Stephano Simbeye, Mwananchi
Vwawa: Mkuu wa mkoa wa Songwe Luteni Mstaafu Chiku Galawa
ameujia juu uongozi wa hamashauri ya Mbozi kufuatia kushindwa kutoa mikopo kwa
vijana na wanawake kama ilivyoagizwa na serikali, kuzitaka halmashauri kutenga
asilimia 10 ya mapato yake kwa ajili ya kuvikopesha vikundi hivyo badala yake
imezielekeza fedha hizo kwenye matumizi mengine.
Hayo yanafuatia
malalamiko ya mkazi wa Vwawa Said Adamu ambaye aliuliza swali katika mkutano wa
hadhara akidai serikali ilitoa ahadi ya kukopesha mikopo yenye masharti nafuu
kwa vijana na wanawake lakini mikopo hiyo hawaioni na kudai apewe maelezo
kikwazo ni nini.
Katika majibu yake Ofisa Maendeleo ya jamii Msolini Dakawa alisema
mikopo imeendelea kutolewa licha ya kuwa ni kidogo ambapo hadi sasa zaidi ya
Sh. 39 milioni zimekopeshwa katika nusu ya mwaka huu wa fedha na kuwa kazi hiyo
inaendelea kadiri fedha zinavyopatikana.
Akifafanua zaidi Dakawa alisema fedha hizo zimetolewa kwa
vikundi 20 vya wanawake na 10 vya vijana ambapo imeidhinishwa wiki iliyopita na
kamati ya mikopo.
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya Edina
Mwaigomole akitoa ufafanuzi alisema halmashauri yake imeshindwa kutekeleza
agizo hilo kutokana na kutingwa na kazi za utengenezaji wa madawati atika msimu
uliopita na kuwa fedha hizo zitatolewa katika kipindi hiki kinachoendelea.
Alisema halmashauri katika nusu ya mwaka wa fedha uliopita
imekusanya zaidi ya Sh. 1.5 bilioni ambapo ilistahili kuwa iwe imetoa mikopo
kwa makundi ya vijana na wanawake zaidi ya Sh. 150 milioni lakini haikufanikiwa
kutokana na changamoto ya mwingiliano wa majukumu.
Hata hivyo sababu hizo hazikumridhisha mkuu huyo wa mkoa
ambapo alikuja juu na kuanza kutoa maelekezo kwamba kushindwa kutoa fedha hizo
kwa makundi husika ni sawa na kutengeneza bomu kwa serikali ambalo litaleta
tatizo baadaye na kuwa ni kuwadhuumu wanyonge haki yao ya msingi.
“ serikali ilipoweka utaratibu huo ilijuwa kuwa halmashauri
zina majukumu mengi lakini mnashindwa kufanikisha haya kutokana na uzembe wenu
wa kushindwa kukusanya mapato ya ndani lakini kama mungekuwa mnaumiza vichwa
kutafuta mapato haya yasingewasumbua” aisema Mkuu huyo wa mkoa
Galawa alitumia muda huo kuiagiza halmashauri kuhakikisha
inakamilisha kutoa mikopo iliyosalia ifikapo mwezi februari mwaka ujao na
taarifa aipate mapema ofisini kwake.
Sambamba na hilo mkuu huyo wa mkoa aliwataka wataalamu wote
wa idara ya maendeleo ya jamii kuhamia katika vijiji ambako ndiko kwenye watu
ili wakawaelimishe namna ya kutumia mikopo hiyo ili iweze kutumika kama mbegu
ambapo ikiota waweze kurejesha na wengine wakopeshwe.
mwisho
No comments:
Post a Comment