Na: Stephano Simbeye, Mbozi
Wananchi wa vitongoji vya Mantengu A
na B pamoja na Mwenge wilayani Mbozi mkoani Songwe wameiomba serikali
kukamilisha ujenzi wa daraja linalounganisha vitongoji hivyo kwenda makao makuu
ya wilaya ambako zinapatikana huduma za jamii baada ya daraja hilo kutelekezwa
likiwa ,inajengwa kupitia mpango wa TASAF II iliyotoa zaidi Sh. 26 milioni.
Wakizungumza jana na gazeti hili
wakazi hao walisema serikali kupitia halmashauri ya Mbozi imewatenga kwa
kutowapelekea huduma muhimu za jamii ikiwa ni pamoja na barabara na vivuko na kufanya
wananchi hao hususani wanawake wajawazito na wanafunzi kushindwa kuvuka hasa
kipindi cha mvua ambapo maisha yao yanakuwa hatarini. Habari zaidi ingia
songwemedia.
Vumilia Kabongo mkazi wa kitongoji
cha Mantengu A, alisema wanapata adha kubwa hasa wanapovuka kwenda kuzika
upande wa pili yalipo makaburi na kulazimika kuzunguka njia ndefu zaidi ya
kilometa 20 badala ya kilometa mbili (2) huku kikwazo ikiwa ni ukosefu wa
daraja.
Steven Simwembe alisema
walitangaziwa kuwa zimetengwa Sh. 26 milioni kwa ajili ya kujenga daraja hilo
ambalo tangu watangaziwe na kazi ya ujenzi kuanza na ghafra ukatelekezwa na
sasa imepita miaka saba na kupelekea adha kubwa ya mawasiliano katika maeneo
hayo mawili kwenda kupata huduma makao makuu ya wilaya ambako kuna hospitali ya
wilaya, soko na shule ya msingi na sekondari Vwawa.
Mmoja wa wanafunzi Daniel Kalinga
kutoka kitongoji cha Mantengu B alisema wanalazimika kukosa masomo katika
kipindi cha mvua kutokana na mto kujaa, hivyo aliiomba serikali kukamilisha
daraja hilo haraka ili kuondoa usumbufu wanaoupata.
Florida Chaming’ombe mkazi wa
matengu A alisema wakati anaelekea hospitali ya wilaya kwa ajili ya kujifungua
alijikuta anajifungulia njiani kufuatia kupita njia ndefu kwa kuhofia kufa,
kuepuka kupita kwenye daraja hilo ambalo wakati huu wa masika mto umejaa.
Mwenyekiti wa kitongoji cha Mwenge
Abraham Kalonge alikiri kuwepo kero ya mawasiliano katika eneo hilo na kuwa
wamekuwa wakilipigania suala hilo katika vikao mbalimbali vya mamlaka ya mji wa
Vwawa pasipo mafanikio na kuiomba serikali kuliangalia tatizo hilo kwa jicho la
tatu ili kunusuru maisha ya watu.
Kwa upande wake Kaimu mkurugenzi wa
halmashauri ya wilaya ya Mbozi Erisey Ngoi licha ya kukiri daraja hilo
kutengewa kiasi hicho cha fedha huko nyuma, alisema fedha hizo hazikutosha
kukamilisha na kwamba halmashauri imeandaa mpango mkakati ili kumalizia daraja
hilo ambalo kazi iliyosalia ni kumimina zege la juu.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment