Waziri wa Maji Profesa Makame Mbarawa ameagiza
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuchunguza chanzo cha
mgogoro uliyopo katika mradi wa maji
Chitete katika wilayani Momba mkoani Songwe, ambapo halmashauri imevunja
mkataba na kumweka mkandarasi mwingine kinyume cha taratibu na kuchelewesha mradi.
Alisema mradi wa maji Chitete wenye thamani ya Sh.493.2milioni Umekuwa na mabishano ambayo yanasababisha
mradi kuchelewa kukamilika na hivyo kuwafanya wananchi waendelee kukosa huduma
ya maji iliyokusudiwa.
“ DC upo hapa naagiza Takukuru waje wafanye uchunguzi
wabaini nini kimejificha katika mzozo huo, kama kuna interest za watu tujue na
wakati huo tuiombe wakala wa manunuzi (PPRA) watoe ufafanuzi juu ya suala kama
hili ili kuondoa ubishani na ili mradi uendelee” alisema Mbarawa
Alisema chanzo cha mabishano hayo ni kufuatia Mkandarasi wa
kwanza kuchelewa kufika eneo la kazi ambapo halmashauri ilichukua hatua ya
kuvunja mkataba, na kumuweka mkandarasi mwingine jambo ambalo ni kinyume cha utaratibu kwa
kuwa halmashauri baada ya kuvunja mkataba ilipaswa ipate kibari toka Wizarani
kisha taratibu nyingine za manunuzi zingefuata.
Mhandisi wa Maji wilaya ya Momba Maua Mgala alisema chanzo
cha mgogoro huo ni mkandarasi kutoonekana eneo la kazi katika kipindi cha miezi
mitano tangu alipokabidhiwa kazi, jambo ambalo ni kinyume cha mkataba ambao
unaeleza kuwa mkandarasi asipoonekana kwenye eneo la kazi mkataba utavunjwa.
“mkandarasi huyu alisaini mkataba Julai 12 mwaka 2017 lakini
hakuonekana hadi Februari 26 mwaka 2018 ambapo ndipo mkataba ulipovunjwa nay
eye kujulishwa ndipo alipoleta vifaa vichache na kuandika barua ya kupinga
kuvunjwa kwa mkataba”alisema Mgala
Alifafanua kuwa hata hivyo alisema halmashauri ilimvumilia
mkandarasi huyo huku ikimwandikia barua za kumkumbusha lakini hakutokea ndipo
ilipovunja mkataba na kumchukua mkandarasi aliyeshika nafasi ya pili kwenye
zabuni ili aendelee na kazi hiyo.
Kuhusu uamuzi wa Waziri kufuatia sakata hilo Mhandisi Maua
alisema ni uamuzi mzuri ambao utatupeleka mahali pazuri na hatimaye kukamilisha
mradi ili wananchi waendelee kupata maji.
Kwa upande wake mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Momba
Adriano Jungu alimwambia Waziri wa Maji kwamba lilipojitokeza suala la utata wa
Mkandarasi huyo alikwenda moja kwa moja Wizarani ili kutoa maelezo ya jinsi
hatua mbalimbali alizozichukua kuhusu mkandarasi huyo.
Aidha Kampuni ya DIPE & Company Limited ya Morogoro
ndiyo iliyoshinda kandarasi ya kujenga mradi wa maji Chitete wenye thamani ya
zaidi ya Sh.493.2 milioni, ambapo wakati wa ziara ya Waziri Mbarawa hakuna
mwakilishi wa kampuni hiyo aliyekuwepo.
No comments:
Post a Comment