WATU wasiofahamika wamefukua kaburi
la mlemavu wa ngozi [ALBINO] kisha kuchukua mifupa na kubakiza fuvu la kichwa na kutokomea
kusikojulikana, katika kijiji cha Nansama kata ya Isansa wilayani Mbozi mkoani
Songwe.
Akisimulia mkasa huo jana, shemeji
wa marehemu Sala Kamwela, alisema shemeji yake alifariki Marchi 28 mwaka 2011
akiwa na umri wa miaka 50 ambapo jana alisema alishangazwa kuona kaburi lake lililosakafiwa
na saruji lilikutwa limefukuliwa na kuondolewa mifupa wakibakiza fuvu la
kichwa.
Alisema baada ya tukio hilo,ambalo
waliligundua wakati wanarudi kutoka shamba,wakalazimika kutoa taarifa kwa
Mwenyekiti wa kitongoji na kijiji na hatimaye polisi kwa kushirikiana na
serikari ya kijiji ambayo ilifika eneo la tukio wakiwa na daktari na mara baada
ya uchunguzi walizika upya fuvu hilo na masalia mengine.
Akizungumzia tukio hilo mjumbe wa
kamati ya kijiji,Baraka Ntenga,alisema marehemu alikuwa ndugu yake anasikitika
kuona kaburi limefukuliwa na kuwa anaomba jeshi la polisi liwasake waliohusika
kufukua kaburi hilo.
Alisema tukio hilo ni la kwanza
kutokea katika kijiji chao na kuwarudisha nyuma kipindi cha matukio ya
uchunaji ngozi za binadamu ulioshamili wilayani mbozi ambayo yalihusishwa na
imani za kishirikina,kwa sasa yametoweka .
Kamanda wa polisi mkoani
Songwe,Mathias Nyange amthibitisha kutokea tukio hilo,na kusema limetokea usiku
wa kuamkia jana na kuwa jeshi lake linaendelea kuwasaka waliohusika na tukio
hilo.
Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na
usalama mkoani humo,Luteni mtaafu, Chiku galawa,alisema vitendo hivyo vinapaswa
kukemewa kwa nguvu zote kutokana na kuhusishwa na imani za kishirikina na kuwa
ikiwa wanafukuwa makaburi wataweza kuwafuata walio hai na kuwaangamiza.
Galawa ambaye pia ni mkuu wa mkoa
huo, alisema atawasiliana na machifu na viongozi wa dini zote kushirikiana na
serikali kupiga vita matukio hayo yanayohusishwa na imani za kishrikina.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment