Social Icons

Friday, 24 February 2017

Wafanyabiashara Vwawa Wamuweka kiti Moto Mwenyekiti wa CCM

Stephano Simbeye, Mbozi

Mvutano wa eneo la kujenga ofisi ya mkuu wa mkoa wa Songwe umeingia katika sura mpya baada ya  jumuia ya wafanyabiashara mjini Vwawa kukihoji chama cha Mapinduzi kwa kushindwa kutolea tamko suala la eneo la kujengwa ofisi za mkuu wa mkoa badala ya Vwawa ilikoamliwa awali na kupelekwa Selewa
 
Mwenyekiti wa Jukwaa la wafanyabiashara Yohana Mwajeka Akitoa utangulizi katika kikao kilichofanyika  katika ukumbi wa Moravian Vwawa mjini wilayani Mbozi mkoani hapa alisema mchakato ulipokamilika wa kuanzishwa  mkoa wa Songwe lilitolewa tamko  na viongozi wa juu wa serikali ya awamu ya nne kuwa makao makuu yatakuwa kata ya Vwawa, pia suala hilo lilinadiwa kama moja ya mambo yaliyotekelezwa na Mbunge aliyemaliza muda wake Godfrey Zambi ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mbeya.

Alisema kinachowafanya wahoji suala hilo ni kutokana na mabadiliko yaliyotokea ya kubadilisha eneo la kujenga ofisi za mkuu wa mkoa badala ya kata ya Vwawa yamepelekwa Selewa iliyopo kata ya Mlowo jambo ambalo wao wanaona ni ukiukwaji wa matamko ya viongozi wa juu.

 Edward Mahenge (Ndisana) alisoma bango lililoandikwa na Mbunge aliyemaliza muda wake Godfrey Zambi likieleza utekelezaji wa Ilani ya CCM kuwa eneo la Vwawa amefanikiwa kuanzisha mkoa mpya wa Songwe na makao makuu yatakuwa Vwawa.

"Tulipoambiwa hapa patakuwa makao makuu tulijiandaa kutumia fursa hiyo kuwekeza, sasa tunakohoji Mwenyekiti kuwa chama kilitudanganya, kama sivyo nani kabadilisha tamko lililotolewa na Rais" alihoji Mahenge

Isaya Mwakidodi alisema Rais John Magufuli wakati wa kampeni za uchaguzi mwaka juzi aliwaahidi wanavwawa kuwa mkoa mpya unaanzishwa na kuwa makao makuu yatakuwa Vwawa na pia aliahidi kutengeneza barabara  yenye urefu  wa kilometa kumi kwa kiwango cha lami lakini wanaona kauli ya Rais na Waziri  mkuu Mmstafu Mizengo Pinda zimebadilishwa huku chama kikiwa kimywa.

Akijibu hoja za wafanyabiashara hao Mwenyekiti wa Chama cha Mapindizi wilaya ya Mbozi Aloyce Mdalavuma alikiri kuwapo na kauli za ahadi za viongozi wakuu wa nchi kama Waziri Mkuu mstaafu Mizengo Pinda na Rais John Pombe Magufuli alitoa ahadi ya Vwawa kujengwa ofisi ya mkuu wa mkoa na kwamba chama hakiwezi kuwa tofauti na Mwenyekiti wake wa taifa.

Alisema chama cha Mapinduzi wilayani Mbozi kilishiriki katika uanzishaji mkoa wa Songwe na kushiriki mapendekezo ya maeneo matatu ya Oldvwawa, Mbimba na Ilembo/Hasamba lakini eneo la nne laSelewa hakikushiriki.

Sakata la mgogoro wa kugombea eneo la kujenga ofisi za mkuu wa mkoa wa Songwe lilianza mwishoni mwa mwezi Desemba mwaka jana mara baada ya kamati ya ushauri mkoa (RCC) kuazimia ofisi hizo kujengwa eneo la Selewa lililopo kata ya Mlowo, badala ya kata Vwawa kama ilivyoahidiwa wakati wa mchakato.
 
Tayari makundi mbalimbali yameanza harakati za kugombania maeneo haya ambapo wiki iliyopita wafanyabiashara na wadau wa mji wa Mlowo walikutana katika kikao ambapo waliazimia kuunda kamati ya watu 15 ambao watafuatilia kuona pendekezo la ofisi za mkoa kujengwa Selewa yanabaki kama yalivyo.
Mwisho.

No comments:

Post a Comment