Social Icons

Friday, 13 January 2017

Kijiji Chakabidhiwa Zahanati, Wanafunzi Kukatiwa Bima ya Afya ya Msingi, wazazi wao kunufaika pia



Na: Stephano Simbeye, Mbozi

Wakazi wa kijiji cha Manyara kilichopo kata ya Nambinzo wilayani Mbozi mkoani Songwe wamekabidhiwa jengo la zahanati, lililojengwa kwa msaada wa shirika la Good neighbors Tanzania kwa msaada wa ufadhiri wa watu wa Jamhuri ya Korea Kusini, huku wanafunzi wa shule ya msingi kijijini hapo wakipatiwa msaada wa sare, huduma za afya, daftari na chakula cha mchana.

Akizungumza jana katika hafla fupi ya kukabidhi jengo hilo, Meneja Uendeshaji wa Shirika la hilo Erick Athuman alisema kuwa shirika lake liliamua kujenga zahanati katika kijiji hicho baada ya kuona wakazi wa eneo hilo wanakabiliwa na tatizo la kufuata huduma za afya umbali mrefu huku katika kijiji hicho kinachokabiliwa na uhaba wa maji safi na salama na kusababisha tatizo la magonjwa ya kuhara, kichocho na homa ya matumbo hasa kwa watoto ambao walifanyiwa uchunguzi wa kitabibu.

 Alisema shirika lake lina lengo la kuhudumia watoto wanaoishi katika mazingira magumu hivyo mara baada ya kufika katika kijiji hicho walianza kufanya utafiti kwa kuwapima wanafunzi wote waliopo katika shule hiyo ili kubaini hali ya afya ya wanafunzi ambapo hata hivyo walibaini kuwapo kwa tatizo ambalo ndio chimbuko la kujenga zahanati, kuchimba kisima cha maji safi na salama katika vijiji vya Nambinzo, Shitunguru na Manyara.

Aliongeza kuwa shirika lake pia linatarajia kuwaunganisha wanafunzi 1200 wa kata hiyo katika huduma ya afya ya msingi (CHF) ambapo idadi hiyo itakwenda sambamba na kaya wanazotoka kama ilivyo ambapo watu sita katika kaya watanufaika.

Akizungumzia Zahanati Athuman alisema kazi ya ujenzi imekamilika kwa asilimia zaidi ya 90 na kuwa kilichosalia ni kuweka vioo vya madirisha kazi ambayo inaendelea kufanywa na mkandarasi Kampuni ya MIROGENA toka Mbozi na shirika litaweka vitanda kwa ajili ya kujifungulia akina mama wajawazito.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa shirika la Good neighbors Tanzania Sung Me Sung akizungumzia miradi ya Shirika hilo alisema inalenga kuiendeleza jamii kwa kuweka huduma za jamii kama kupunguza tatizo la ndoa za utotoni, kuwakwamua watoto wanaonyanyaswa, kutoa msaada wa kisheria ili kuona jamii ya atoto inaishi vizuri na kupata elimu bora.

Aidha alisema shirika lake limetenga zaidi ya Sh. 1 bilioni kwa ajili ya kufanikisha miradi yake katika mkoa wa Songwe ambayo ni pamoja na kutoa huduma za afya kwa watoto, kutoa vifaa vya shule, sare, kuchimba visima, kutoa pembejeo za kilimo ili kuinua uzalishaji katika kilimo na kuwalipia bima ya afya kaya zaidi ya 1200.

Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Manyara Alinanuswe Mwanyalu alisema kuwa misaada iliyotolewa na shirika hilo imesaidia kupunguza utoro shuleni hapo ambapo kabla ya kuanza mahudhurio yalikuwa mabaya yaliyochangia taaluma kushuka, lakini kwa sasa mahudhurio ya wanafunzi ni mazuri.

Aliitaja baadhi ya misaada inayotolewa shuleni kwake kuwa ni pamoja na kila mwanafunzi kupewa sare za shule ikiwemo kaputura, shati na sweta, daftari na kalamu na kila baada ya miezi mitatu wanapatiwa chakula hali ambayo pia inatia motisha kwa wanafunzi kuhudhuria shuleni.

Mwanyalu alisema pamoja na misaada hiyo ya mavazi lakini pia shirika hilo limechimba kisima kirefu kuwezesha kupatikana kwa maji safi na salama wakati wote shuleni jambo ambalo nalo limepunguza magonjwa ya mara kwa mara kwa wanafunzi na kuwawezesha kuhudhuria masomo mfululizo.

Mkazi wa kijiji hicho Kitalina Mwakajila alisema kukamilika kwa ujenzi wa jingo la zahanati hiyo litawasaidia kuondokana na kero ya kwenda mbali kufuata huduma za afya ambapo wakati mwingine wagonjwa walifia njiani wakati wakipelekwa kwenye matibabu ambako ni mbali.

Alisema ujio wa zahanati yao ni tumaini jipya kwa afya zao kwani kijiji chao ni kipya ambacho huduma nyingi za kijamii hazipatikani.

Mgeni rasmi katika hafla hiyo Katibu Tawala wilayani hapa Tusubilege Benjamini alisema wakazi wa kijiji hicho wanapaswa kuitumia vizuri bahati waliyoipata ya kujengewa zahanati kwa kuitunza na kutumia nguvu hiyo kujenga nyumba ya mganga haraka ili ianze kutumika.

Alisema fedha zilizotolewa na mfadhili ni kodi za wananchi wa Korea Kusini, zitafsiliwe kwa wakazi wa kijiji hicho nao kuchangia zaidi katika maendeleo ikiwa pia ni chachu ya kujiletea maendeleo.

Aidha Katibu Tawala huyo ambaye pia alimwakilisha mkuu wa wilaya ya Mbozi John Palingo alitumia fursa hiyo kuwaasa wakazi wilayani Mbozi kuacha mara moja tabia ya kuwakatisha masomo na kuwaoza watoto wa kike na kuwa kufanya hivyo kutawapelekea kukabiliwa na rungu la sheria mpya ya mtoto ambapo ni kifungo kisichozidi miaka 30, na wahusika wengine wakihukumiwa kifungo cha miaka mitano na faini ya Sh. 5 milioni.
Mwisho.





No comments:

Post a Comment