Social Icons

Monday, 31 October 2016

Watumishi waliopoteza Mil. 410 za Halmashauri ya Mbozi Waliohama Kurejeshwa



Na Stephano Simbeye,Mbozi

WATUMISHI watano wa halmashauri ya wilaya ya Mbozi mkoani Songwe ambao wamehamishwa na wengine kustaafu wanatakiwa kurejeshwa ili kuja kutoa maelezo matumizi ya zaidi ya Sh. 410 milioni zilizopotea kwa mazingira tata.

Hayo yapo kwenye mapendekezo ya Tume iliyoundwa na mkuu wa mkoa wa Songwe Luteni Mstaafu Chiku Galawa kuchunguza upotevu wa fedha hizo katika halmashauri ya wilaya ya Mbozi, kufuatia imeshindwa kukamilisha uchunguzi wake baada ya  kukosa nyaraka muhimu, hivyo kulazimika kuwaita maofisa waliohusika licha ya kuwa wengine walikwishastaafu ili kukamilisha uchunguzi wake. 

Akisoma sehemu ya taarifa hiyo Mwenyekiti wa kamati hiyo ya watu wanne Kastory Msigala alisema kamati yake ilipewa hadidu za rejea tatu ili kuzifanyia kazi ambazo ni pamoja na kujua iwapo fedha zinazolalamikiwa zilifika katika halmashauri ya Mbozi, kufahamu malengo mahususi ya fedha hizo na iwapo zilitumika kwa malengo yaliyokusudiwa na ni miradi gani iliyokusudiwa kutumia fedha hizo.

Alisema katika uchunguzi wake tume imejiridhisha kuwa fedha hizo ziliingia katika akaunti ya halmahshauri ya Mbozi kiasi cha Sh. 410,136,002 na kuwa zililetwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo na mfuko wa barabara kwa mtiririko kuwa, Julai 19, 2012 ziliingizwa Sh. 233,019,897, Agosti 2, 2012 ziliingizwa Sh. 38,774,600 na Oktoba 19, 2011 ziliingizwa Sh. 133,341,585 na kufanya jumla ya Sh. 410,136,002.

Msigala alisema hata hivyo tume hiyo imeshindwa kupata majibu halisi jinsi fedha hizo zilivyo tumika baada ya kukosa hati za malipo, hata hivyo kamati hiyo imebaini kuwa Sh. 238 milioni ziliingia na zikahamishwa kwenda kwenye akaunti mpya ya pamoja ambayo ilikuwa na fedha nyingi wakati huo ilikuwa na fedha nyingi zaidi ya Sh. 2bilioni hali hiyo pia ilisababisha kukosa hati za malipo.

Aliendelea kueleza kuwa Sh. 38 milioni zilihamishiwa kwenye akaunti ya mishahara katika ofisi ya Mganga mkuu ambapo pia madokezo yaliyohamisha fedha hizo hayakupatikana pi takwimu na kumbukumbu za watumishi waliolipwa fedha hizo kama mshahara hazikupatikana.

Msigala alisema pia walihitaji kuona miradi ambayo fedha hizo zilipelekwa lakini hawakupata na kuwa maofisa walioitwa kwenye tume hiyo ili kutoa maelezo wengi hawakuwepo wakati huo hivyo kuhitaji maofisa waliokuwepo wakati huo akiwemo Mkurugenzi mtendaji, Mtunza hazina, Ofisa elimu sekondari Ofisa Mipango na Mganga mkuu wa wilaya ili kupata maelezo.

Diwani wa kata ya Isasa Emir Mzumbwe akichangia hoja hiyo alisema suala hilo limeigharimu halmashauri kwa kukosa fedha za maendeleo kufuatia kupata hati zenye mashaka ambapo awali ilidaiwa kuwa fedha hizo hazikuingizwa na hivyo kulazimika kutuma watu kufuatilia hazina.

Alisema ni vizuri wahusika wakatafutwa popote walipo ili waje watoe maelekezo vipi fedha hizo zilitumika.
Sebastian Kilindu ni Diwani wa kata Mlowo Sebastian alisema pamoja na watumishi hao kuitwa ili wahojiwe pia Mwenyekiti wa halmashauri Erick Ambakisye anastahili kukaa pembeni ili kupisha uchunguzi kwa faida y halmashauuri na pia kulinda heshima yake.

Mwanasgheria wa halmashauri ya wilaya ya Mbozi Deogratus Nchimbi alisema kuna vyombo vinavyohusika kuwaita watumishi hao ni vizuri vitumike kufuata utaratibu wa kisheria na kwa hatua ambayo suala hili limefikia ni vizuri vyombo vya dola vifanye kazi yake.

Katibu tawala mkani hapa Elia Ntandu alisema bada ya tume hiyo kukosa majibu mkuu wa mkoa ameagiza maofisa waliohusika wakamatwe ikiwemo waliohamishwa na waliostaafu hata hivyo alisema mtumishi mmoja uhamisho wake umestishwa na tayari yuko wilayani hapa kwa ajili ya hoja hiyo.

Naye Mwenyekiti wa halmashauri ya Mbozi Elick Ambakisye akizungumzia tuhma hizo zilizomhusisha nay eye alidai kuwa tuache taratibu zifuatwe na ukweli utajulikana.
Mwisho.

No comments:

Post a Comment