Na: Stephano Simbeye
VWAWA: Shule ya
msingi Ilindi iliyopo kata ya Idiwili wilayani Mbozi mkoani Songwe, haina
kitabu hata kimoja kufuatia uhaba wa
vitabu na kufanya walimu walazimike
kuazima kutoka shule jirani ili waweze kufundisha kwa njia ya kuwasomea
wanafunzi wakiwa darasni.
Hayo yalisemwa jana na mwalimu mkuu wa shule hiyo Getrude
Mwasambili alipokuwa akitoa taarifa kwa Mbunge wa Jimbo la Vwawa Japheti
Hasunga kuwa shule hiyo ina uhaba mkubwa wa vifaa vya kujifunzia na kufundishia
kama vitabu vya kiada na ziada ambapo wamelazimika kuazima kitabu kimoja kila
somo kutoka shule jirani ili walau waweze kutimiza malengo ya muhtasari.
Alisema pia shule hiyo ina upungufu wa miundombinu kama
matundu ya vyoo 17, vyumba vya madarasa 8, nyumba 10 za walimu na walimu 7
ambapo hata hivyo wanajitahidi kujipanga kulingana na mazingira yaliyopo ili
taaluma isipotee kabisa.
Mwanafunzi Felista Mwazembe alisema hajawahi kuona kitabu
shuleni hapo na kuwa walimu wamekuwa wakiwafundisha kwa nadharia na kuandika
ubaoni na kwa kutumia karatasi za mitihani zilizotumika katika shule nyingine
ambapo wamekuwa wakifanya mitihani hiyo na kufanya usahii ndipo wanajifunza
zaidi.
“ mwalimu akiingia darasani anatupatia maelekezo kutoka
kitabu alichoshika na kutupa kazi ya kwenda kufanya nyumbani, ambapo
tunafundishana sisi wenyewe kupitia makundi”
Kwa upande wake Afisa Elimu kata ya Idiwili Michael Nzunda
alisema tatizo hilo limeanza mwaka huu baada ya serikali kusitisha kununua
vitabu kutokana na kutaka kuwa na mchapishaji wa aina moja hali ambayo imelit
usumbufu mkubwa kwa walimu na wanafunzi.
Akijibu swali kama kwanini wasitumie fedha za ruzuku
zinazotolewa hivi sasa na serikali alisema fedha hizo zinakuja na maelekezo
maalumu kuwa zitumike katika masuala ya utawala, Michezo, ukarabati na taaluma
kwa ajili ya kuandalia mitihani mbalimbali ya majaribio.
Kwa upande wake Mbunge Japheti Hasunga akizungumzia uhaba wa
vitabu shuleni hapo alisema amegundua
kuwa shule hiyo ina changamoto nyingi, hata hivyo kuhusu changamoto ya vitabu
alisema atajitahidi kutafuta ili walau kupunguza uhaba uliopo ili watoto waweze
kusoma na kuwa pasipo vitabu na vitendea kazi vingine haiwezekani kutoa elimu
bora.
Sambamba na hilo Mbunge Hasunga ametumia muda huo
kuwatahadharisha watu wazima wenye tabia ya kuoa watoto walio chini ya umri wa
miaka 18 na kwamba Bunge limepitisha sheria kari za kuwalinda watoto ili wapate
nafasi ya kusoma na kutimiza ndoto zao.
Mwisho
No comments:
Post a Comment