Stephano Simbeye, Mbozi
Vijana wameilalamikia
halmashauri ya wilaya ya Mbozi mkoani Songwe, kuwa na milolongo mirefu ya
utoaji mikopo kwa vijana na wanawake hali inayowakatisha tamaa na kusababisha washindwe
kujikwamua kiuchumi.
Malalamiko hayo yalitolewa jana
mjini Vwawa wakati wa uzinduzi wa mradi wa ushirikishwaji vijana katika sekta
ya kilimo na ufugaji utakaowanufaisha zaidi ya vijana 2000 wilayani hapa
katika kipindi cha miaka mitano tangu 2016 hadi 2021 unaoendeshwa na shirika la
Heifer International ambapo watapatiwa stadi za mafunzo ya ujasiriamali kwa
vitendo.
Jakob Mkisi ni mmoja wa vijana hao
alisema kundi la vijana bado ni tegemezi lisilomiliki rasimali yoyote, huku
likabiliwa na ukosefu wa ajira wakati wengi wao wakiwa ndiyo kwanza wametoka
masomoni kuwa kundi hili linahitaji uwezeshi na uangalizi wa aina yake ili
kuweza kujikomboa kiuchumi kwa kujiajiri ili nao waweze kutoa mchango kwa pato
la taifa.
Alisema kutokana na uchanga wao
wanakosa kujiamini katika kusimamia mambo mbalimbali ambayo yatawasaidia
kuiandaa kesho yao kwa kufanya kazi leo kutokana na wengi kutaka utajiri wa
haraka, pia changamoto ya kuwapo na milolongo mirefu ya upatikanaji wa huduma
inawakatisha tamaa na ukosefu wa njia sahihi ya upashanaji habari wanajikuta
wanaingia katika makundi yasiyo sahihi.
Peter Mwansite ni kiongozi wa kundi
la vijana la Focus Forward akizungumzia tatizo la ajira kwa vijana alisema ni
vema wazazi wakaona umuhimu wa kuwapatia rasilimali kidogo ambazo zitawasaidia
kuanzishia miradi ya kujiajiri huku mamlaka husika zikisaidia kuwaondolea
urasimu wa upatikanaji mikopo na kuwapatia stadi za mafunzo stahiki.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa
halmashauri ya wilaya ya Mbozi Elick Ambakisye alisema halmashauri yake
imeupokea mradi huo kwa mikono miwili na kuwa itatoa ushirikiano wa dhati
kuhakikisha malengo yake yanatimia kwa kufanya kazi bega kwa bega na Shirika na
makundi mbalimbali ya vijana ili kuwakwamua na tatizo la ukosefu wa ajira.
Aidha alisema zipo changamoto nyingi
zinazojitokeza katika utoaji wa mikopo ya vijana na wanawake, ikiwemo kushindwa
kurejesha mikopo na kuwa hata hivyo halmashauri imejipanga upya kuona hilo
halijitokezi.
Naye Mkuu wa mkoa wa Songwe Chiku
Galawa akizungumza katika hafla hiyo ya uzinduzi wa mradi aliziagiza
halmashauri mkoani humu kutenga maeneo ya kutosha kwa ajili ya vijana ambapo
alisema utengaji wa maeneo uende sambamba na kuhakikisha asilimia 10 ya
makusanyo ya mapato yake zinakwenda kwa makundi ya vijana na wanawake.
Aidha Galawa alisema fedha hizo
hazitolewi kwa hiari bali ni lazima na ni haki ya makundi husika hivyo
halmashauri ambayo itashindwa kufanya kutoa fedha hizo mkurugenzi
atawajibishwa.
Kwa upande wake Kaimu Meneja wa
Shirika la Heifer International Damas Damiani alisema mradi huo unalenga
kuwajengea stadi za ujasiliamali vijana wenye umri kuanzia miaka 18 hadi 24
kundi ambalo limekuwa halijihusishi na kilimo na ufugaji ili nalo liweze kuona
kuwa sekta hiyo inaweza kuwapatia ajira na kuwaongezea kipato.
Alisema vijana hao watapangwa katika
makundi mbalimbali kulingana kazi watakazochagua wenyewe kuzifanya na kisha
baada ya hapo watakuwa wakipatiwa mafunzo na stadi mbalimbali za uzalishaji
mali
Mwisho.
No comments:
Post a Comment