Social Icons

Thursday, 26 January 2017

Wajumbe wa Baraza a Mamlaka ya Mji wa Vwawa walidhia Kuundwa Manispaa, Wataka Iitwe Manispaa ya Vwawa



Stephano Simbeye, Mwananchi

Wajumbe wa Baraza la Mamlaka ya Mji mdogo wa Vwawa wilayani Mbozi mkoa wa Songwe jana wameridhia kwa kauli moja kuunganisha mji huo na mji wa Mlowo na miji mingine ili kukidhi vigezo vya kuunda Manispaa  kwa sharti la kubadili jina.

Hayo yametokea jana katika kikao cha Baraza kilichofanyika katika ukumbi wa Mamlaka hiyo mjini Vwawa mara  baada ya Ofisa mtendaji wa Mamlaka Joel Kaminyoge  kutoa ufafanuzi wa ajenda hiyo akieleza faida za kuundwa Manispaa kuwa ni pamoja na kupata miradi mikubwa ya maendeleo.

Alisema kwa muda mrefu mamlaka hiyo imekuwa ikijitahidi ili ipande hadhi ili kufikia adhima yake ya kuwa halmashauri na kuboresha huduma kwa wananchi wake.

Hata hivyo makubaliano hayo yalifikiwa kwa tabu kufuatia wajumbe kupinga wazo la kuungana na Mlowo kwa madai kwamba huko nyuma waliwahi kuomba waunganishe miji hiyo miwili lakini wenzao wa Mlowo walikataa na kuhoji kulikoni leo huku wakilihusianisha jambo hilo na uamuzi wa eneo la kujenga ofisi ya mkuu wa mkoa ambalo kiuhalisia wajumbe hao hawakubaliani na maamuzi yaliyotolewa.

Mwenyekiti wa kitongoji cha Vwawa sekondari Damasi Mlungu alisema kuwa zaidi ya mara moja waliwafuata wenzao wa mji wa Mlowo ili kuungana na kuunda halmashauri ya mji lakini waliwakatalia kwa madai ya kutoungana na mji usiokuwa na mapato ya kutosha, kisha akahoji imekuwaje leo wanataka kuwaunganisha kwa haraka.

“ tunatambua kuwa chanzo cha jambo hili ni makao makuu ya mkoa baada ya kuona uamuzi umetolewa ofisi hizo zijengwe kwenye eneo lao sasa wanaona umuhimu wa kuunganisha miji hii, sasa sisi tunakataa bali tuendelee kupambana wenyewe ili kufikia vigezo stahili badala ya kuungana na hao” alisema Mlungu.

Naye mwenyekiti wa kitongoji cha Ilolo Ambakisye kibona alisema kwa kuwa wakazi wa Vwawa wamedharaulika hawataweza kuungana na mlowo kwa wakati huu.

Hata hivyo kufuatia wajumbe kuendelea kukataa kuridhia kuunganisha miji hiyo miwili ili kupata Manisaa moja Mbunge wa jimbo la Vwawa Japhet Hasunga alitowa ufafanuzi na uelewa kwa wajumbe kuwataka kuunga mkono wazo lililopelekwa mbele yao.

Alieleza  faida za kuwa na Manispaa kwa maendeleo yao kuwa ni pamoja na bajeti kuongezeka ili kupata maendeleo ya haraka na miradi mikubwa ya Benki ya dunia ya kuboresha miundombinu ya barabara na huduma nyingine nyingi za kijamii.

Aidha Hasunga aliwasihi wajumbe kukubaliana kuungana ili kutimiza vigezo vya kuunda Manispaa hiyo ambayo ni kwa ajili yao na kuwa ofisi zake zitawekwa katika eneo lao kwa ajili ya manufaa ya wakazi wa eneo hilo na si vinginevyo.

Naye mkuu wa wilaya ya Mbozi John Palingo aliwasihi wajumbe hao kuacha kuhusianisha ofisi za mkuu wa mkoa na uanzishaji wa manispaa na kwamba Manispaa ni yao, ndiyo yenye faida kwao ukiinganisa na ofisi ya mkuu wa mkoa

“Nashauri tukubali kuunda Manispaa ndiyo italeta maendeleo ikiwemo miradi mikubwa, lakini pia nashauri mtulie pamoja na kuwa muna hasira kutokan*--a na michakato mingi imekosewa na ndiyo chanzo chanzo cha hasira za wajumbe , lengo la kasi hii ni zuri ili kwenda na kasi ya wenzetu waliko mbali” alisema Mkuu huyo wa wilaya.

Kufuatia ufafanuzi uliotolewa na viongozi hao mwenyekiti wa Mamlaka hiyo Ephraim Mwakateba aliwahoji wajumbe wake kama wanakubaliana kuunda Manspaa ndipo walikubali kwa sharti la kutaka kubadili jina badala ya kuitwa Manispaa ya Mbozi iitwe manispaa ya Vwawa.

Aidha hasira za wajumbe hao zinatokana na kubadilishwa eneo la kujenga ofisi za mkuu wa mkoa, ambapo awali ilipendekezwa zijengwe katika mojawapo kati ya maeneo matatu ya oldvwawa, TacRi Mbimba na Hasamba yaliyopo kata ya Vwawa, lakini tofauti na hilo hivi sasa uamuzi umetolewa kuwa ofisi hizo zijengwe eneo jipya la Nselewa lililopo kata ya mlowo.
Mwisho.



No comments:

Post a Comment