Social Icons

Sunday, 6 November 2016

Madereva wa Daladala Tunduma Mpemba Watishia kugoma

Stephano Simbeye,

Tunduma: Madereva wa mabasi madogo yanayofanya safari kati ya Tunduma, na Mpemba wilaya ya Momba mkoani Songwe, wametishia kusitisha huduma hiyo kufuatia madai ya kunyanyaswa na askari wa usalama barabarani kwa kuwatoza faini nyingi zisizokuwa na msingi na kuwataka kulipia faini hizo kwa njia ya M pesa.
 
Wakizungumza jana katika mahojiano na waandishi wa habari baadhi ya madereva hao waliokutwa katika kituo kikuu cha mabasi mjini Tunduma  walidai kuwa askari hao wa usalama barabarani wamekuwa wakiwakamata kila wanapowaona na kuwaandikia karatasi za kulipa fain (notification) na iwapo wakiwadai stakabadhi wanawabambikizia makosa mengine.

Mmoja wa madereva hao Ayub John aliyataja makosa ambayo wanakamatwa nayo kuwa ni pamoja na kuzidisha abiria (Level seat) jambo ambalo kwa biashara ya safari fupi ni hasara kutokana na kuwa mabasi hayo madogo yanabeba abiria wachache na nauli yake ni ndogo ya Sh. 500 hivyo iwapo wakipakia abiria  11 hadi 17 kipato wanachopata ni kidogo ukilinganisha na gharama za mafuta kiasi ambacho ni hasara.

Dereva Baton Tumbope alisema iwapo hali hii itaendelea watalazimika kusitisha huduma hiyo kwa kuwa wanaona kazi haiwapatii faida tokana na kero hiyo na kuliomba jeshi la polisi kukaa nao ili kuweka sawa mambo.

“Sisi madereva wa daradara tunanyanyasika na askari wa usalama barbarani wametufanya chanzo cha mapato yao wakati Fulani wanataka tuwaingizie fedha za faini kupitia simu kwa njia ya M pesa na ukihoji kwanini imekuwa hivyo unawekwa mahabusu” alisema Baton Tumbopee

Kiongozi wa madereva hao Patson Simbeye alisema amekuwa akipokea malalamiko ya madereva kila wanapotoka na kurudi kwenye safari zao ya kukamatwa hovyo na kutozwa faini jambo ambalo linawafanya washindwe kutimiza malengo ya biashara na kufanya kazi hiyo kuwa ngumu.

Alisema kufuatia kero hiyo walikwisha peleka malalamiko yao kwa Mkuu wa mkoa wa Songwe na Kamanda wa polisi mkoani hapa lakini bado hayajafanyiwa kazi bado kero hiyo inaendelea.

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi mkoani hapa Mathias Nyange alisema polisi wanafanya kazi zao vizuri kwa kusimamia sheria zilizopo vizuri hata hivyo aliwasihi madereva hao kwa mwenye ushahidi wa kutakiwa kutuma fedha za faini kwa njia ya mpesa waupeleke ili hatua zichukuliwe dhidi ya askari huyo kwani huo sio utaratibu wa malipo ya fedha za serikali.

“ ukiona askari wanalalamikiwa ujue wanafanya kazi zao vizuri katika utendaji huwezi kupendwa, isipokuwa kama kuna suala la kuomba rushwa tunaomba tupatiwe ushahidi ili askari husika achukuliwe hatua za kinidhamu kwa mujibu wa sheria” alisema Kamanda Nyange            
Mwisho.
 
 
 
Stephano Simbeye

Tunduma: Jeshi la polisi mkoani Songwe limekamata kete 200 za madawa ya kulevya aina ya heroin  ambayo thamani yake bado haijajulikana katika msako uliofanywa katika halmashauri ya mji wa Tunduma wilayani Momba.

Kamanda wa Polisi mkoani hapa Mathias Nyange aliwambia jana waandishi wa habari kuwa tukio hilo lilitokea Novemba 3 mwaka huu wakati polisi wakifanya msako wa kubaini watumiaji na wauuzaji wa madawa hayo na kufanikiwa kuwakamata  Watoto wawili wenye umri wa miaka 15 na 17 (majina tunayo) baada ya kukutwa na kete 20 za madawa ya kulevya aina ya heroin

Alisema katika msako huo pia polisi walipata kete 180 za madawa hayo yaliyokutwa katika nyumba moja ambayo mwenye madawa hayo alikimbia kusikojulikana, thamani ya madawa hayo  bado haijajulikana na kuwa jeshi hilo linaendelea na msako kuwabaini wote wanaojihusisha na biashara hiyo haramu.

Kamanda Nyange aliongeza kuwa watu hao watafikishwa mahakamani mara tu upelelezi utakapokamilika pia aliitaka jamii kuacha kujihusisha na madawa ya kulevya kwani mkono wa sheria ni mrefu ambao utawashughulikia kila kona watakayojificha.
Mwisho.
 

No comments:

Post a Comment