Social Icons

Monday, 15 May 2017

Mwanamke aliyetaka Kuiba Kichanga Afungwa Miaka Saba Gerezani

Na: Stephano Simbeye, Mbozi
 
Mahakama ya wilaya ya Mbozi mkoani Songwe imemhukumu  kifungo cha miaka saba gerezani mwanamke mmoja  mkazi wa Majengo katika halmashauri ya Tunduma, Happness Mwakisyala(28) baada ya kukiri kutaka kuiba mtoto wa kiume mwenye umri wa saa 12 katika hospitali ya serikali ya wilaya (Vwawa) kinyume cha kifungu cha sheria 169 (1) b sura ya 16 kanuni ya adhabu kama ilivyofanyiowa marekebisho mwaka 2002.

Akisoma hukumu mara baada ya mshitakiwa kukiri mahakamani hapo,  hakimu wa mahakama hiyo Nemes Chami alisema kwa kuwa mshitakiwa amekiri yeye mwenyewe kutenda kosa hilo na kwa kuwa vitendo kama hivyo vinaanza kukithiri kwenye jamii, mahakama yake inamhukumu kifungo cha miaka saba gerezani ili iwe fundisho kwa wengine wenye nia kama hiyo.

Awali ilidaiwa mahakamani hapo na mwendesha mashitaka Samwel Siro kuwa mshitakiwa huyo kwa makusudi aliingia kwenye wadi ya wazazi katika hospitali ya serikali ya wilaya, na kumuiba mtoto wa kiume na kwenda kumficha chooni kabla ya kuondoka naye.

Siro alidai kuwa tukio hilo lilitokea Mei 11 mwaka huu saa 11alfajiri katika hospitali hiyo na kumwiba mtoto mchanga.

Mwendesha mashitaka huyo aliiomba mahakama kutoa adhabu kari kwa mshitakiwa kutokana na vitendo vya kuiba watoto kukithiri hivi sasa ili iwe fundisho kwa wengine wenye nia kama hiyo.

Aidha mshitakiwa huyo alipopewa nafasi ya kujitetea ili mahakama iweze kumuonea huruma kabla ya kutoa hukumu alisema “ ni kweli nilitenda kitendo hicho naiomba mahakama inihurumie na kunisamehe” alisema
Mwisho.
 

No comments:

Post a Comment