Na: Danny Tweve - Mlowo
ASKOFU wa Kanisa la KKKT DAYOSISI YA KONDE
DR ISRAEL PETER MWAKYOLILE amesema kuna haja kubwa kwa wananchi wa Tanzania
kuunga mkono jitihada za Rais John Pombe
Magufuli anazozifanya katika kusafisha serikali yake na wananchi pia kuwa
sehemu hiyo ya usafi.
Akizungumza wakati wa kuhitimisha zoezi la
usafi wa mazingira katika mji mdogo wa Mlowo wilayani Mbozi mkoa wa Songwe ambako
alikuwa mgeni rasmi askofu Mwakyolile alisema, wakati Magufuli akisimamia usafi
na uadilifu wa watendaji wa serikali, wananchi nao wanapaswa kuwa wasafi tangu
kwenye kaya zao, maeneo yao ya biashara na mazingira wanayoyazunguka ili kwa
pamoja kuifanya nchi kuwa edeni njema.
Alisema wakati Mungu akiwaweka watu wake
kwenye bustani ya Edeni, alitarajia kuwa wangeyafaidi mema ya bustani hiyo
lakini kwa bahati mbaya ushawishi wa shetani uliwapotosha watu wale sawa na
sasa ambapo nchi zetu zimekuwa na kila namna ya fursa na utajirj lakini baadhi
ya watu wametumia vibaya fursa hizo kwa kujinufaisha binafsi.
Akizungumzia zoezi la usafi wa mazingira,
Askofu Mwakyolile alisema kuwa wakati huu tunapoingia kwenye kipindi cha
masika, ni dhahiri kutajitokeza milipuko ya magonjwa hasa kipindupindu hivyo ni
vyema wananchi wakajielekeza kuhakikisha kuwa wanajali usafi kwenye maeneo yao.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Mbozi John
Palingo alisema hatua ya kushirikisha viongozi wa kiroho kwenye kampeni za
usafi inalenga kuongeza ushiriki wa wananchi kwenye jukumu hilo hasa kutokana
na ukweli kwamba viongozi hao wamekuwa na ushawishi mkubwa kwa waumini wao.
Alisema eneo la Mlowo ni miongoni mwa maeneo
ya kimkakati katika masuala ya usafi wa mazingira na kwamba kupitia utaratibu
wa usafi kila Jumamosi, wananchi watakuwa wakijisimamia wenyewe kwenye maeneo
yao na hivyo kupunguza uwezekano wa kukumbwa na magonjwa ya mlipuko kutokana na
uchafu.
Zoezi hilo limehusisha wananchi,
wafanyabiashara, viongozi wa ngazi mbalimbali na waendesha bodaboda ambapo watu
wanaokaidi maelekezo pia walitozwa faini za papo kwa papo kiasi cha shilingi
50,000/=kwa kaya
Mwisho.
No comments:
Post a Comment