Stephano Simbeye - TUNDUMA:
Mkuu wa mkoa wa Songwe Luteni Mstafu Chiku Galawa
ametoa siku saba kuanzia jana kwa wafanyabiashara wanaoendesha shughuli zao kwenye eneo la mpaka kati ya Tanzania na Zambia mjini Tunduma
wilayan Momba, kuhama katika eneo hilo na kuhamia maeneo mengine yaliyotengwa
na halmashauri ya mji huo.
Kauli hiyo aliitoa jana wakati alipofanya ziara kukagua
mpaka huo ambao umevamiwa na wafanyabiashara
katika eneo hilo ambalo halipaswi kufanywa shughuli yoyote mita 50 kutoka
kwenye jiwe la mpaka kila upande na kueleza kuwa serikali imetenga maeneo
kadhaa ya kufanyia biashara ili watu wake wasivunje sheria za kimataifa
zinazolinda mpaka huo.
Aliwaambia baadhi ya wafanyabiashara hao kuondoa kila kitu
na kuacha mpaka wazi katika umbali unaokubalika na kuachana kuendesha shughuli
zao kwa kiholela jambo ambalo linaleta sura mbaya kwa nchi jirani ya Zambia na
nchi nyingine zilizo Kusini mwa Afrika kutoakana na kuwa mpaka wa Tunduma ni
mapokezi ya wageni wanaoingia nchini Tanzania.
Galawa alisema kitendo cha wafanyabiashara hao kukaa karibu
ya mpaka kinatowa mwanya kwa watu wenaopitisha mizigo ya magendo kuingia nchini
bila kujulikana hali ambayo pamoja na kuikosesha serikali mapato lakini pia
inafanya mpaka huo kuwa holela kwa watu wake kutofuata taratibu na hivyo
kuwataka kubadilika na kuondokana na mazoea waliyokuwa nayo.
“ hebu angalieni wenzenu nchi jirani kattika eneo lao la
wazi wamelitunza na kupanda miti hali ambayo inalifanya lipendeze, lakini huku
kwetu lipo kiholela jambo ambalo linaleta sura mbaya hivyo shughuli hizi za
magereji, uegeshaji magari, maaduka wakiwemo wauza mazao na mkaa sitaki kuwaona
hapa baada ya muda huo kupita name nitakuwa nikipita kila wiki na wewe DC
hakikisha utekelezaji wa agizo langu” alisema Galawa
Mmoja wa wafanyabiashara aliyekutwa eneo hilo ambaye anatoka
upande wa Zambia Joel Siame alisema eneo hilo amekuwa akilimiliki miaka mingi
lakini kwa kutambua kuwa lipo katika mpaka aliandika barua ofisi ya Mkurugenzi
wa Tunduma ili aweze kupimiwa aweze kuendeleza shughuli zake kihalali.
Braight Ngwila mkazi wa Nakonde alimwambia mkuu huyo wa mkoa
kuwa wamekuwa wakilitumia eneo hilo kama viwanja vya michezo na kuwa viongozi
wa pande zote akiwemo mwalimu Julius Nyerere waliwataka kulitunza pasipo
kufanya shughuli nyingine bali liwe eneo la amani.
Alisema katika kipindi kirefu wamekuwa wakiishi kama ndugu
kwa kushirikiana katika mambo mbalimbali hivyo si vizuri wakaanza kugombana kwa
ajili ya eneo ambalo waasisi wan chi hizo waliagiza liwe la amani.
Mmoja wa wafanyabiashara katika eneo hilo Beaty Mwasyeba
aliomba serikali kuwapa muda zaidi ili waweze kuhama katika eneo hilo ombi
ambalo hata hivyo lilikataliwa na mkuu huyo wa mkoa kwa madai kuwa wapo katika
eneo hilo kwa kuvunja sheria hivyo waharifu hawawezi kupewa muda zaidi ili
waendelee kufanya uovu.
Mwasyeba alisema wanalazimika kuwepo katika eneo hilo ili
kuwa karibu na wateja ambao wengi wanatoka nchini Zambia na kuwa hawawezi
kufika kwenye maeneo mengine kwa kuhofia kuvunja sheria.
Rose Damsoni alisema kitendo cha wafanyabiashara wengine
kukaa katika maeneo yasiyo rasmi kinawafanya walioko kwenye masoko maalumu
kukosa wateja lakini iwapo kila mmoja akatimiza wajibu wake kwa kuhamia eneo
rasmi hali itabadilika.
Kwa upande wake Mkurugenzi mtendaji wa Mji wa Tunduma Valery
Kwembe alisema halmashauri imetenga maeneo mawili katika soko la kimataifa
ambako wafanyabiashara hao walipewa na kujenga vibanda zaidi ya 2000 lakini
hawataki kwenda kulitumia eneo hilo na eneo linginne limetengwa katika eneo la
Kaloleni kwa ajili hiyo.
Aidha alisema yeye pamoja na timu yake siku ya kesho (jana)
watakwenda kuwaonesha wale wote ambao hawajapata eneo la kuweka vibanda vyao
ili waweze kuendesha biashara zao.
Hata hivyo katika eneo la mpaka wa Tunduma ambalo limekuwa
likikuwa kwa kasi limejengwa kiholela, hali inayofanya baadhi ya watu kujenga
kwenye eneo la wazi la mpaka huku upande mmoja wa nyumba ukiwa Tanzania na
upande mwingine ukiwa Zambia hali inayofanya hali ya ulinzi hasa udhibiti wa
biashara za magendo kuwa mgumu.
mwisho
No comments:
Post a Comment