Stephano Simbeye,
Mbozi
MBOZI: Halmashauri ya wilaya ya Mbozi mkoani Songwe
imeanzisha rasmi Mamlaka ya mji mdogo wa Mlowo, ikiwa ni njia ya kusogeza
karibu huduma kwa wananchi katika mji huo ambao unakuwa kwa haraka ikiwa na idadi kubwa
ya watu.
Afisa mtendaji Mkuu wa Mamlaka hiyo Msoleni Dakawa akizungumza
wakati wa kuhitimisha mafunzo ya wenyeviti wa vitongoji ambao wanatarajia
kuunda baraza la mji huo na kuhitimisha rasmi mamlaka za serikali za vijiji, alisema
mamlaka hiyo imeanzishwa kisheria na ilitakiwa kuanza tangu Julai mosi mwaka
huu lakini kutokana na sababu mbalimbali haikuweza kuanza na kuwa hivi sasa
inatarajia kuanza baada ya kukamilisha zoezi la kutoa elimu kwa viongozi.
Alisema mara baada ya kuanza litaundwa baraza ambalo
litakuwa na mwenyekiti na Makamu wa Mamlaka, pia zitaundwa kamati tatu za
kudumu ambazo ni Kamati ya uchumi, ujenzi na mazingira (Huduma za jamii),
kamati ya fedha uongozi na mipango miji na kamati ya elimu afya na maji.
“ hata hivyo kwa mujibu wa sharia mamlaka itakuwa na uwezo
wa kuunda kamati nyingine mbili kadiri itakavyoona inafaa kulingana na
mazingira ya mamlaka ikiwemo kamati ya kudhibiti Ukimwi” alisema Dakawa.
Mwenyekiti wa halmashauri ya Mbozi Elick Ambakisye aliwataka
wajumbe wa mamlaka hiyo kufuata sheria kanuni zilizopo katika kufanikisha
majukumu yao lakini pia kuandaa sheria ndogo ambazo hazitakinzana na sheria mama
ili kuharakisha maendeleo ya wakazi wa mji wa mlowo.
Alisema Mlowo imekuwa kama kijiji kwa muda mrefu hivyo
panahitajika jitihada za makusudi kurejesha tabia ya watu kutofuata taratibu na
sheria kwa kufuata taratibu zilizowekwa na zinazotarajiwa kutungwa pia
aliwataka wajumbe hao kujitoa Zaidi katika majukumu waliyokabidhiwa.
Aliwashukuru wajumbe ambao walikuwa wenyeviti wa vijiji kuwa
halmashauri inatambua majukumu waliyoyafanya na kuwa mabadiliko haya yamekuja
kutokana na mji kukua imelazimu kujipanga upya na kuwa kukua huku kunatarajiwa
kuendelea kadiri ya mahitaji.
Mmoja ya wajumbe wa Mamlaka ya mji wa Mlowo Monica Mnkondya
alisema mafunzo hayo yamewasaidia kufahamu namna ya uendeshaji wa mamlaka na
kwamba yatawasaidia kusimamia shughuli zilizopo mbele yao.
Alisema wamejifunza masuala ya kufuata kanuni sheria na
ulinzi na usalama mambo ambayo tangu walipochaguliwa hawakuwahi kuyafanya na
hivyo wamekuwa wakifanya kazi bila kujua taratibu zinazopaswa.
Kuanzishwa kwa Mamlaka
ya mji mdogo wa mlowo, kunahitimisha serikali za vijiji ambazo zilikuwa
vijiji vinne vya Mlowo,Nambala, Mbimba
na Ivwanga na kuwa kuna vitongoji 24
ambapo wajumbe wake wanatoka kwenye vyama vya CCM na Chadema kwa idadi sawa ya wajumbe
( CCM 12 na Chadema 12)
Mwisho
No comments:
Post a Comment