Stephano Simbeye, mwananchi
MBOZI: Mbunge wa jimbo la Mbozi
mkoani Songwe, Pascal Haonga (Chadema) amewasomea wapiga kura wake taarifa ya
mapato na matumizi ya fedha za mfuko wa jimbo zaidi ya Sh.76milioni alizopata
kwa awamu mbili tangu achaguliwe kushika wadhifa huo mwaka 2015 kitendo ambacho
hakijawahi kufanywa na watangulizi wake.
Hatua hiyo aliifanya jana katika
hafla ya kukabidhi kisima alichokichimba katika mji wa Mlowo wilayani hapa
ambapo alisema fedha za mfuko wa Jimbo si mali ya Mbunge bali zinatokana na
kodi zao, hivyo ni lazima wapate taarifa ya jinsi zinavyotumika na kuwa
serikali inatowa fedha hizo ili kuchochea na kuchangia nguvukazi katika miradi
ya wananchi.
Haonga alisema mwaka jana mfuko huo
ulipokea Sh. 33milioni ambazo alizielekeza katika miradi ya kuweka vifaa vya
umeme jua katika zahanati pamoja na kukamilisha vyumba vya madarasa katika
vijiji 17, ili kuunga mkono nguvu za wananchi ambao walijenga kufikia hatua ya
mtambaa panya pamoja, kujenga daraja la kuunganisha vijiji vya Shasya na
Halungu na kununua tenki la kuhifadhia maji katika kijiji cha Igamba.
Akizungumzia fedha nyingine ya mfuko
wa jimbo ambayo imepokelewa hivi karibuni kiasi cha Sh.43 milioni alisema fedha
hizo zitatumika kukamilisha vyumba 21 vya madarasa na ofisi 3 za walimu, nyumba
2 za walimu, kukamilisha majengo 5 ya zahanati na vyoo matundu 18 na kununua
vifaa vya umeme jua katika zahanati ya Iwalanje.
Akizungumzia kisima cha maji
alichokizindua katika mji mdogo wa Mlowo Haonga alisema kimegharimu zaidi ya
Sh. 11milioni fedha ambazo zaidi ya sh. 10.4 milioni zimetoka mfukoni mwake, na
Sh. 660000 zimetolewa na serikali ya kijiji.
Mmoja ya wakazi wa Mlowo Onesmo
Kapungu alisema kitendo cha Mbunge huyo kuwasomea taarifa ya mapato na matumizi
wananchi wake kimeonesha njia kwa watendaji wengine kufanya hivyo na kuwa
hakuna mbunge aliyewahi kufanya hivyo.
Naye Rahel Lyanda alisema Mbunge
ameonesha njia kwa wengine kufuatia uamuzi wake wa kuwafafanulia na kuwajulisha
juu ya fedha zao za mfuko wa jimbo ambazo hawajawahi kufahamu kama zinaingia
ngapi na zinatumikaje.
Mganga mfawidhi wa Zahanati ya Mlowo
Semeni Mswima ambako kilizinduliwa kisima kwa ajili ya kuwapatia huduma ya maji
wagonjwa na wakazi wa jirani na eneo hilo, alisema maji hayo yatasaidia
kupunguza kero ya maji wanayopata kwa ajili ya shughuli mbalimbali ikiwemo
kunywa.
Aidha mganga huyo alisema katika
zahanati hiyo wengi wanaofika kupata matibabu wanasumbuliwa na magonjwa
yanayotokana na kunywa maji yasiyosafi na salama ya kuhara, homa ya matumbo na kuhara
damu.
Mwisho
No comments:
Post a Comment