Social Icons

Friday, 7 October 2016


na Stephano Simbeye



VWAWA: Viongozi wawili wa kikundi cha wakulima wa kahawa cha kata ya Nambinzo wilayani Mbozi mkoani Songwe, jana walifikishwa katika mahakama ya wilaya ya Mbozi kujibu shitaka la wizi wa kuaminika wa zaidi ya Sh. 674milioni mali ya wakulima wa kikundi cha Nambinzo Coffee kinyume na kifungu cha shertia namba 273 (b) sura ya 16 kanuni ya adhabu kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Ilidaiwa mahakamani hapo na mwendesha mashitaka wa Polisi  Saada Abduli kuwa kati ya Julai 4,2010 na septemba mwaka huo huo washitakiwa hao wakiwa viongozi wa kikundi waliiba fedha tasilimu Sh. 674 milioni  zilizotokana na mauzo ya kahawa kilo 129696 ambazo walikabidhiwa na wanachama wa kikundi hicho ili wakauze katika soko la kimataifa.

Aliwataja washitakiwa hao kuwa ni Mnegro Haonga (43) ambaye ni katibu wa kikundi na Jackson Mwashiuya (22) ambaye ni mtunza hazina wa kikundi hicho.

Hata hivyo washitakiwa hao walikana shitaka linalowakabili na kuiomba mahakama kuwapatia Dhamana, ombi ambalo  hakimu  Mfawidhi  wa mahakama ya wilaya ya Mbozi Asha Waziri anayesikiliza kesi hiyo alisema mahakama itafikiria ombi hilo na kutoa majibu baadaye.

Hivyo washitakiwa hao walirudisha mahabusu hadi Oktoba 20 mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa tena.
Mwisho.

No comments:

Post a Comment