Stephano Simbeye, Mwananchi
ssimbeye@mwananchi.co.tz
MBOZI:Zao la kahawa ambalo miaka ya nyuma
lilipata umaarufu mkubwa wilayani Mbozi,mkoani Songwe limeanza kupoteza
umaarufu, huku vijana wakisusa kujishughulisha nalo, badala yake wakulima
wamejiingiza zaidi kulima mahindi na mazao mengine ya nafaka
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya
wakulima, walisema kuwa zao hilo limepoteza mvuto kiuchumi kutokana na
kukabiliwa na matatizo mengi likiwemo soko la uhakika,magonjwa na ukame, hali ambayo imekuwa chanzo cha kuwarudisha
nyuma badala ya kuwainua kiuchumi.
Laurent Mgala ni mkulima toka kijiji cha Ibembwa alisema zao la kahawa
linakabiliwa na magonjwa matatu makubwa ambayo yamekuwa kikwazo katika
uzalishaji nayo ni pamoja na ugonjwa wa mizizi ambao unakausha mibuni, Chulebuni na kutu ya majani na kuwa magonjwa
hayo yanarudisha nyuma jitihada zao.
Alisema mbali na magonjwa hayo pia kuna
mdudu ambaye amekuwa akitoboa mibuni na kufanya ikauke, jambo jingine ni
mabadiliko ya tabia nchi ambayo yanafanya ukame wa muda mrefu ambapo zao hilo
linahitaji maji mengi wakati wa kuchavusha, kukomaza punje na hata wakati wa
kuchakata, lakini kutokana na ukame wanakosa maji ya kumwagilia kwa kukosa
mabwawa.
Amosi Kibona mmoja wa vijana alisema ni
vigumu kwa vijana kujiingiza kwenye kilimo cha kahawa kwa kuwa hakilipi, bali
wanaweza kufanya biashara ya kununua na kuuza kahawa badala ya kulima pia zao
hilo linahitaji uwekezaji wa muda mrefu tofauti na mazao ya nafaka.
“ hatuwezi kujiingiza kwenye kilimo cha
kahawa kwani tunaona wazee wetu jinsi ambavyo wanahangaika bila ya mafanikio
yoyote tofauti na miaka ya nyuma” alisema Kibona
Kwa upande wake Meneja wa kituo cha Taasisi
ya Utafiti wa kahawa nchini (TaCRi) kilichopo Mbimba wilayani hapa Isaac Mushi
alikiri zao la kahawa kukabiliwa na changamoto ya mabadiliko ya tabia nchi
ambapo kuna kiangazi cha muda mrefu ambacho kinaathiri zao hilo.
Sambamba na hilo ili kuongeza uzalishaji na
kukabiliana na magonjwa sumbufu Mushi alishauri wakulima kupanda miche mipya
iliyofanyiwa utafiti na taasisi yake inayokinzana na magonjwa hayo sumbufu.
Aidha aliongeza kuwa hivi sasa taasisi hiyo
inaendelea na utafiti ili kupata miche ambayo inastahimili ukame ili kunusuru
na kufanya uzalishaji uongezeke .
Mkulima toka Isansa ambaye pia ni diwani wa
kata hiyo Emir Mzumbwe alisema wanakosa mvua za vuri zinazotarajiwa kuanza
Septemba hadi Novemba ambazo zingesaidia kuchavusha, lakini kukosekana kwa mvua hizo ni chanzo cha
zao kuporomoka na kutokuwa na tija.
Alisema iwapo halmashauri haitachukua hatua
za makusudi kujenga mabwawa ya umwagiliaji zao linakufa na itabaki historia,
alitoa mfano katika bajeti ijayo kuwa fedha iliyotengwa kuendeleza zao hilo ni
Sh. 75milioni na mwaka jana zilitengwa Sh. 60milioni hali ambayo inatishia
usalama wa zao.
Kwa upande wake kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya
Mbozi Elisey Ngoi alikiri kuwa uzalishaji wa kahawa unayumba kulingana na msimu
kuwa iwapo mvua za vuri zikinyesha vizuri uzalisaji huongezeka na zikiwa mbaya
unashuka, alitowa mfano kuwa katika msimu 2015/2016 uzalishaji ulikuwa tani
15260, lakini msimu wa 2016/2017 ulishuka hadi tani 8558 na msimu 2014/2015
tani 7665.
‘ tunawahamasisha wananchi watunze vyanzo vya maji ili
kulinda uzalishaji na kuondokana na kutegemea mvua kwa asilimia kubwa” alisema
Ngoi.
Aidha aliongeza kuwa halmashauri inatambua umuhimu wa
mabwawa ya umwagiliaji, lakini alisema ili kufanikisha hilo panahitajika
utafiti wa kutosha na fedha nyingi, hata hivyo alisema tayari mabwawa mawili
yamechimbwa katika vijiji vya Msia na Hamwelo na kuwa wataendelea kuchimba
mabwawa zaidi kadiri watakavyokuwa wakipata fedha.
Zaidi ya asilimia 70 ya mapato ya ndani ya halmashauri hiyo ambayo ni zaidi ya Sh. 3.5 bilioni yanatokana
na pato la zao la kahawa, lakini fedha inayotengwa ili kuboresha zao hilo ya
Sh. 75milioni ni kidogo.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment