VWAWA: Mkuu wa wilaya ya Mbozi
mkoani Songwe John Palingo, jana alitembelea gereza la mahabusu wilayani hapa,
kisha kugawa misaada ya kibinadamu yenye themani ya Sh. 1.1 milioni na
kustushwa na idadi kubwa ya mahabusu wanaoingia na kutoka kila siku
Alisema hayo kufuatia taarifa ya
Mkuu wa gereza Salum Manjawa aliyoitoa kwa wajumbe wa kamati ya ulinzi na
usalama kuwa gereza hilo linakabiliwa na mrundikano wa mahabusu hali
iliyosababisha kuzidi uwezo wa gereza ambapo linapaswa kuwa na mahabusu 110
lakini waliopo ni 238.
Aidha Mkuu huyo wa gereza alisema
chanzo cha mrundikano huo ni kuchelewa kwa upelelezi hivyo usikilizaji wa kesi
kuchukua mufa mrefu na kuwa jitihada za kupunguza mahabusu zinafanywa na vyombo
husika hata hivyo kila siku wanaoingia wapya kati ya 20 na 30.
Akionesha kustushwa na hali hiyo Mkuu huyo wa wilaya aliviagiza vyombo vya usalama kufanya utafiti wa kina ili kufahamu chanzo cha uharifu uliokithiri wilayani hapa kasha kupata majibu ya kisayansi ambayo yakifanyiwa kazi yatasaidia kupunguza makosa ambayo ni chanzo cha kuwa na mahabusu wengi.
“ hali hii inaitia hasara serikali kuwalisha mahabusu ni vizuri tukafanya uchunguzi chanzo cha uharifu, na baada ya hapo tukashirikisha wadau mbalimbali kuelimisha jamii kujiepusha kujiingiza kwenye makosa ya jinai, tushirikiane pia na viongozi wa deni kukemea hali hii, hata hivyo jambo hili litajadiliwa kwenye kikao cha kamati ya ulinzi na usalama” alisema Palingo
Kamanda wa Polisi mkoani hapa Matias Nyange alisema chanzo kikubwa cha uhalifu katika mkoa wa Songwe ni migogoro ya ardhi, imani Potofu za kishirikina ambazo pia zinachangia kuwapo na mauaji.
Alisema jeshi lake liko imara kuhakikisha usalama kwa raia na mali zao ili kutoa fursa kwa wananchi kufanya shughuli zao kwa amani na utulivu.
Awali Katibu Tawala wilayani hapa Tusubilege Benjamini alisema misaada mbalimbali iliyotolewa katika ziara hiyo imetolewa na wadau mbalimbali ambayo ni pamoja na Blanketi, Chakula, sabuni, nguo za watoto kwa ajili ya watoto ambao wanaishi gerezani kufuatia mama zao kufungwa na king’amuzi kwa ajili ya kuwawezesha mahabusu hao kuona taarifa mbalimbali kupitia luninga.
Aliwataja wadau waliochangia misaada hiyo kuwa ni Pamoja na Kampuni ya Uandaaji kahawa (CMS), Banki ya CRDB, NMB benki, Halmashauri ya wilaya ya Mbozi, Mbunge wa jimbo la Vwawa ambaye pia aliahidi kutoa msaada wa Kompyuta mwezi Novemba mwaka huu.
Mwisho
No comments:
Post a Comment