Wednesday, 21 March 2018
TFDA Yatoa Mafunzo kwa Wasindikaji Vyakula
Stephano Simbeye, Mbozi:
Wajasiriamali wadogo mkoani Songwe wameonywa kuepuka kuingiza na kufungasha bidhaa zilizopigwa marufuku kuingia nchini ili kulinda afya za walaji na kutokinzana na sheria za nchi.
Onyo hilo lilitolewa jana na Kaimu Katibu Tawala mkoani hapa Herman Tesha wakati akifungua mafunzo ya siku mbili ya wasindikaji wadogo wa vyakula yaliyoandaliwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Chakula na Dawa (TFDA) yanayofanyika ukumbi wa Southern Garden Hotel iliyopo mjini Vwawa wilayani Mbozi kuwa wasitumie mwanya wa mkoa kuwa mpakani kuingiza bidhaa zisizostahili.
Alisema kutokana na biashara kuwa huria baadhi ya wajasiriamali wamekuwa wakitumia mwanya huo vibaya kuingiza bidhaa zilizopigwa marufuku kuingia nchini, aliwataka kuzingatia sheria kwa kuendelea kufungasha bidhaa bora ambazo zimethibitishwa na mamlaka husika zitakazoshindana na nyingine kutoka popote duniani.
Aidha Tesha aliwataka wajasiriamali hao kulasimisha biashara zao ili ziweze kujulikana na kutambuliwa na mamlaka husika ili ziweze kukua na kushindana na nyingine kutoka popote hasa katika kipindi hiki ambacho Taifa linaingia katika uchumi wa kati wa viwanda na soko huru.
Kaimu Mkurugenzi wa Usalama wa Chakula kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Chakula na dawa Justin Makisi alisema mamlaka hiyo inao wajibu wa kuwasaidia wasindikaji wadogo wa vyakula ili waweze kukuwa na kuzalisha vyakula kwa mujibu wa kanuni bora za uzalishaji ili waweze kumudu ushindani wa soko la ndani na nje.
Alisema kukuwa kwa viwanda vidogo kutakuwa na mchango mkubwa katika kuongeza ajira na kipato katika ngazi ya kaya, kukuza kilimo cha mazao ya vyakula kutokana na kuwepo kwa soko na kuchangia pato la Taifa.
Mganga mkuu mkoa wa Songwe Dk. Heri Kagya alisema katika mafunzo hayo ambayo yameziunganisha mamlaka zinazohusika katika udhibiti na urasimishaji wa vyakula za TFDA, Shirika la Viwango (TBS), Shirika la Kuhudumia viwanda vidogo (SIDO) Brera kutasaidia wajasiriamali kupata majibu ya maswali mengi ambayo kwa muda mrefu yalikosa majibu.
Naye Mjasiriamali mdogo Peter Mwansite alisema licha ya kuwapatia mafunzo hayo ingekuwa jambo jema kama mamlaka ya chakula na dawa ikawa na utaratibu wa kutembelea mara kwa mara katika maeneo yao ya biashara ili kuwashauri zaidi kwa lengo la kuboresha na kuona waliyojifunza yanatetendewa vipi kazi.
Betha Mwankupili ni mjasiliamali kutoka mji wa Mlowo alisema pamoja na kupatiwa mafunzo hayo bado wanalo tatizo la kukosa mitaji na maeneo ya kufanyia kazi hali inayowafanya wafanyie kazi zao jikoni na kuhifadhi sebureni jambo ambalo katika mafunzo hayo wamegundua kuwa si sahihi. Kwa upande wake Ofisa mwendeshaji Biashara toka Shirika la kuhudumia viwanda vidogo (SIDO) kanda ya Mbeya Homila Ngolo alisema shirika lake limeandaa vifungashio bora kwa wajasiriamali wadogo ili waweze kuvipata
Mwisho
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment