaimu Katibu Tawala mkoani hapa Erick Mapunda aliwartaka madiwani hao kuridhia mapendekezo ya mkoa ya kutaka kuipandisha hospitali hiyo kuwa ya mkoa ili Serikali iweze kuongezea bajeti ya kuihudumia, pia italeta madaktari bingwa na vifaa tiba kuliko ilivyo hivi sasa.

“ hii ni fursa nawaomba waheshimiwa madiwani ipokeeni ili Serikali iweze kutia mkono wake kwani itaongeza bajeti yake na kuboresha miundo mbinu ili iweze kuendana na mahitaji halisi ya hospitali ya mkoa, na kwamba mawazo waliyo nayo wayatafakari kwa kina kwani ni vigumu kuboresha kwenye nyumba ya mwingine badala ya nyumbani”alisema Mapunda.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Mbozi Elick Ambakisye alisema wazo ni jema Lakini halikufuata utaratibu kwa wazo kuanzia juu badala ya kuanzia ngazi ya chini badala ya hatua zilizochukuliwa hivi sasa za kuanza mchakato pasipo kuihusisha Halmashauri yake.

“ hapa tunaona kama wazo hili lisingerudishwa kwetu na wizara lingekuwa limefika mbali jambo ambalo linaleta msigano usiokuwa wa lazima, tunakuomba mwakilishi wa RAS fikisha salaam, tunahitaji kushirikiana sote tuujenge mkoa Lakini si hivi mnavyotaka kufanya”Alisema Ambakisye

Msemaji wa Kanisa la Moravian Jimbo la Kusini Magharibi Mchungaji Zakaria Sichone akizungumza kwa njia ya simu amesema bado hawajapokea ombi la kutaka kuipandisha hadhi hospitali yao kuwa ya rufaa ya mkoa, Lakini alisema iwapo ombi hilo litawasilishwa litafanyiwa kazi kwa kupelekwa katika vikao husika.

Alisema hospitali ni huduma ya wananchi ambapo wazo la kuipoandisha hadhi si tofauti na lengo 
lililokusudiwa tan gu awali hivyo Kanisa halitakuwa na kipingamizi chochote iwapo Serikali imeamua kuitumia hospitali hiyo.
Mwisho

No comments:

Post a Comment