Social Icons

Thursday, 20 October 2016

CCM Mbozi waanza Kutumbuana



Stephano Simbeye,Mbozi

VWAWA: Wajumbe wa halmashauri kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Mbozi mkoani Songwe wamewavua madaraka viongozi wawili waandamizi kwa madai ya kukigawa chama na kutozingatia maadili ya viongozi.

Uamuzi huo umetolewa jana kwenye kikao kilichofanyika katika viwanja vya ofisi ya chama wilaya ambapo waliotimuliwa walitajwa kuwa ni Mjumbe wa halmashauri kuu ya CCM Taifa (NEC) George Mwenisongole na Katibu Itikadi na uenezi  wa wilaya Walen Kaminyoge.

Awali Katibu wa CCM wilayani hapa Doris Kimambo akiwasilisha agenda ya kujadili mienendo ya viongozi wa chama hicho alisema Katibu Itikadi na uenezi  Walen Kaminyoge amekuwa anatoa siri za chama na tabia isiyo ridhisha kwenye jamii na ambayo inakidhalilisha chama ya ulevi huku akikopa vinywaji ambapo chama kimemlipia mara mbili ili kuondoa fedhaha kwa kiongozi wake.

Alisema suala hilo limezungumzwa katika ngazi za awali na kuwa bado hajabadilika na hivyo kuamua kulepeleka katika kikao hicho ambacho ni kikubwa Zaidi ili kiweze kulijadili na kulitolea maamuzi na ambacho ndicho chenye jukumu la kuangalia mienendo ya wanachama.

Baada ya kuanzisha hoja hiyo alisimama mjumbe mmoja Edward Mwamundi ambaye alidai kuwa ni kweli mwenezi huyo anakiaibisha chama , lakini alihoji kuwa kuna kiongozi mmoja ameachwa ambaye ni MNEC nayeye ajadiliwe katika kikao hicho jambo ambalo liliungwa mkono na wajumbe wengine.

“ ndugu mwenyekiti inavyoonesha mtu mwenye fedha mnamuogopa na hachukuliwi hatua zozote kwani tumekuwa na mgogoro na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (MNEC) muda mrefu naye huyu hatufai mbona hamjaleta hoja yake hapa ” alihoji Mwamundi.

Alisema Mjumbe wa halmashauri kuu anakigawa chama kwa kutumia uwezo wa fedha alizo nazo , amekuwa akitumia lugha ya matusi ya nguoni kwa viongozi wake pia wakati wa uchaguzi aliahidi anamwangusha aliyekuwa Mbunge wa Mbozi na amefanikiwa kufanya hivyo.

Hata hivyo baada ya wajumbe kuunga mkono hoja ya mjumbe mwenzao Mwenyekiti wa Chama wilaya ya Mbozi Aloyce Mdalavuma aliwahoji wajumbe kuhusu hoja ya kumjadili MNEC ambapo wajumbe walikubali na kuanza kumjadili.

Katibu wa chama hicho Doric Kimambo alitowa mwongozi  alisema kuhusu MNEC  zipo taratibu stahiki zinazopaswa kufuatwa kama zilivyofanyika kwa Katibu Mwenezi jambo ambalo wajumbe walimkatalia.

Akizungumza kwa njia ya simu Katibu Itikadi na uenezi Walen Kaminyoge alisema bado hajapata taarifa ya kiofisi na kwamba mara atakapopata ujumbe huo ndipo atakuwa na jambo la kuzungumza ingawa alisema kikao hicho ndiyo waajili wake hivyo hawezi kurumbana nao.

Alisema pamoja na kuwa amaheshimu maamuzi ya kikao lakini bado kanuni hazijafuatwa kwa kupewa nafasi ya kujitetea.

Naye mjumbe wa Halmashauri kuu ya Chama cha Mapinduzi Taifa (NEC)  George Mwanisongole akizungumza kwa njia ya simu alikiri kupata taarifa isiyo rasmi kuhusu maamuzi hayo lakini alisema kikao kilichofanya maamuzi hayo ni batili kutokana na kuwa baadhi ya wajumbe walihongwa kushawishi wajumbe wenzao na wengine hawakuwa wajumbe halali wa kikao.

Alisema katika kikao hicho hapakuwa na ajenda ya kumjadili yeye bali kuna baadhi ya viongozi ambao anapingana nao kisiasa ndiyo waliotoa fedha kuwahonga wajumbe wasiozidi saba ambao walijenga ushawishi hadi  hoja ya kumjadili ikaingizwa kwenye kikao.

Kuhusu madai ya kuwa anakigawa chama alisema hajaelewa maana yake kwa kuwa baadhi ya mambo yaliyodaiwa kwenye kikao hicho ni ya muda mrefu na yalikwishapatiwa ufumbuzi na kuwa hakuna wanachama ambao yeye amewagawa.
Mwisho



No comments:

Post a Comment