Stephano Simbeye, Mbozi
Kamati ya Ushauri ya mkoa wa Songwe imeridhia ofisi
za mkuu wa mkoa kujengwa katika kijiji cha Nselewa kilichopo kata ya Mlowo
wilaya ya Mbozi na kuazimia kuuanzisha Manispaa ya Mbozi na halmashauri ya Mbozi.
Suala la wapi zijengwe ofisi za mkuu wa mkoa limekuwa
likijadiliwa na watu wa lika mbalimbali tangu kuanzishwa mkoa, hivyo kuwapo kwa
makundi yanayovutana kila moja likivutia upande
wake, lakini pia makundi hayo yakijihusisha na Siasa, hivyo kufanya kuwa
ajenda ya kuzungumzwa kila mahali.
Hata hivyo jana katika kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa
(RCC) ili kupata eneo la kujenga ofisi hizo,wajumbe walizingatia vigezo kama
vilivyoainisha na wataaamu ambapo maeneo hayo mawili yalilingana vigezo hali
iliyofanya uamuzi kupatikana kwa kupiga kura na eneo la Nselewa kupata kura
nyingi huku eneo la Hasamba likipata kura moja.
Akiwasilisha azimio la kamati ya ushauri ya wilaya ya Mbozi
(DCC) mkurugenzi wa halmashauri Edina
Mwaigomole alisema kamati hiyo iliazimia kuwa ofisi ya mkuu wa mkoa
ijengwe katika eneo la Hasamba kutokana na eneo hilo kuwa tulivu kwa kuwepo
ikulu ndogo, pia fidia ya mashamba ni kidogo na kuwa eneo la Nselewa halifai
kutokana na kuwa karibu na barabara na shughuli za watu, hivyo linaweza
kusongwa na watu na pia fidia ya mashamba ya watu ni kubwa.
Akizungumzia uundaji
wa Manispaa ya Mbozi na halmashauri ya Mbozi mkurugenzi huyo alisema kamati
ilipendekeza manispaa kuundwa na kata 18, huku halmashauri ikibaki kuwa na kata
22 zenye vijiji 101 na vitongoji 540 na kuwa Manispaa itakuwa na idadi ya watu
140000.
Mwenyekiti wa halmashauri ya Tunduma Ally Mwafongo akijadili
alisema ni vizuri ofisi za mkuu wa mkoa zijengwe Nselewa ili kuleta madhari
nzuri ya mkoa kwa vile eneo hilo lipo katika mwiinuko na kuwa patapendeza zaidi
na kuwa mapendekezo ya kuunda manispaa yabaki jinsi yalivyo.
Mbunge wa Jimbo la Vwawa Japheti Hasunga alisema iwapo
uamuzi utatolewa kujenga ofisi za mkuu wa mkoa eneo la Nselewa ni eneo ambalo
kutokana na kuwa jirani na makazi, shughuli za watu na kuwapo na barabara kuu
ya Tunduma – Dar es salaam patasongwa muda mfupi na hivyo kuleta usumbufu.
Alisema sababu ya kupendekeza eneo la Hasamba pajengwe ofisi
hiizo ni kuwa eneo hilo ni tulivu kwa staha ya kimkoa, kiusalama na kuwa
panafaa hata kujenga Ikulu ndogo kwa ajili ya kupumzikia Rais ukilinaganisha na
Nselewa.
Hasunga aliongeza kuwa eneo la Hasamba halihitaji kuwafidia
watu kwani ni la serikali ambalo lilikuwa linamilikiwa na walowezi na baadaye
kuchukuliwa na serikali ambayo ililikodisha kwa wananchi , lakini pia
litarahisisha mawasiliano kati ya wilaya ya Ileje na makao makuu ya mkoa na pia
wakati wa Kampeni za uchaguzi Rais aliwaahidi wananchi kuwajengea barabara yenye urefu wa kilometa 7
kuelekea eneo hilo
Mbunge wa Jimbo la Mbozi Pascal Haonga alipendekeza Nselewa
ili kuunganisha miji ya Mlowo na Vwawa kuwa Manispaa moja pia wageni wataweza
kuona kitu kipya na kuwa sababu zozote zinazotolewa hazina msingi wowote.
Awali Mwenyekiti wa kikao hicho mkuu wa mkoa Songwe Chiku
Galawa aliwaeleza wajumbe kuwa taasisi za mkoa zinapaswa kusambazwa katika
maeneo tofauti ili kusambaza huduma kwa jamii na kuwa huduma kama hospitali ya
rufaa ya mkoa, Chuo kikuu, Uwanja uwanja wa michezo, VETA na taasisi nyingine
zitaekwa katika maeneo mengine ndani ya manispaa ya Mbozi.
Alisema wazo la kujenga taasisi zote katika eneo moja
halitafaa kwa sasa bali zitasambazwa ili kila mwananchi aguswe.
Kwa upande wa wananchi wakazi wa mji wa Vwawa baada ya
kupata taarifa za kuteuliwa kwa eneo hilo walitaharuki huku wakiwa katika
makundi wakijadili suala hilo kwa masikitikiko huku wenzao wa eneo la Mlowo
wakipokea taarifa hizo kwa furaha na shangwe.
Nivard Lwila ni mkazi wa Vwawa alisema inasikitisha kuona
kuwa ahadi ya Rais na aziri mkuu wa
awamu ya nne waliyoitoa wakati alipofika kuomba kura imepuuzwa ambapo pia
aliahidi kujenga kilometa 10 za barabara ya lami kuelekea eneo la hasamba
lilikopendekezwa kujengwa ofisi za mkuu wa mkoa.
“sasa mji wa Vwawa unazidi kumalizwa nadhani hatuna wawakilishi
maana wameshindwa kutetea mapendekezo ya awali”alisema Lwila
Naye Sailas Kayuni mkazi wa Mlowo alisema kilichotokea ni
ushindi ambao unatokana na viongozi wao kuwa mahili wa kuwasilisha hoja.
Aidha awali maeneo matatu ndiyo yaliyopendekezwa kujenga
ofisi za mkuu wa mkoa ambayo ni pamoja na eneo la Oldvwawa, Mbimba Tacri na
Hasamba na baadaye kuongezwa eneo la Nselewa ambalo halikuwepo kwenye
mapendekezo ya awali.
Hata hivyo maeneo yote manne yaliyopendekezwa yalifanyiwa utafiti na
wataalamu ambapo maeneo mawili ndiyo yaliyokidhi vigezo ikiwemo uwezo wa udongo
kuhimili kujengwa majengo marefu ikiwa ni eneo la Nselewa na Hasamba.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment