Na Stephano Simbeye, Mbozi
Wafanyabiashara katika mji wa Vwawa
wilayani Mbozi mkoani Songwe, wameiomba serikali kuufungua mji huo na maeneo
mengine kwa kuboresha miundombini ya barabara ili kurahisisha mawasiliano katika
usafirishaji na uchukuzi ili kusaidia kuvutia wawekezaji.
Kilio hicho kiliwasilishwa jana katika
mkutano uliofanyika mjini hapa kwa Mbunge wa jimbo la Vwawa Japheti Hasunga (CCM)walipokuwa
wakiwasilisha kero zinazowakabili na Greenwell
Nsyukwe (Jack Msafwa) ambaye
alisema mji huo umekuwa kisiwa licha ya kuwa ni makao makuu ya mkoa kutokana na
kukosa mawasiliano ya uhakika na maeneo mengine jirani hali ambayo inasababisha
ufanyaji wa biashara kuwa mgumu.
"Mheshimiwa Mbunge hebu tusaidie
kufungua barabara za kuingia katika mji wetu ambapo zilizopo ni chafu zisizopitika
wakati wote na kufanya kuwa kero kwetu inayotufanya tushindwe kufanya
biashara" alisema Greenwell.
Alitaja baadhi ya njia ambazo endapo zikiboreshwa
zitarahisisha mawasiliano kuwa ni pamoja na barabara ya Ilembo Mahenje hadi Kimondo, Hasamba Nyimbili hadi
Ileje, Hasamba Izyila hadi Mbeya vijijini na Igamba Mbozi Club ambazo ni muhimu
kwa uchumi wa mji huo.
Nivard Lwila alisema mji huo umezorota
kibiashara kutokana na kuwa hauna wageni wanaoingia kutokana na kutokuwa na
barabara zinazopitika wakati wote huku serikali ikiwa haijaonesha mikakati
yoyote ya kuboresha barabara hizo.
“ tumejiandaa kuwekeza ili tuzitumie fursa
za kuanza kwa mkoa mpya lakini bado kikwazo ni miundombinu ambayo ni muhimu kwa
ajili ya usalama vyombo vya uchukuzi na mji wowote ule unahitaji mawasiliano
ili watu wake kujiletea maendeleo lakini hapa tunakosa huduma hiyo” alisema
Lwila.
Naye mfanyabiashara Edward Mahenge
(Ndisana) alieleza kusikitishwa kwake jinsi sheria ya zimamoto inavyotekelezwa
kwa kuwalazimisha kutoa fedha za ada pasipo kuelimishwa, badala yake watendaji
wake wamekuwa wakipita kwenye biashara zao wakiwa na askari Polisi huku
wakiacha vitisho ukuki.
“ tunaona huu ni ubabe usio na msingi
wanafika kwenye biashara kudai fedha wakati hata huduma yenyewe ya zimamoto
hatuioni kwanini kusiwekwa utaratibu wa kutekeleza mambo kama haya ili mtu
aelewe anatoa fedha kwa ajili gani”alisema Ndisana.
Akijibu hoja za wafanyabiashara hao Mbunge
Hasunga alikiri kutambua kero hiyo, lakini alisema neema ya kuanzishwa kwa mkoa
wa Songwe itasaidia kuwepo kwa wakala wa barabara (TANROAD) ambao inapata
fedha nyingi za matengenezo ya barabara ukilinganisha na halmashauri ambao
zitasaidia kutengeneza barabara hizo ili zipitike wakati wote.
Alisema mipango ya mkoa ni kufungua njia
tatu muhimu ambazo ni pamoja na barabara ya Mbozi Club kupitia Igamba hadi
Mkwajuni wilayani Songwe, barabara ya Vwawa kupitia Nyimbili Hezya hadi Ileje
na barabara ya Ihanda Chindi hadi Chitete wilayani Momba, na kuwa iwapo
barabara hizo zitafunguka zitasaidia kurahisisha mawasiliano mkoani hapa na pia
kuufungua mji wa Vwawa.
Aidha Hasunga aliwataka wafanyabiashara hao
kuanza kuchangamkia fursa za ujio wa wageni wataalamu mbalimbali wamaoletwa
kuja kufanya kazi mkoani hapa, kwa kujenga nyumba nzuri za kupangisha ili
wajiongezee kipato na fursa nyingine ni ya kuwa wageni hao watahitaji vyakula
na mahitaji mengine ya kibinadamu.
Naye
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya Mbozi Elisey Ngoi alisema katika
bajeti ya halmashauri hiyo mwaka ujao wa 2016/2017 imeweka vipaumbele vitatu
ambavyo ni kujenga barabara na madaraja, kukamilisha vyumba vya madarasa na
zahanati vilivyojengwa na wananchi na kulipa madeni ya wazabuni wake, hali
itakayofanya mji huo kuwa na barabara zinazopitika wakati wote.
Aidha mji wa Vwawa ambao ni makao makuu ya
mkoa wa Songwe unakabiliwa pia na changamoto ya barabara za mitaa zenye hadhi
ya makao makuu ya mkoa
Mwisho.
No comments:
Post a Comment