ssimbeye@mwananchi.co.tz
MOMBA: Wakulima wa kata ya Msangano katika
wilaya ya Momba mkoani Songwe, wameingiwa na hofu ya kukumbwa na njaa msimu
ujao, baada ya mazao ya mpunga na mahindi waliolima mwezi Desemba kukauka
kufuatia kukosekana mvua za vuri za mwezi January na Februari mwaka huu.
Baadhi ya wakulima waliohojiwa na
mwandishi wa habari hizi walisema mvua za vuri zilianza kunyesha mwezi Desemba badala
ya Novemba kama ilivyozoeleka ambapo walianza kulima na kupanda mahindi na kusia
mbegu za mpunga kwenye vitaru, hata hivyo baada ya kuota mvua haikunyesha mwezi
mzima wa Januari hadi wiki ya tatu ya mwezi Februari ambapo tayari mazao
yalikuwa yamekauka.
Mkazi wa kijiji cha Ntinga Emanuel
Sinkamba alisema hali ya ukame imewafanya washindwe kuelewa hatima ya maisha
yao kutokana na kuwa fedha waliyokuwa nayo waliitumia kujiandaa na kilimo hicho
ambapo sasa mazao yamekauka na kutokana na hali ngumu wanashindwa kuzitumia
mvua zinazonyesha sasa kupanda mazao mengine ya muda mfupi.
"Tunaomba tusaidiwe mbegu za
mtama za muda mfupi ili tutumie mvua zinazoendelea sasa kupanda mazao ya muda
mfupi" alisema Sinkamba.
Mwenyekiti wa kijiji cha Msangano
Simon Sichalwe alisema kutokana na ukame ambao umeathiri mazao yao hali ya
chakula kijijini hapo itakuwa ngumu msimu ujao kutokana na kuwa hawatavuna kama
inavyokuwa miaka mingine.
Alisema mazao wanayolima katika eneo
hilo ni pamoja na Mpunga na mahindi ambayo huanza kupandwa mwezi Novemba kila
mwaka na kuwa inapofika mwezi Machi na April yanakuwa yamekomaa, lakini hali ni
tofauti mwaka huu ambapo mvua zilichelewa kuanza na pia zilisimama kwa muda mrefu
kati ya Januari na Februari.
Kaimu ofisa kilimo wilayani Momba
aliyejitambulisha kwa jina moja la Kiondo akizungumza kwa njia ya simu alikiri
kuwapo ukame katika vijiji vitatu katika kata ya Msangano, ambavyo ni Msangano,
Ntinga na Ipata na kijiji kimoja cha Nkara katika kata Chitete hata hivyo
alisema wanawahamasisha wakulima kuanza kupanda mazao yanayostahimili ukame na
yanayokomaa kwa muda mfupi kama mtama na mihogo.
Kuhusu takwimu halisi za hasara na
uzalishaji uliotokea, alisema hawezi kuzitoa kwa vile yuko nje ya ofisi kikazi
hata hivyo aliongeza kuwa ukame huo ungeathiri pia kata nzima ya Chitete lakini
kutokana na kuwepo mradi wa umwagiliaji wa Naming’ongo umesaidia wakazi wengi
wa kata ya Chitete kulima mazao yao kwa kumwagilia.
Jitihada za kumpata Mkurugenzi Mtendaji
halmashauri ya wilaya Momba Adriano Jungu ili kuzungumzia madhara yaliyosababishwa
na ukame huo, na jitihada za halmashauri hiyo kusaidia upatikanaji wa mbegu za
mtama na mhogo hazikuzaa matunda baada ya kutopokea simu yake ya mkononi kwa
muda mrefu na hata alipoandikiwa ujume mfupi wa maneno (SMS) hakujibu lolote.
Aidha eneo hilo ndilo linalotegemewa
kwa uzalishaji wa mpunga ambao hulisha maeneo ya Tunduma, Mbalizi (Mbeya
vijijini) na maeneo ya Mlowo na Vwawa katika wilaya ya Mbozi, hivyo
yatakabiliwa na upungufu wa mpunga.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment