Social Icons

Wednesday, 5 October 2016

Mzee Auawa akielekea Shambani Asubuhi




Stephano Simbeye,
MBOZI:
Mkazi wa kijiji cha Utambalila wilayani Mbozi mkoani Songwe Daimon Simchimba (68)amekufa baada ya kupigwa na kitu kizito kichwani na Huruma Mwashiuya (38) mkazi wa kijiji hicho, anayedaiwa kuwa mtumiaji wa dawa za kulevya aina ya Bangi.

Ofisa mtendaji kijiji cha Utambalila Felix Mwampashe  alisema kuwa tukio hilo lilitokea jana saa 3.00 asubuhi wakati marehemu huyo akielekea kwenye shughuli zake za shamba ndipo aliviziwa na muuaji ambaye alimpiga na kitu kizito kichwani na kusababisha kifo hicho.

Alisema taarifa za mauaji hayo zilitolewa na mtoto wa muuaji ambaye alipiga yowe kuomba msaada ndipo wanakijiji walipojitokeza na kumzingira na kumweka chini ya ulinzi na kisha kumfikisha katika ofisi ya kijiji ambapo walipomhoji alikataa kusema chochote akidai atakwenda kueleza mbele ya safari  sababu za mauaji hayo.

Kamanda wa Polisi mkoani hapa Mathias Nyange amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuwa mtuhumiwa wa mauaji hayo anashikiriwa na jeshi hilo na kuwa bado chanzo cha mauaji hayo hakijafahamika na kwamba uchunguzi wa awali unaonesha kuwa mtuhumiwa ni mvutaji wa bangi iliyomfanya kuchanganyikiwa na kufanya kitendo hicho cha kikatili.

Wakati huo huo Kamanda Nyange amesema mtu mmoja mkazi wa mtaa wa Ipito katika Halmashauri ya mji wa Tunduma Musa Sanga (54) amefariki dunia baada ya kujinyonga kwa kamba ya manila  baada ya kukelwa na kuugua ugonjwa wa kisukari muda mrefu.

Tukio hilo limetokea jana saa 11:40 jioni ambapo mwili wa marehemu ulikutwa unaning’inia ndani ya nyumba yake huko katika kitongji cha Ipito katika kata ya Mpande, Tunduma mkoani Songwe.

Aidha hivi karibuni Kamnda Nyange alikaririwa akisema kila baada ya saa sita linaripotiwa tukio moja la mauaji katika mkoa wa Songwe kutokana na imani za kishirikina, wivu wa mapenzi na migogoro ya ardhi.
Mwisho


No comments:

Post a Comment