Na: Stephano Simbeye, Mbozi
Juhudi za serikali za kukomesha
pombe kali za viroba huenda zikakwama baada ya baadhi ya wafanyabiashara
wilayani Mbozi mkoa wa Songwe kubuni njia mpya ya kuuza vinywaji hivyo
vilivyopigwa marufu kwa kuvibatiza majina mapya ya Sub Ufa, Samaki mkavu au
maziwa.
Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hizi
kwa siku tatu wilayani hapa katika maeneo mbalimbali yanayouza vinywaji hivyo,
imeshuhudiwa kuwa wahudumu wa maeneo hayo wanawafahamu wateja wao ambao
wakifika hutamka majina hayo na kisha kupewa huduma kimya kimya.
Neema Mwampashe mmoja wa wamiliki
hao aliiomba serikali kuwaongezea muda ili waviondoe viroba hivyo kwa kuwa
biashara zao wanaendesha kwa fedha za mkopo ambapo wamekuwa wakirejesha kila
mwezi baada ya mauzo na wao wanategemea zaidi biashara hiyo ambayo inawapatia
faida kubwa.
Mmoja wa wateja waliokutwa
wakijipatia kinywaji hicho Daniel Simwinga mkazi wa Vwawa alisema kuviondoa
viroba vitawapa wakati mgumu kutokana na kuwa vimekuwa vikiuzwa kwa bei nafuu
ambayo wao wenye kipato kidogo wanamudu gharama za kuvinunua.
Alisema wanaiomba serikali kutafuta
njia mbadala ya kuviweka viroba hivyo kwenye chupa na kuuza kwa bei nafuu ili
waweze kumudu kuvinunua kwa kuwa pombe hiyo si haramu bali kinachokatazwa ni
karatasi.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya
wafanyabiashara wilaya ya Mbozi Yohana Mwajeka (JEKAS) alikiri kuwa
wafanyabiashara wamebadilisha majina ya vinywaji hivyo na kusema kuwa ili
serikali ifanikiwe kudhibiti biashara hiyo itumie busara kwa kuwajali
wafanyabiashara kwa kuongezea muda wa kuviondoa viroba sokoni.
Alisema ilitakiwa viroba hivyo
virudishwe viwandani ili vikawekwe kwenye chupa na kurudishwa sokoni badala ya
kuvikataza ili hali wengi walikuwa na shehena kubwa ambayo ililipiwa na kodi
stahiki za serikali vikiwa tayari vimewekwa nembo ya ubora toka shirika la
viwango nchini (TBS).
Aidha mwanzoni mwa mwaka huu
serikali kupitia kwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kasim
Majaliwa aliagiza kwamba ifikapo Marchi mosi mwaka huu vinywaji hivyo viwe
vimeondoka sokoni ili kunusuru vijana wengi ambao wamekuwa wakivinunua kwa bei
ya chini na kunywa nyakati zote pasipo kufanya kazi, tangu tarehe hiyo
mamlaka husika zimekuwa zikifanya msako na kukamata pale wanapopata bidhaa hiyo
inauzwa.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment