Stephano Simbeye,
Timu ya Soka ya Kimondo SSC ya mkoa
wa Songwe jana ilitoka sale ya bila
kufungana katika mchezo wa ligi kuu Tanzania Bara dhidi ya Coastal Union ya
Tanga, katika mchezo uliochezwa katika uwanja wa CCM Vwawa wilayani Mbozi.
Katika mchezo huo ambao ulianza kwa
kila timu kujihami kwa kucheza kwa tahadhari kubwa huku timu ya Kimondo ikishuhudia kosakosa
nyingi langoni mwa lango la wapinzani wao kutokana na washambuliaji wake
kutokuwa makini.
Kipindi cha Kwanza dakika 45 timu ya
Kimondo ililisakama mara kadhaa lango la mpinzani wake lakini ilionekana washambuliaji
wake kuwa butu baada ya kushindwa kuliona lango licha ya kuwa walitawala kila
idara wakiichezesha mchakamchaka timu hiyo ya wagosi wa kaya.
Baada ya timu ya kimondo kutakata
wakicheza soka safi licha ya kushindwa kuliona lango,timu ya wagosi wa kaya
walianza kujihami wakichelewesha mipira na kujiangusha mara kadhaa wakitaka
wapate sare, hivyo hadi mwamuzi wa mchezo huo Misheki Suda kutoka Singida anapuliza kipenga cha dakika 90 kumalizika timu hizo zilikuwa
hazijafungana.
Akizungumza na waandishi wa
habari,kapteni wa timu ya Costal Union,Mbwana Hamis alisema wamejitahidi kutoka
sare maana mpira ulikuwa mgumu hasa uwanja ulivyo kuwa mbovu ulichangia wao
kupwaya na kuwa mechi ijayo watajipanga ili washinde.
Kocha wa timu ya Kimondo,Fulgence
Novatus alisema vijana wake walicheza vizuri ila walikosa umakini,tatizo ni
umaliziaji,huku kocha wa Costal Mohammed Kampira alikiri kuwa walitingwa na
kusema wanajipanga mechi ijayo watahakikisha wanashinda.
Mkurugenzi wa timu ya Kimondo SSC, Elick
Ambakisye,alisema wameliona tatizo la timu yake ni umaliziaji kwa kuwa kocha
ameliona atalifanyia kazi na kuwa wachezaji wengi muhimu walikuwa majeruhi
walipocheza na timu za Malawi na Zambia katika michezo ya majaribio hivyo mechi
zijazo anaamini watafanya vizuri.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment