Social Icons

Thursday, 8 June 2017

Waonywa Kujihadhari na Matapeli wanaouza Bima Feki



Na: Manuel Kaminyoge- Mbozi
Wamiliki na watumiaji wa  vyombo vya usafili mkoani Songwe na nchi nzima kwa ujumla wametakiwa kuhakikisha bima zao kama ni halali ili kuepusha usumbufu unaoweza kutokeza pindi matatizo yanapojitokeza   kwa upande wa abilia ama gari lenyewe kuharibika .-

Kauli hiyo ilitolewa na Muhasibu wa mamlaka ya Bima Tanzania (TIRA) Nyanda za Juu Kusini Kulenje Mbura kuhusiana na wamiliki wa magari na madereva, kuwa makini pale wanapokata Bima kwa mawakala wanao husika na ukataji wa sticker za Bima, ambapo aliwaonya wale wanatoa sticker feki kuacha mara moja kwani  hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

Kwa upande wake  Meneja wa NIC  LTD   Tanzania mkoa wa mbeya  Ally Mohamed alipokuwa akizungumza na wandishi wa habari na kuongeza kuwa wamiliki   wengi wa vyombo vya moto na watumiaji hawana elimu namna ya kujua Bima ya bandia na halisi hali inayosababisha usumbufu wawapo barabarani.

Mohamed alisema kuwa baada ya zoezi la ukaguzi wa Bima hizo katika  mkoa wa Songwe wamebaini kuwapo matumizi ya Bima bandia hali inayosababishwa na watumiaji wengi wa vyombo vya moto kupenda kupitia njia za mkato 

Mmoja wa madereva Asante Rashidi alilalamikia zoezi hilo kuwa linakabiliwa na changamoto kubwa ya kukaa kwa muda mrefu wakati wa kukaguliwa  wakipoteza muda mwingi bila kufanyakazi hali inayofanya kukwamisha safari zao na kusababisha kupata hasara kwa kushindwa kutimiza malengo.

Mwanasheria wa Mamlaka ya Bima Tanzania Nyanda za Juu Kusini  (TIRA) Michael Mbena alisema kuwa madereva na wamiliki wa vyombo vya moto wanatakiwa kufika katika ofisi za kutolea Bima ili kuepukana na makanjanja ambao wamesambaa nchi nzima ,ikiwa ni pamoja na kupata elimu inayo husu masuala ya bima ya vyombo vya usafiri.

Aliongeza kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa wale wote ambao watakiuka sheria na taratibu za kupata bima ya  vyombo vya usafiri.
mwisho

 
Na: Manuel Kaminyoge, Mbozi

Wanachi wa wilaya ya Mbozi mkoani Songwe, wameaswa kulinda na kutunza mazingira kwa kutofanya shughuli za kilimo katika vyanzo vya maji kitendo ambacho ni kosa la jinai na ni kinyume cha sheria.

Hayo yalisemwa na Katibu Tawala wilayani hapa Tusubilege Benjamin  ambaye alikua mgeni rasmi katika sherehe za maadhimisho ya siku ya mazingira duniani,  ambazo kiwilaya zimefanyika kata ya Hezya akimuwakilisha mkuu wa wilaya ya Mbozi John Palingo lengo ikiwa ni kuhamasisha wananchi kijijini hapo kutunza mazingira kutokana na kata hiyo kukithiri kwa uharibifu wa mazingira.

Alisema suala la mzingira ni la dunia nzima na kwamba kufuatia hilo sababu  kubwa ya maadhimisho hayo ni kubuni mikakati mbali mbali itakayosaidia kupunguza uharibifu wa mazingira, jamii kuwajibika katika kupanda miti kwa ajili ya matumizi mbali mbali na kutoa elimu ya mazingira katika Nyanja mbalimbali hususani masuala ya afya na usafi wa mazingira.

Baadhi ya wananchi kijijini hapo walisema sheria ya mazingira kutaka shuguli za kibinadamu kutofanyika ndani ya mita 60 imewaathiri  kwakuwa  wengi wao wanategemea kujipatia kipato kwa kulima kilimo cha umwagiliaji.

Maiko  Mkumbo aliiomba serikali ipunguze mita 60 badala yake waweke mita 30 ili ziwasaidie kujipatia kipato.

Awali katika risala iliyosomwa na ofisa wa mazingira wilaya ya Mbozi mkoani hapa Hamis Nzunda  alisema wilaya ya Mbozi imefanikiwa kuwa na vyanzo vingi vya maji pamoja na  misitu lakini kutokana na changamoto za wananchi kuvamia maeoneo hayo kwa kufanya za kilimo  katika vyanzo hivyo  kitendo ambacho ni kinyume na sheria ya mazingira na 20 ya mwaka 2004. 

Nzuda alisema sheria inatoa hamasa kwa wananchi na wadau mbali mbali  kuendesha shughuli rafiki katika maeneo hayo kama ufugaji nyuki na bustani za miche ya miti na mabwawa ya samaki.
Mwisho

Na: Manuel Kaminyoge, Mbozi

Wakazi wa vijiji vya Chizumbi na Ukwile kata ya Isandula wilayani Mbozi mkoani Songwe, wameanza kutengeneza kipande cha barabara kwa nguvu yao katika eneo oevu baada ya mkandarasi anayetengeneza Barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 5 kushindwa kutokana na eneo hilo kuwa na maji mengi.

Potea  Mwembe, alisema  makubaliano ya kujitolea ujenga kipande hicho yalifikiwa mwishoni kwa wiki katika eneo hilo ambapo kufuatia kero wanayoipata ya kushindwa kupita eneo hilo.

Malaika Mbisa alisema kuwa wapo tayari kutumia nguvu yao ili ghalama zilizokuwa zinatakiwa kutumika eneo hilo badala yake zihamishiwe mbele ili kuimarisha barabara hiyo ambayo itaunganisha na kijiji jilani cha Mbebe wilayani Ileje na kurahisisha mawasiliano.

Kwa upande wake diwani wa kata ya Isandula Vasco Msongole  aliwapongeza wananchi wake kwa makubaliano waliyoyaamua na kwamba wameonyesha ushilikiano na moyo wa uchungu juu ya ukosefu wa barabara katika eneo hilo kwa muda mrefu.

Mwenyekiti wa halimashauri ya Mbozi Elick Ambakisye licha ya kuwapongeza wananchi hao kwa hatua hiyo pia alisema kuwa anawahakikishia kuwa pesa yao waliyotengewa kuhusu barabara hiyo itafanya kazi ipasavyo ili kuleta mawasiliano na muunganiko mzuri wa vijiji hivyo.

Ambakisye aliongeza kuwa atahakikisha anasimamia barabara hiyo inatengenezwa kwa ustadi na kwamba itasaidia kuleta maendeleo ya kata hiyo na kurahisisha mawasiliano kwa wananchi wa kijiji cha chizumbi na chimbuya.

Aidha barabara ya Chimbuya – Chizumbi yenye urefu wa kilometa 5 inajengwa na mkandarasi Subiri Ndambo inatarajia kukamilika mwezi ujao.
Mwisho

No comments:

Post a Comment