Social Icons

Thursday, 29 December 2016

RC Galawa Atofautiana na Wafanyabiashara Vwawa



 Stephano Simbeye, Mbozi

Wafanyabiashara wa mji wa Vwawa wilayani Mbozi mkoani Songwe wametofautiana na kushindwa kuelewana na mkuu wa mkoa huu Chiku Galawa kuhusiana na eneo la kujenga ofisi ya mkuu wa mkoa.

Hali hiyo ilijitokeza jana katika mkutano ulioitishwa na mkuu huyo wa mkoa kwa lengo la kifahamiana ambapo mwishoni mwa mkutano huo alitowa nafasi ya kuulizwa maswali ndipo likajitokeza suala la eneo la kujenga ofisi ya mkoa ambapo baadhi ya wauliza maswali walitaka kufahamu kilichosababisha kuwepo mabadiliko tofauti na walivyotarajia.

Raphael Kibona alianza kwa kueleza kuwa awali makao makuu ya mkoa wa Songwe yalipangwa kuwa katika kata ya Vwawa lakini kuna mabadiliko ya eneo hilo, je ninani aliyegushi na kuyapeleka Nselewa katika kata ya Mlowo na aliyefanye hivyo Takukuru wanamchukulia hatua zipi.

Kwa upande wake Joel Kasebele aliomba ufafanuzi toka kwa mkuu wa mkoa kuhusu eneo la kujenga ofisi za mkoa na ni vikao vipi vimebatilisha uamuzi wa vikao vya ngazi ya chini ambavyo viliazimia ofisi hizo kuwa eneo la Hasamba badala yake uamuzi huo umetenguliwa.

“ kitedo cha kubadili maamuzi ya awali kimekiuka hata taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi iliyotolewa na Mbunge aliyepita na hapa naomba nitoe kielelezo cha taarifa hiyo”alisema Kasebele

Naye Mwenyekiti wa wafanyabiashara wilayani Mbozi Yohana Mwajeka alisema kuwa kwa upande wao wafanyabiashara hali si shwali kwani walitarajia kuwa iwapo ofisi za makao makuu ya mkoa zikijengwa katika mji huu zitasaidia kuchangamsha mji ambao umezorota kibiashara ukilinganisha na miji mingine ya Mlowo na Tunduma.

Alisema walitarajia kuwa ofisi hizo pamoja na nyingine za taasisi na serikali zingeweza kuongeza idadi ya watu wanaokuja kufuata huduma ikiwa ni pamoja na watumishi wataongeza mzunguko wa fedha ili nao waweze kupata maendeleo na kuinua uchumi wa n chi kwa ujumla.

Akijibu maswali hayo mkuu wa mkoa Luteni Mstaafu Chiku Galawa alisema serikali inafanya kazi kwa maandishi tangazo la serikali la kuanzisha mkoa wa Songwe limeeleza kuwa makao makuu ya mkoa yatakuwa wilaya ya Mbozi na hapo hakuna aliyebadilisha na ndiyo maana tumekuja Mbozi na kuwa tangazo hilo halikueleza kwa maandishi katika maeneo hayo yanayotajwa.

Alisema tumejipanga kufanya kazi kuleta maendeleo ya mkoa wa Songwe wenye halmashauri tano  na uwa kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa (RCC) imeamua kujenga ofisi ya mkuu wa mkoa na si makao makuu na tunatarajia ofisi za idara nyingine zitatawanywa maeneo mbalimbali ili kuleta usawa ili kila mwananchi aguswe.

Galawa aliongeza kuwa mawazo ya wafanyabiashara kuwa ofisi ya mkuu wa mkoa italeta mabadiliko ya kibiashara si sahihi kutokana na kuwa ofisi hiyo ina wafanyakazi wachache ambao hawawezi kuzidi 120, jambo la msingi kwa wakazi wa Vwawa ni kufikiria namna ya kuboresha biashara zao kwa kushirikiana kwa kuunda ya kuanzisha mabaraza ya biashara ambayo yatasaidia kuwaweka pamoja.

Aidha alisema kazi ya ofisi ya mkuu wa mkoa haifanyi kazi za kila siku za kuonana na wananchi bali kazi hiyo hufanywa na halmashauri za wilaya, na kazi ya mkoa ni kusimamia wilaya na kuinua kipato cha wananchi kutoka hapo walipo na kuwa bora zaidi na hiki ndicho kipimo chake.



Aliwasihi wafanyabiashara hao kuwa na maono ya mbali kutumia fursa za viwanda zinazokuja ikiwa ni pamoja na uwepo wa chuo kikuu, chuo cha ufundi stadi, hospitali ya mkoa na kuwepo kwa migodi mikubwa  ambavyo  vitachochea uchumi na biashara zao kukua

Hivi karibuni kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa wa Songwe kiliazimia kwa kupiga kura kuwa ofisi ya Mkuu wa mkoa huu ijengwe katika eneo la Nselewa na idara nyingine za serikali zitatawanywa katika maeneo mbalimbali ya wilaya ya Mbozi, hata hivyo uamuzi huo umeonekana kutokubaliwa na wakazi wengi wa Vwawa kutokana na sababu mbalimbali.
Mwisho



No comments:

Post a Comment