Monday, 19 September 2016
Stephano Simbeye
Chitete: wakati katika maeneo mengine ya nchi wananchi wamekuwa wakijitolea kujenga zahanati kwa nguvu yao hali ni tofauti katika kijiji cha Yala kilichopo kata ya Chitete wilaya ya Momba mkoani Songwe baada ya wananchi hao kujitokeza kifua mbele kuomba serikali iwajengee zahanati.
Wakizungumza na waandishi wa habari waliotembele kijijini hapo baadhi ya wananchi hao waliiomba halmashauri wilayani humo kuwajengea zahanati ili kunusuru maisha yao ambayo yamekuwa yakipotea na hasa kwa akina mama wajawazito, watoto na wazee kutokana na kukosa huduma ya afya jirani.
Kijiji hicho ambacho kipo katika kata ya Chitete ambayo ipo makao makuu ya wilaya ya Momba ni moja ya vijiji vinavyokuwa kwa kasi huku shughuri za kijamii zikiongezeka lakini kimekumbwa na changamoto lukuki ikiwemo ukosefu wa zahanati na kusababisha watu kutembea umbali wa zaidi ya kilometa 30 kufuata huduma za matibabu katika kijiji jirani.
Mkazi wa Yala Dorasia Simkoko,alisema akinamama wajawazito wanapopatwa na uchungu wa kutaka kujifungua wanalazimika kukodi bodaboda hadi kwenye vituo vya afya vilivyopo kwenye kata za mbali hivyo wengi wao wanajikuta wanajifungulia barabarani.
Naye Amani Mtafya mkazi wa kijiji hicho,alisema kufuatia kukosekana kwa zahanati kijijini hapo kulisababisha mke wake kujifungulia polini wakati akiwa njiani kwenda kupata huduma ya kijifungua hivyo aliiomba serikali kukiangalia kwa jicho la tatu kijiji hicho ili kipatiwe zahanati.
Wakati wakazi way ala wakilalamikia zahanati wilaya mama ya Mbozi wananchi wake wamejenga maboma zaidi ya 80 ambayo yapo katika hatua mbalimbali yakisubiri nguvu ya halmashauri ili kuyamalizia yaanze kutoa huduma ya afya.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Momba Methew Chikoti, alikiri kuwepo tatizo hilo,lakini aliwataka viongozi wa kata kuwahamasisha wananchi kuanzisha ujenzi hadi mtambaa panya alafu halmashauri itamalizia kupaua kuunga mkono nguvu kazi za wananchi.
Aliwataka wakazi wa wilaya ya Momba kuacha kulalamikia serikali wakati wao hawajaonesha nguvu kwa kuanza kisha serikali itawaunga mkono na si serikali kuwajengea zahanati na kuwa hakuna utaratibu wa aina hiyo,na kuwataka viongozi wa kata wawaunganishe wananchi kwa pamoja ili kutimiza na kuondoa changamoto hiyo.
Mwisho
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment