Na: Stephano Jonasi - Mbozi
Wakulima wa mahindi wanaofanya
kilimo hifadhi wameanza kunufaika kwa kuongeza kiwango cha mavuno kutoka gunia
8 walizokuwa wanapata awali kwa ekari moja hadi gunia 25 kwa ekari na hivyo
kuanza kuboresha maisha yao.
Wakizungumza jana katika sherehe ya
siku ya wakulima iliyofanyika katika kijiji cha Shiwinga wilayani Mbozi mkoani
Songwe wakulima hao walisema awali walikuwa hawaamini waliposhauriwa na
wataalamu kuanza kulima kilimo hifadhi jambo ambalo hawakuamini.
Bw. Sikujua Msukwa ni mkulima kutoka
kijiji cha Nkanga akitoa ushuhuda wake alisema walipopelekwa kwenye mafunzo
katika kituo cha utafiti Uyole jijini Mbeya kupatiwa mafunzo ya namna ya kulima
kilimo hifadhi hakuweza kuamini na aliendelea kuvumilia ili apate posho
waizokuwa wanalipwa tu.
Alisema mara baada ya mafunzo na
aliporudi nyumbani wakati wa kufanyia kazi yale waliyojifunza alilazimika
kugawa shamba lake katika sehemu mbili ili sehemu moja alime kilimo alichozoea
na sehemu nyingine alianza kulima kilimo hifadhi kama alivyofundishwa,
ambapo alipanda siku moja kwa kutumia mbolea na mbegu bora katika sehemu
zote mbili.
“ nawaambia ndugu zangu wakati mimea
inakuwa nilianza kuona tofauti kati ya eneo lililopandwa kwa kuzingatia kilimo
hifadhi na lile lililopandwa kwa kilimo tulichozoea, kwani sehemu niliyolima
kilimo hifadhi mimea yake ilikuwa vizuri huku shamba likiwa na unyevunyevu
wakati wote tofauti na upande wa pili ambako udongo wake ulikauka muda mwingi”
alisema Bw. Msukwa.
Aidha Msukwa alisema mafunzo
waliyopata yamewasaidia pia kufanya shughuli za kilimo pasipokumtegemea
mtaalamu wa ugani na kutoa wito kwa wakulima wengine kufika shambani
kwake kujifunza kwani wagani ni wachache hivyo wanahitaji kufundishana wenyewe
mambo madogo madogo yamsingi katika kilimo chao.
Akisoma risala mbele ya mgeni rasmi
mmoja wa wanakikundi cha Maendeleo Shiwinga ambacho pia kinajihusisha na
kilimo hifadhi Bw. Moses Roa alisema wamefanikiwa kuongeza tija ya
uzalishaji ambapo wamekuwa wakilima mazao ya maharage, mahindi na Soya kwa
kutumia njia mbalimbali kupitia mashamba darasa kwa kuonesha matumizi ya
mbegu bora na kilimo hifadhi udongo
Akizungumzia kipato katika zao la
maharagwe Bw. Roa alisema katika eneo walilotunza vizuri walivuna debe 3
½ na katika maeneo yaliyolimwa kienyeji walivuna debe moja na kuwa maeneo hayo
yalikuwa sawa kwa ukubwa wa mita 10 kwa 10
Meneja wa Mradi wa kilimo hifadhi
kanda ya Nyanda za Juu Kusini Bw. Erastus Mkojera alisema mradi unaendeshwa
chini ya usimamizi wa taasisi ya mtandao wa kilimo hifadhi Barani Afrika (CTN)
kwa kushirikiana na AGRA, S.N.V, Rucodia, na Pass una lengo la kuhifadhi udongo
na kuongeza kipato kwa wakulima.
Akiwahutubia wakulima waliohudhuria
sherehe hizo mgeni rasimi ambaye pia ni Ofisa kilimo wilayani Mbozi Bw. Richard
Siriri aliwataka wakulima kukimbilia fursa zinazojitokeza badala ya kusubiri
ili wanufaike nazo, pia aliwaasa kuitumia siku hiyo kwa kupokea ujumbe
waliopata na kuyatumia vizuri mashamba darasa kujifunza tecknolojia
inayofundshwa.
