Stephano Simbeye, Mbozi
Mbozi:Vijiji 40 vyenye wakulima zaidi ya 4000,katika wilaya
ya Mbozi mkoani Songwe, vimeanza kunufaika na mafunzo yanayotolewa na wadau wa
mnyororo wa thamani wa zao la mahindi (Unyiha Maize Consortium) kupitia mradi
wa AGRA – IGGSAS ambapo wameongeza uzalishaji kutoka gunia 8 – 15 kwa hekari
moja, hadi kufikia gunia 25 – 35 msimu huu, hivyo kuongeza kipato.
Wakitoa uzoefu walioupata katika mwaka wa kwanza wa kuanza
mafunzo hayo ambayo wanayafanya kwa vitendo kupitia mashamba darasa, mkulima
kiongozi toka kijiji cha Ipyana Elias Mswima alisema katika kikundi chao
walitenga eneo lenye ukubwa wa robo hekari ambapo walipanda mbegu aina mbili
tofauti na kutumia mbolea ya kupandia na kukuzia mara tatu na kuwa wamevuna
gunia 7.5 sawa na gunia 30 kwa hekari.
Alisema kupitia shamba darasa hilo wakulima walifundishwa
mbinu bora za kilimo cha kisasa na chenye kulenga kuongeza uzalishaji na
hifadhi ya ardhi, kisha ujuzi huo kwenda kuutumia kwenye mashamba yao hali
ambayo imewaongezea pato la mavuno.
Eva Ndawila ni mkulima toka kijiji cha Ihowa alisema
zimejitokeza changamoto kadhaa ambazo zimekuwa kikwazo ni kuchelewa kupata
pembejeo hali ambayo inawafanya kuchelewa kupanda, alitowa mfano kwamba msimu
huu walichelewa kupanda, badala ya kupanda mapema mwezi Novemba walianza
kupanda Decemba 26.
Mdau wa mnyororo wa thamani zao la mahindi na mzalishaji wa
mbolea toka kampuni ya Yara Kefasi Sima alisema
mabadiliko ya tabia nchi yanawafanya wakulima kushindwa kupanga mipango yao,
hivyo kuwashauri kulima kuzingatia hifadhi ardhi na kutumia pembejeo sahihi
zenye virutubisho vingi.
Aliwataka waongeze jitihada kuhakikisha shamba linapandwa
mimea kwa idadi sahihi isiyopungua 21733 kwa hekari moja kwa nafasi ya sentimeta25
kwa 75, ambayo ikitunzwa vizuri watapata mavuno zaidi yanayoweza kufikia gunia
45 hadi 55 badala ya 30 walizopata msimu
huu.
Awali akisoma risala mratibu wa mradi wa mnyororo wa thamani
wa zao la mahindi Aloyce Kamzora alisema mradi huo unatekelezwa katika wilaya
mbili za Mbozi na Momba utagharimu dola za kimarekani 299,568 sawa na zaidi ya Sh.
674.03 milioni za Tanzania katika kipindi cha miaka minne 2016/2020, utawafikia
zaidi ya watu 10000 katika vijiji 200.
Alisema katika mafunzo hayo wanawaelimisha wakulima umuhimu
wa kutumia pembejeo sahihi katika eneo sahihi, kulima eneo ambalo mkulima
anaweza kumudu kulihudumia, badala ya kuwa na shamba kubwa ambalo hawawezi
kumudu kuhudumia.
Ofisa kilimo kutoka halmashauri ya Mbozi, Lydia Shonyela aliwataka
wakulima hao kuhifadhi vizuri mahindi waliyovuna, na iwapo watahitaji kuuza
wayakaushe vizuri kwani kuuza yangali mabichi yataharibu sifa yake na
kuwakosesha soko ikigundulika yapo chini ya kiwango kwenye masoko ya ndani na
nje ya nchi.
Alisema mafanikio waliyopata yameongeza uzalishaji
ukilinganisha na mwaka jana ambapo mavuno yalikuwa tani 212729 na kuwa mwaka huu
zitavunwa jumla ya tani 258837
Kuhusu kero ya kuchelewa kupata pembejeo kwa wakati, Mkuu wa wilaya ya Mbozi John Palingo aliwataka
wakulima wilayani hapa kuungana katika ushirika na kutumia mfumo wa stakabadhi
gharani kupata mikopo ya kununua pembejeo mapema badala ya kusubiri ruzuku
ya serikali ambayo ni kidogo isiyokidhi
mahitaji ya wakulima.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment