Social Icons

Sunday, 25 December 2016

WAZIRI wa Maji na Umwagiliaji




 – Mbozi

WAZIRI wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Gerson Lwenge amezitaka mamlaka za maji kote nchini kuhakikisha zinatia dawa ya kutibu maji kabla ya kuyasambaza kwa wananchi ili kujiridhisha kuwa maji yanayosambazwa ni safi na salama.

 Agizo hilo alilitoa mwishoni mwa wiki wakati akiongea na wataalamu wa sekta ya maji mkoani Songwe wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku mbili kuwa hivi sasa serikali imeondoa kodi ya ongezeko la tamani kwenye dawa za kutibu maji hivyo gharama yake kupungua na kuwa hapatakuwa na sababu yoyote ya kushindwa kutia dawa kwenye maji kabla ya kuyasambaza kwa wananchi.

Lwenge alisema sambamba na kutibu maji amezitaka pia mamlaka hizo kuhakikisha wakazi waliopo kwenye vyanzo vya maji wanapatiwa huduma hiyo ili waweze kuwa na ari ya kuvitunza, badala ya kuwaacha wakiyaona tu maji yakipelekwa maeneo mengine na wao wakihangaika hawana maji  safi na salama.

“ si vizuri watu waliopo kwenye vyanz wakaachwa bila huduma hata kama maji ni kidogo nao wafikiriwe kwani wakati huu tunayaona maji kidogo ya mgawo lakini iwapo tusipotunza vyanzo na mazingira utafika wakati hata hayo maji kidogo hatutayaona na hapo ndipo hali itakuwa mbaya zaidi,”alisema Waziri Lwenge

Awali akiwasilisha taarifa ya mkoa mkuu wa mkoa wa Songwe Luteni Mstaafu Chiku Galawa alisema mkoa unakabiliwa na upungufu wa lita 12 milioni za maji kila siku kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kukauka kwa vyanzo vya maji, miundombinu michakavu na ukame wa muda mrefu.

Alisema mkoa umeweka mkakati wa kvuna maji ya mvua kwa kuhakikisha kila anayetaka kujenga anaonesha namna atakavyovuna maji na kuwa utekelezaji wa mkakati huo umeanza katika taasisi za umma ili kuwaonesha mfano wananchi.

Kwa uande wake Kaimu Meneja wa Mamlaka ya maji Vwawa Akiba Kibona alikiri kutokuwa na mitambo ya kusafisha maji na hivyo kutokuwa na maji safi, hata hivyo alisema wamekuwa wakitia dawa ya kuua wadudu kabla ya kuyasambaza kwa wananchi.

Alibainisha kuwa hivi sasa wmeandaa andiko la kuomba fedha ili kujenga mtambo wa kusafisha maji kabla ya kuyapeleka kwa wananchi.

Mkazi wa Mlowo Evarine Kayange alitupia lawama mamlaka ya maji kwa kushindwa kuwawekea huduma hiyo katika eneo lao ambako kuna chanzo cha maji cha Lutumbi hali ambayo ilisababisha baadhi ya watu kukata bomba ili nao wapate huduma hiyo.

Aidha aliiomba serikali kuweka alama katika maeneo ambayo hayastahili kufanyika shughuli za kibinadamu ili kuondokana na migogoro na watendaji kwakuwa wananchi wengi wanashindwa kuelewa  wapi hawastahili kufika.
Mwisho.

 

No comments:

Post a Comment