Na: Stephano Simbeye, Mbozi
Serikali imeshauriwa kutatua kero
mbalimbali zinazowakabili walimu ikiwemo kuwalipa madeni yao sambamba na
kuboresha miundombinu ya kutolea elimu ili kuongeza ufaulu.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Katibu
wa chama cha walimu Tanzania (CWT) mkoa wa Songwe Emelia Mwakyoma wakati
akijadili matokeo mabaya ya mitihani ya darasa la saba na kidato cha nne mwaka
jana ambapo mkoa wa Songwe ulishika mkia, kuwa wakati zinatizamwa changamoto
zilizochangia matokeo mabaya pia litazamwe suala la walimu kutolipwa stahiki
zao ambalo linawafanya washindwe kufanya kazi kwa ari.
Katika kikao hicho ambacho
kilifanyika katika shule ya sekondari Vwawa wilayani Mbozi mkoani hapa, Mwakyoma
alisema kuwa sababu nyingine ni utoro wa walimu kutofanya kazi ingawa wanafika
shuleni lakini hawafundishi hatua ambayo usimamizi thabiti unatakiwa ili
kuidhibiti
Mkaguzi na mdhibiti wa elimu
wilayani Mbozi Jackson Lwafu alisema kudorora
elimu kunatokana na wakurugenzi wa halmashauri kutotekeleza ushauri wanaopewa
na wataalamu wa ubora wa elimu ambao hutolewa baada ya ukaguzi na kubaini mapungufu huwa haufanyiwi kazi hasa katika shule za
serikali.
Alisema baadhi ya kasoro wanazobainisha katika
ukaguzi ambazo pia huwa wanashauri wakurugenzi wa halmashauri ni pamoja na
uwiano mbovu wa ikama ya walimu ambapo kuna shule zinakuwa na walimu wengi hasa
za mjini, wakati zingine zina uhaba, mrundikano wa watoto madarasani, baadhi ya
walimu kutofundisha ingawa wanafika kazini, usimamizi mbovu na kukosekana
ufuatiliaji.
"Yote mapungufu haya tumekuwa
tukitowa taarifa lakini hayafanyiwi kazi hasa kwa shule za serikali, na mahala
pengine tinalazimika kuamuru mwalimu arudie kufundisha somo husika, na pengine
tunashauri walimu wakuu waliopo wavuliwe madaraka kutokana na udhaifu katika
usimamizi lakini yote hayafanyiwi kazi"alisema Lwafu.
Charles Chenza mi mmoja ya wadau
akichangia mawazo yake alisema kuna upungufu wa viwango vya vipimo vya malengo
ya kuongeza ufaulu, na kuwa mbali ya changamoto ya miundombinu kuna mapungufu
ya mahudhurio kwa wanafunzi na walimu.
Alisema ni vizuri ikawekwa mikakati
na alama za ufaulu wa kujipima ambazo lazima kila mwanafunzi azifikie, harafu
usimamizi uimarishwe ili kuhakikisha walimu wanahudhuria kufundisha, lakini pia
nao wanafunzi wanahudhuria ili kupata mtiririko mzuri wa masomo.
Naye mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya Momba
Adriano Jungu alisema wilaya yake ambayo imekuwa ya mwisho kati ya halmashauri
tano za mkoa huo inakabiliwa na tatizo la utoro kutokana na jamii ya wafugaji
kuhamahama na umasikini ambapo baadhi ya wazazi wanawatumia watoto ambao ni
wanafunzi kufanya vibarua ili kupata chakula.
Alitowa mfano mwaka jana ambapo wanafunzi zaidi ya 800 walisajiliwa kidato cha
nne lakini waliojitokeza kufanya mtihani ni wanafunzi 300, hata hivyo ili
kukomesha tabia ya utoro wameamua kuanzisha mahakama inayotembea (mobile court)
kuwasaka wazazi wenye watoto watoro na kuwahukumu papo hapo.
Akitoa
takwimu za ufaulu mwaka 2016 kaimu ofisa elimu mkoa wa songwe Samweli Mshana
alisema mkoa una jumla ya shule za msingi
404 zikiwemo 397 za serikali na 7 ni za binafsi
na shule za sekondari ni 104 zikiwemo 82 za serikli na 22 za watu
binafsi.
Alisema katika matokeo ya kumaliza
darasa la saba mwaka jana mkoa wa Songwe ulishika mkia kitaifa na katika
matokeo ya kidato cha nne ya mwaka jana mkoa ulishika nafasi ya 20 kitaifa
matokeo ambayo bado hayaridhishi.
Aidha akifungua kikao hicho mkuu wa
mkoa wa Songwe Chiku Galawa alipiga marufuku walimu wakuu kuja wilayani kupata
huduma mbalimbali za kiofisi badala yake aliwataka wakurugenzi na maofisa elimu
kupanga ratiba ya kutembelea vijijini na kujionea wenyewe hali ya shule zao na
kuwatatulia walimu matatizo yao kwa kufanya hivyo walimu hao watapata muda
mzuri wa kusimamia shule na kufundisha.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment