Social Icons

Friday, 21 October 2016

Ugomvi wa Skafu ya Chadema Yasababisha Kifo

Na Ibrahim Yassin,Kyela

KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida mkazi wa kijiji cha Kafundo kata ya Ipinda tarafa ya Ntebela wilayani Kyela Mbeya,Stephen Emmanuel amefariki dunia kwa kuchomwa na kisu maeneo kadhaa katika mwili wake na kijana ambaye ni mkazi wa Iringa ambaye jina lake halikufahamika.

Shuhuda wa tukio hilo ambaye ni rafiki wa marehemu,Alimoni Mwanjasi mkazi wa Lufilyo halmashauri ya Busokelo wilayani Rungwe,alisema wakati wa tukio marehemu Emmanuel alikuwa na mdogo wake,Samwel Emmanuel wakinywa pombe kilabuni.

Alisema wakati wanakunywa pombe katika virabu vya Ipinda mjini,kaka wa marehemu alikuwa amevaa skafu ya chadema ndipo alipotokea kijana huyo mkazi wa Iringa aliyefika kijijini humo kwa kazi za ujenzi wa nyumba aliomba apewe skafu kwa kuwa aliipenda.

Alisema baada ya kutopewa Samwel aliinuka kwenda kujisaidia haja ndogo,wakati anatoka kijana huyo alimfuata na kumpiga visu vya shingoni,mkononi na kichwani ambapo mdogo mtu aitwaye Stephen alifika kumsaidia kaka yake ndipo alipopigwa visu maeneo kadhaa na kupoteza fahamu.

Aliongeza kuwa baada ya hapo watu walijaa maeneo hayo wakitaka kuchukua sheria mkononi kwa kutaka kumuua ambapo jeshi la polisi lilifika eneo hilo na kutuliza ghasia na kumchukua mtuhumiwa kumpeleka polisi na majeruhi kupelekwa kituo cha afya Ipinda.

Mwanjasi alisema majeruhi akiwa kituo cha afya alifanyiwa huduma za matibabu na kushonwa sehemu alizochomwa visu lakini baada ya dakika kumi alifariki dunia na kumbeba hadi kijijini kwao Kafundo kwa taratibu za maziko.

Aliongeza kuwa yeye ni mkazi wa kijiji cha Lufilyo Busokelo anafanya kazi ya umachinga huku kijana aliyefariki alikuwa akimsaidia kazi za kuuza na kuzungusha bidhaa zake kabla ya kukutwa na umauti akiwa kirabuni na kaka yake akinywa pombe.

John Ambike Mwenyekiti wa kitongoji cha Kafundo,katika maziko ya kijana huyo yaliyofanyika leo,alisema wao kama wananchi wapo sambamba na familia ya marehemu kuhakikisha sheria inafuatwa kwa kuwa kitendo kilichofanyika ni kosa la jinai.

Alisema kaka wa marehemu ambaye naye alijeruhiwa kwa kuchomwa vifu alitibiwa na kuruhusiwa kurudi nyumbani huku hali yake ikiendelea vizuri.

Hata hivyo jina la mtuhumiwa wa mauaji hayo halikuweza kufahamika ambapo juhudi za kulipata jina hilo zitakamilika pindi atakapo pandishwa kizimbani.

Kamanda wa polisi mkoani Mbeya Dhahiri Kidavashari,alithibitisha kutokea tukio hilo na kuwa  jeshi la polisi limemkamata mtuhumiwa huyo ambaye bado hajapewa jina lake kutokana na kuwa ni mgeni katika kijiji hicho na kuwa uchunguzi unaendelea kabla ya mtuhumiwa kupelekwa mahakani.

Mwisho.

No comments:

Post a Comment