Alisema kilimo hifadhi ndicho
kitakachoisaidia nchi kuhifadhi udongo kutokana na ukweli kwamba ardhi na maji
ndizo rasilimali pekee ambazo haziongezeki lakini kutokana na ongezeko la watu
rasilimali hizo zinazidi kupungua siku hadi siku na hivyo zisipohifadhiwa
zitapotea na kuleta janga linaloweza kuleta madhara makubwa kwa taifa.
Aidha kilimo hfadhi ni kilimo
ambacho wakulima wanatumia tecknolojia ya madawa pasipo kulima kwa
kuvuruga ardhi bali mara baada ya mavuno wanaacha matandazo ya mimea waliyovuna
shambani ambapo mvua ikija inaacha unyevunyevu ambao unasaidia kuhifadhi udongo
ambapo hakuna udongo unaosombwa na maji tofauti na eneo lililolimwa ambalo
linakuwa kame na udongo husombwa na maji ya mvua.
Mwisho
Na: Stephano Jonasi, Mbozi
Mbunge wa viti maalumu mkoa wa
Songwe Bi. Risala Kabongo (Chadema) amesema kukosekana kwa maji katika mkoa wa
Songwe wenye mito na vyanzo vingi ni matokeo ya mipango mibovu ya serikali.
Kauli hiyo aliitoa alipozungumza na
wakazi wa kitongoji cha Majengo kilichopo katika kata ya Vwawa wilaya ya Mbozi
kuwa ni jambo la kushangaza eneo lenye mito, mabonde yanayotililisha maji mwaka
mzima halafu wananchi katika eneo hilo wakawa na shida ya maji.
"Inasikitisha sana wakati neema ya mito na vyanzo 26 tumepata lakini bado wanawake wanahangaika na kutumia muda mrefu kutafuta maji badala ya kufanya kazi za kuwaongezea kipato" alisema Bi. Kabongo.
Alisema hajaridhishwa na jinsi serikali inavyoshughulikia changamoto za ukosefu wa maji safi na salama kwa watu wake hata baada ya miaka hamsini ya uhuru kupita.
Mheshimiwa Kabongo aliongeza kuwa serikali ya awamu ya tano inayojinadi kuipeleka nchi kuwa ya viwanda wakati bado maji na mindomvinu ya barabara ni tatizo kubwa huku hatua zinazochukuliwa hazioneshi kutatua haraka changamoto hizo.
" wananchi pigeni kelele kudai haki yenu ya msingi na mtuunge mkono tinapopiganoa haki zenu, kama ilivyo katika awamu hii ambayo inatuzuia tinapotaka kukutana na wanawake wenzetu" alisema Kabongo.
Aidha Mji wa Vwawa unaokadiriwa kuwa na watu zaidi ya 50000 kwa mujibu ya sensa ya 2012 bado unatumia miundombinu ya maji iliyojengwa miaka ya 1960 wakati mji huu ukiwa kijiji na sasa ni mamlaka ya mji mdogo hivyo kufanya huduma ya maji kutolewa kwa mgawo na wakati fulani kukosekana kabisa.
Mkazi wa eneo la Mtambwe Bw. Livingstone
Kibona alisema wamekuwa na shida ya kupata maji ambapo mabomba yaliyopo na
waliyounganishiwa kwa bei nzuri hayatoi maji muda mrefu na kusababisha
kulazimika kufuata maji umbali mrefu hivyo muda mwingi kupotea bure bila
uzalishaji wowote.
Alisema kukosekana kwa maji katika mji huo kumewafanya wanawake kutumia saa nyingi kutafuta maji na wakati mwingine kuleta migogoro katika ndoa jambo ambalo linarudisha nyuma ustawi wa ndoa zao.
Akizungumzia upungufu wa maji katika mji wa Vwawa mbele ya Madiwani wa Halmashauri ya Mbozi Mhandisi wa maji Bw. Akson Mwasyange aliwashauri madiwani kutafuta fedha ya dharura ili kutafuta chanzo kipya cha maji ambayo yatatengenishwa na taasisi nyingine kama hospitali ili kuongeza upatikanaji wa maji.
Alisema chanzo kilichopo hakina maji ya kutisha hali ambayo inasababisha uhaba muda mwingi na kuleta usumbufu hasa kwa wagonjwa waliolazwa katika hospitali ya serkali ya wilaya (Vwawa)
Mwisho.
No comments:
Post a Comment