Na: Stephano Simbeye – Mbozi
JESHI la Polisi mkoani Songwe Kwa kushirikiana na Kampuni ya
Mbegu ya Pana jana zilikamata mbegu feki za mahindi aina mbalimbali kiasi cha
Kilogramu 455 zenye thamani ya Sh. 3.6milioni katika mamlaka ya mji mdogo wa
Mlowo wilayani Mbozi mkoani Songwe.
Kamanda wa Polisi mkoani Songwe Matias Nyange akizungumzia
sakata la kukamatwa kwa mbegu hizo Alisema oparesheni ya kuwakamata
wafanyabiashara hao wa Mji mdogo wa Mlowo katika Wilaya ya Mbozi ilifanyika
Oktoba 30 mwaka huu.
Kufuatia kukamatwa kwa mbegu hizo mkuu wa Mkoa wa Songwe, Luten
Mstaafu Chiku Galawa, ametangaza vita kali na wazalishaji na wasambazaji wa
pembejeo feki zinazosababisha hasara kwa wakulima katika Mkoa huo.
Galawa aliyasema hayo jana wakati akizungumza na waandishi
wa habari ofisini kwake kuwa, serikali mkoani humo haitamvumilia mtu yeyote atakayesambaza
mbegu feki , pamoja na pembejeo nyingine ambazo matokeo yake ni kusababisha
hasara kwa mkulima.
“Utafiti umeonyesha wazi kuwa suala la pembejeo feki ni tatizo
kubwa, kwani utafiti uliofanywa n a watafiti kutoka Chuo kikuu cha Dar es
salaam katika Wilaya za Mbozi na Momba pekee
unaonyesha kuwa asilimia zaidi ya 70 ya mbegu na viua tirifu zinazouzwa
madukani humo ni feki” alifafanua Galawa.
Aliongeza kuwa, mkoa wa Songwe umejipanga kudhibiti hali
hiyo ambapo wakuu wa wilaya na kamati zao wahakikishe wanafanya ukaguzi wa mara
kwa mara
Aidha, Galawa alisema serikali Mkoani humo itahakikisha
inaongeza udhibiti katika mpaka wa Tunduma kupitia kitengo cha kuthibiti ubora
na usalama wa mbegu zinazoingizwa nchini kutoka nje ili kuzuia uingizwaji
nchini mbegu feki za mahindi ambazo kwa asilimia kubwa zimekuwa hazina ubora
wala usalama.
Kwa upande wake, mkulima kutoka mtaa wa Ichenjezya Kati
Pascal Lwila alisema wao kama wakulima hawawezi kutambua mbegu feki bali
wanaiomba serikali kwa kuwatumia wataalamu waliopo iongeze juhudi za kudhibiti
ili kuwaokoa wakulima wasiangamizwe na wimbi la uuzwaji wa pembejeo feki
Mwisho.
safi sana, tena waendelea kua hvyo hvyo, maana tumechoka kupewa mbengu feki
ReplyDelete