Stephano Simbeye , Mbozi
VWAWA: Mkuu wa mkoa wa Songwe Luteni Mstaafu Chiku Galawa
amemfukuza katika mkoa wake Ofisa Mazingira wa halmashauri ya wilaya ya Mbozi
Hamisi Nzunda baada ya kushindwa kutekeleza agizo lake la kufanya usafi kila
jumamosi na kutokuwa na mpango kazi unaeleweka wa kufanya miji kuwa safi.
Hayo yalijitokeza jana alipokuwa akizungumza na wafanyakazi
wa halmashauri hiyo wakati wa kuhitimisha ziara yake ya siku mbili wilayani
hapa ambapo alikuwa anawaita wakuu wa
idara mmoja baada ya mwingine akitaka kupata taarifa zao za utendaji kazi,
lakini ilipofika zamu ya ofisa huyo alishindwa kueleza mikakati aliyo nayo
katika kuweka miji ya Mlowo na Vwawa katika hali ya usafi.
Mkuu huyo wa mkoa alimuuliza ofisa huyo wa mazingira namna
agizo lake la kufanya usafi wa jumla kila Jumamosi, ikiwemo na utekelezaji wa
agizo la Rais la kufanya usafi kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi ambapo katika
majibu yake alikiri kuwa tangu atoe agizo hilo limetekelezwa mara mbili tu
jambo lililomkasilisha Galawa.
“ wewe hunifai
kufanya kazi na mimi sikutaki ndani ya mkoa huu, unachukua mshahara bila
kufanya kazi, tangu nitoe maagizo ya kuwataka kufanya usafi wa jumla kila
jumamosi mmefanya mara mbili tu mnataka Mkuu wa mkoa aje ndipo mfanye
asipokuwepo hamfanyi” alisema Galawa kwa kufoka
Alisema kuna majanga ya moto yanatokea katika maeneo ya
hifadhi lakini hakuna hatua zozote zinazochukuliwa, pia kuna mtu amejenga juu
ya kilima aliagiza aondolewe lakini hakuna hatua zilizochukuliwa huku ujenzi
katika maeneo ya hifadhi ya misitu ukiendelea.
Awali akitoa majibu yake kwa mkuu wa mkoa ofisa mazingira
huyo Hamisi Nzunda alikiri kutotekeleza maagizo ya kufanya usafi kila jumamozi
kutokana na uchakavu wa magari ya kusombea taka kuwa halmashauri ina gari moja
na trekta moja ambayo yote ni machakavu, hivyo kutokidhi mahitaji ambapo taka
zinazozalishwa katika miji hiyo ni nyingi zinazokadiliwa kufikia zaidi ya tani
18 kwa siku.
Alisema katika kutatua tatizo hilo halmashauri imetenga
zaidi ya Sh. 88milioni kwa ajili ya kununua trekta lenye matela mawili kwa
ajili ya kazi hiyo.
Kwa upande wake Mkurugenzi mtendaji wa halmashuri ya Mbozi
Edina Mwaigomole alisema halmashauri yake imeandaa sheria ndogo inayowataka wazalishaji
wa taka kuchangia gharama za kuzoa taka ili kuondoa mlundikano wa taka katika
miji.
Alisema katika mpango huo wanatarajia kuwatumia vijana wenye
pikipiki za magurudumu matatu ambao watapita kila mtaa kukusanya taka majumbani
na kwenda kuzitupa kweny dampo na kuwa mpango huu pia utatoa ajira kwa vijana
ambao watalipwa asilimia 70 ya makusanyo ya fedha ya uchagiaji.
Hata hivyo suala la usafi liliibuka pia katika mkutano wa
hadhara kwenye mji mdogo wa Mlowo ambapo mkazi wa mji huo Mawazo Mdolo alisema
serikali ihamishe ghuba lililopo karibu na makazi ya watu kutokana na
mlundikano wa taka ambao unatishia afya za wakazi wa eneo hilo.
Alisema wamekuwa wakifuatilia suala hilo katika mamlaka ya
mji huo lakini majibu wanayopatiwa hayawaridhishi hivyo kuona kama serikali
haijali afya zao na watoto wao ambao wanaweza kushambuliwa na magonjwa ya
mlipuko kama kipindupindu na kuhara.
No comments:
Post a Comment