Stephano Simbeye,MBOZI:
Mkuu wa mkoa wa Songwe Chiku Galawa amepiga marufuku
upeperushaji wa bendera za vyama na biashara katika hifadhi ya barabara kuu ili
kuweka mandhari ya miji katika hali ya usafi.
Kauli hiyo aliitoa jana katika kikao cha wadau wa Afya
kilichofanyika mjini Vwawa wilayani Mbozi kuwa shughuli zozote zinazofanyika
katika hifadhi ya barabara kuu, ikiwa ni pamoja na bendera za vyama
zinazopeperushwa eneo hilo zitoke ili kuacha maeneo hayo safi.
“ Kwakuwa hao wanaofanya biashara zao barabarani wanafuata
wateja kwenye vituo vya mabasi, halmashauri zitafute maeneo mengine mazuri nje
ya barabara kuu ndiko wajenge stendi na magari yanayochukua na kushusha abiria
yaingie huko”alisema Galawa
Kuhusu uchafu unaozagaa kando ya barabarani mkuu huyo wa
mkoa aliwaagiza maofisa afya kuanza kuwakumbusha abiria kutotupa hovyo taka wawapo
safarini bali watumie vyombo vya kukusanyia taka ambavyo vitakuwa vikitumika
ndani ya basi.
Katibu wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo wilayani Mbozi James Mbasha akizungumzia suala la
kuondoa bendera barabarani kwa njia ya simu alisema chama chake bado hakijapata
taarifa kuhusu zoezi hilo hata hivyo alisema bendera hizo zina wenyewe walioziweka katika maeneo hayo
hivyo ni vizuri akawaita wahusika azungumze nao awambie sababu ya kuziondoa.
“Sisi hatuwezi kuondoa bendera maana hatujui sababu, kwanini
anawaogopa wenye bendera awaite akae nao, tunangoja mtendaji yeyote atakayekuja
kuziondoa tutamchukulia hatua kwa kumshitaki mahakamani maana zipo kwa mujibu
wa sheria” alisema Mbasha.
Akizungumzia kuhusu kuhamisha stendi kando ya barabara
Mbasha alisema hilo ni wazo zuri kwani maisha ya watu yapo hatarini kutokana na
baadhi ya stendi kuwa barabarani kama ilivyo stendi ya Mlowo ambapo usalama wa
watu uko hatarini.
Afisa Mtendaji wa
Mamlaka ya Mji Mdogo wa Mlowo Msolomi Dakawa alisema tayari mipango ya
kuhamisha stendi imeandaliwa katika eneo jipya la Forest na sasa wanasubiri
taratibu za wataalamu wa idara ya ardhi kukamilisha uwekaji wa alama za mipaka
baada ya hapo wataingia mikataba na wafanyabiashara ili wajenge vibanda
kuzunguka eneo hilo.
Mwisho
No comments:
Post a Comment