Na: Bershaza Mwabenga, Mbozi
Wananchi mkoani Songwe wametakiwa kujiunga katika vikundi vya
ujasiriamali ili kupunguza changamoto mbalimbali za kimaisha na ukali wa maisha
kuliko kufanya shughuli za kiuchumi wakiwa mtu mmoja mmoja.
Wito huo umetolewa na mwenyekiti wa kikundi cha mshikamano Meshack
Mwambogolo wakati wa maadhimisho ya mwaka mmoja ya kikundi hicho yaliyoambatana
na zoezi la upandaji miti 300 katika shule za msingi Mlowo Na Itete zilizopo
katika kata ya Mlowo wilayani Mbozi mkoani Songwe.
Mwambogolo alisema kuwa wananchi wanatakiwa kujitokeza kujiunga katika
vikundi ikiwemo kujiunga na kikundi cha mshikamano ili kiweze kusajiliwa kama
saccos kuliko kubaki kama kikundi cha ujasiaramali ambacho idadi ya wananchama
ni chache hivyo ili kuwa saccos ni vyema watu wakajitokeza kujiunga na kikundi
hicho.
Akizungumza wakati wa hafla ya kuadhimisha mwaka mmoja wa kikundi hicho
mzee Alan Mwampamba alisema kuwa wanakikundi hicho wanatakiwa kushikamana kwa
pamoja kuliko kuwa na vikundi vya mpito ambavyo havina mwendelezo na wasikubali
kamwe kuruhusu mianya ya migogoro ambayo itawafanya kupunguza mshikamano na
umoja ndani ya kikundi.
Naye mshauri kutoka ofisi ya ushirika mkoani Songwe Fredy Katundu alisema
kuwa kikundi hicho kiwe mfano kwa vikundi vingine ambavyo vimewahi kuanzishwa
na kuishia kuwa na dhuluma kwa wanachama huku viongozi wa vikundi wakiwa na
jeuri ya kutofikishwa mahakamani kwa kukosa ushahidi hali iliyochangia wilaya
kushindwa kukopesheka na taasisi za kifedha.
Kwa upande wake mgeni rasimi mkuu wa wilaya ya Mbozi John Palingo
akimwakilisha mkuu wa mkoa wa Songwe alisema kuwa ushirika ndiyo njia pekee ya
kumkomboa mwananchi wa hali ya chini na kumuinua kiuchumi.
Aidha Palingo aliongeza kuwa kikundi hicho kinahitaji kuongeza wanachama
ili kiwe saccos na kuwa wao kama halimashauri wako katika hatua za kuunganisha
vyama viwili vya ushirika ili waunde chama kimoja cha ushirika kilicho na nguvu
kutokana na kuwa vyama vingi vya ushirika havikopesheki kwa kukosa viongozi
walio na maadili.
No comments:
Post a Comment