Social Icons

Wednesday, 19 October 2016

CAG Aeleza Mambo Makubwa manee yaliyosababisha Halmashauri ya Mbozi Kupata hati za Mashaka

Na Stephano Simbeye, Mbozi



MDHIBITI mkuu wa hesabu za serikali (CAG) ameliambia Baraza la Madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Mbozi mkoani Songwe sababu kubwa nne zilizosababisha halmashauri hiyo kupata hati yenye shaka katika hesabu za mwaka wa fedha wa 2014/2015 na miaka mitatu mingine ya nyuma.

Akizungumza jana kwenye kikao cha baraza hilo kilichokutana kupitia hoja za ukaguzi mwakilishi wa CAG mkoani hapa Deogratus Njau alisema  sababu zilizosababisha hati ya mashaka ni pamoja na kutotenganisha mali za kudumu ardhi na majengo kama matakwa ya kanuni za kihasibu zinavyotaka, kutoonesha thamani ya mali za kudumu katika hesabu.

Aliendelea kueleza sababu nyingine kuwa ni kutoonesha thamani halisi ya ardhi kwenye hesabu hizo na kushindwa kuonesha hasara ya thamani ya fedha kiasi cha Sh. 410,755,546.97 ambayo haikuoneshwa ipasavyo kwenye hesabu za mwisho kwa sababu hesabu za mwaka 2012/2013 zilijumuisha mali za kudumu, mapato na matumizi ya halmashauri ya mji wa Tunduma ambapo fedha hizo zilitakiwa zionekane huko kwani walitakiwa kutengeneza hesabu zao.

Njau alieleza mtiririko wa hati zilizotolewa kwa halmashauri ya wilaya ya Mbozi katik kipindi cha miaka minne kuwa mwaka 2011/2012 ilipata hati ya mashaka, 2012/2013 ilipata hati yenye mashaka, 2013/2014 hati inayoridhisha na mwaka 2014/2015 hati yenye mashaka.

Aidha ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za serikali imetoa ushauri na mapendekezo ya jumla kwa halmashauri hiyo kuwa iongeze juhudi zaidi ya utekelezaji wa mapendekezo ya hoja yaliyobakia, kutofanya hivyo kutasababisha kujirudia kwa mapungufu hayo, kuimarisha utoaji huduma , matumizi mabaya ya mali za umma na usimamizi wa fedha na udhibiti usio na ufanisi wa rasilimali .

Kwa upande wake mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya Mbozi Edina Mwaigomole alisema halmashauri yake inakabiliwa na upungufu mkubwa wa watumishi ambao umesababishwa na mgawanyo wa halmashauri mbili za Momba na Tunduma ambapo watumishi waligawanywa kutoka halmashauri mama ya  Mbozi hali inayosababisha kazi nyingi kukwama.

Alitoa mfano kazi ya kuthaminisha ardhi haikuweza kufanyika kutokana na kukosa wathamini ambapo pia idara ya ardhi haina mpima ambaye anatakiwa kupima ardhi, pia aliitaja idara ya ujenzi kuwa inakabiliwa na upungufu mkubwa na wataalamu hivyo kuiomba serikali kuwapatia wataalamu ili kuongeza ufanisi.

Akichangia hoja katika kikao hicho Diwani wa kata ya Mpito Richard Mahaya alisema  baadhi ya madeni hayajawahi kuletwa katika vikao vya kawaida lakini wanashangaa leo kuyaona katika hesabu za ukaguzi na kuwa yangeletwa katika vikao vya kawaida yangetafutwa ufumbuzi kuliko kuyaacha yakasababisha hoja za ukaguzi.

Alisema wakati wa kugawanya wilaya mbli za Momba na Mbozi waligawa mali na madeni lakini alishangaa kuopna baadhi ya madeni ya momba kuonekana katika hesabu hizo jambo ambalo linaongeza hoja zisizo za msingi alipendekeza ziondolewe.

Mmoja ya wananchi waliofika kusikiliza kikao hicho  Frank Mwilenga alishangazwa na ukimywa ya viongozi kuhusu zaidiya Sh. 410milioni ambazo zimekuwa zikibishaniwa muda mrefu kutoeleza ukweli kama fedha hizo ni mali ya halmashauri ya mji wa Tunduma mapema hli iliyosababisha kuundwa Tume ya kuzifuatilia.
Mwisho

No comments:

Post a Comment